Dar es Salaam. Ukienda mjini leo, unaweza kuhisi ni sikukuu au mwisho wa juma (weekend), baada ya barabara kufungwa kutokana na ugeni wa marais na viongozi mbalimbali wanaoshiriki mkutano wa kimataifa wa Nishati unaoanza leo, Januari 27, 2025 jijini Dar es Salaam.
Ilivyozoeleka siku ya Jumatatu katikati ya mji, kuna mishemishe na purukushani za hapa na pale, lakini hali ni tofauti leo, kwani watu si wengi kama ilivyo kawaida, na kimya kimetawala maeneo mbalimbali.
Baadhi ya maduka yamefungwa, na maeneo kama Kariakoo hakuna msongamano wa magari; hata bajaji ni ngumu kuzipata, ingawa bodaboda wapo wawili watatu.
Hali hii inaweza kudumu kwa siku hizi mbili za mkutano huu, ambao unafanyika Tanzania, ukiwa ni mkutano wa kwanza kuwakutanisha marais zaidi ya 20 kwa mara moja.
Tangazo la Jeshi la Polisi lililotolewa Jumamosi Januari 25, 2025 na Kamanda Kanda Maalumu ya Polisi Dar es Salaam, Jumanne Muliro, lilieleza kuwa kutokana na ugeni wa viongozi watakaokuja kwenye mkutano, barabara zitafungwa.
Barabara zilizofungwa ni Nyerere, kutokea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kuelekea katikati ya Jiji. Nyingine ni Barabara ya Sokoine, Kivukoni na Lithuli, kuanzia taa za Gerezani kuelekea Hoteli ya Johari Rotana, Hyatt Regency hadi Ikulu.
Pia, Barabara ya Ohio kutokea Kivukoni kuelekea Hoteli ya Serena, na ile ya Ghana kutokea barabara ya Ohio kuelekea Hoteli ya Onomo.
Vilevile, Barabara ya Bibi Titi, kutokea makutano ya Barabara za Ohio na Ally Hassan Mwinyi, kuelekea Hoteli ya Crowne, na Barabara ya Azikiwe kuelekea Hoteli ya Four Points, Hoteli ya Golden Tulip City Center na Hoteli ya Holiday Inn.
Pia, Barabara ya Morogoro kutokea Sokoine kuelekea Hoteli ya Tiffany No. 1, na ile ya Makunganya kutokea Azikiwe kuelekea Hoteli ya Tiffany No. 2.
Aidha, Barabara ya Garden kutokea Barabara ya Lithuli kuelekea Hoteli ya Southern Sun, pamoja na Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa JNICC, nayo itafungwa kutokana na ugeni huo.