Mkutano wa nishati: JNICC kumeanza kuchangamka

Dar es Salaam. Mambo yameanza kuchangamka katika viunga vya kituo cha mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), unakofanyika mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika kuhusu nishati.

Kabla ya ratiba rasmi ya wahudhuriaji kuingia ukumbini, tayari burudani mbalimbali zimeanza kushuhudiwa nje ya kituo hicho.

Ngoma ya Msewe, yenye asili yake Unguja visiwani Zanzibar, ndiyo iliyofungua milango ya rasharasha za burudani katika eneo hilo, huku Wamasai nao wakiruka na kupandisha mori.

Kama ni mpenda burudani, nje ya ukumbi pekee kungemaliza shida zako. Ngoma ya Mganda kutoka Ruvuma haikukosekana.

Kilichowaweka wengi nje ya ukumbi ni aina mbalimbali ya minenguo iliyoshuhudiwa na kila kikundi cha ngoma za asili nje ya ukumbi huo.

Naam, ni shamrashamra zinazowakaribisha wakuu wa nchi 25 kutoka mataifa ya Afrika, wanaokutana katika kituo hicho kujadili mustakabali wa nishati Afrika.

Mkutano huo, ambao ni matokeo ya azimio la Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Benki ya Dunia, unalenga kutoa azimio litakalowezesha Waafrika milioni 300 kufikishiwa huduma ya umeme ifikapo 2030.

Katika mkutano huo wa siku mbili, kuanzia leo Jumatatu, Januari 27, 2025, unatanguliwa na mawaziri wa kisekta, na kesho wakuu wa nchi wataketi kuhitimisha.

Kikundi cha ngoma ya Msewe kutoka Zanzibar kikitoa burudani nje ya kituo cha mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam leo Jumatatu, Januari 27, 2025 ambako kutafanyika mkutano wa nishati kwa wakuu wa nchi za Afrika. Picha zote na Sunday George

Kama ulidhani minenguo inaishia Ruvuma na mikoa mingine ya kusini mwa Tanzania, kwa taarifa yako Wamasai nao hawajambo.

Kwa sababu haikuharamishwa kuchukua picha ya burudani zilizoendelea, kila mwenye simu janja alionekana akipata picha moja na mbili za wanasanaa wa asili.

Kama ilivyo ada, Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa Tanzania (Basata), Dk Kedmond Mapana, hakuwa mbali na maeneo hayo. Alijaribu kucheza kila mlio wa ngoma uliopigwa nje ya ukumbi.

Hayo yote yanaendelea, huku wageni mbalimbali waliendelea kuwasili ukumbini.

Suti ndilo lililokuwa vazi kuu kwa wageni waliokuwa wanawasili. Khanga zilionekana kwa uchache na zilivaliwa na watoa burudani, huku mavazi ya jinsi na fulana haya yakiadimika.

Aina ya mavazi ya baadhi ya wahudhuriaji yalikuwa kama nakshi fulani ukumbini hapo. Baadhi walivalia sare za suruali na blauzi za vitenge walizoshona sare.

Kabla hujafika zinapopigwa burudani mbalimbali, unakaribishwa na mabango yanayoonyesha hifadhi za taifa, huku maandishi ya ukaribisho yalienea kila upande.

Related Posts