Dar es Salaam. Mkutano wa wa nchi za Afrika kuhusu nishati unaofanyika nchini kwa siku mbili kuanzia leo Jumatatu, Januari 27-28, 2025, umekwamisha kutolewa uamuzi wa mashauri mawili yaliyofunguliwa na mwanasiasa maarufu nchini, Dk Wilbrod Slaa, kuhusiana na kesi ya jinai inayomkabili.
Dk Slaa, aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), anakabiliwa na kesi ya jinai katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Dar es Salaam, akidaiwa kuchapisha taarifa za uongo katika mtandao wa kijamii.
Mgombea huyo wa urais kwa tiketi ya chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 alipandishwa kizimbani mahakamani hapo na kusomewa shtaka linalomkabili, Januari 10, 2025, akidaiwa kutenda kosa hilo, Januari 9, 2025, ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Tangu siku hiyo, amekuwa mahabusu katika Gereza la Keko ambapo mpaka leo amekaa kwa siku 17, akisubiri kusikilizwa na kuamuliwa kwa shauri la maombi ya Jamhuri ya kupinga kupewa dhamana.
Hata hivyo, kupitia jopo la mawakili wake, amefungua mashauri mawili ya maombi ya Jinai Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam, chini ya hati ya dharura, moja kuhusiana na hatima ya dhamana yake na lingine akihoji uhalali wa kesi hiyo inayomkabili.
Mashauri hayo, ambayo yote yalisikilizwa na Jaji Arnold Kirekiano, Alhamisi na Ijumaa iliyopita, yalikuwa yamepangwa kutolewa uamuzi leo, Jumatatu, Januari 27, 2025.
Uamuzi wa mashauri hayo unatarajiwa kuamua hatima ya dhamana yake pamoja na kesi hiyo inayomkabili.
Hata hivyo, kutokana na kuwepo kwa mkutano huo nchini unaoanza leo na kesho, Januari 28, uamuzi wa mashauri hayo umeahirishwa hadi Januari 30, 2025.
Mmoja wa mawakili wa Dk Slaa, Hekima Mwasipu, alieleza kwa Mwananchi kuwa alipigiwa simu na Msajili wa Mahakama Kuu, kumjulisha kuahirishwa kwa uamuzi wa mashauri hayo na mabadiliko hayo ya tarehe kutokana na kuwepo kwa mkutano huo.
Wakili Mwasipu ametoa taarifa hiyo baada ya kuulizwa na Mwananchi iwapo walikuwa na taarifa za mabadiliko ya uamuzi huo kutokana na mkutano huo, kutokana na kufungwa barabara za kuingia katikati ya Jiji.
“Nimepigiwa simu na msajili, maamuzi yatasomwa Januari 30, badala ya leo, kutokana na njia kufungwa kutokana na mkutano wa nishati wa wakuu wa nchi za Afrika,” amesema Mwasipu.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Dar es Salaam, Livin Lyakimana, amelieleza Mwananchi kuwa mashauri hayo ya Dk Slaa na mengine yote yameahirishwa kupisha mkutano huo.
“Kutokana na njia kufungwa kufuatia mkutano huu, tumeelekezwa na Serikali kuwa watumishi wafanye kazi nyumbani,” amesema Lyakimana na kufafanua: “Kwa hiyo mashauri yote hapa yameahirishwa kwa njia ya video conference (mkutano kwa njia ya teknolojia ya mawasiliano ya picha)”.
Kutokana na kufungwa kwa barabara za kuingilia katikati ya Jiji kwa ajili ya mkutano huo, Serikali ilielekeza watumishi wa umma wafanyie kazi nyumbani isipokuwa wale ambao mazingira ya kazi zao yanawalazimu kuwepo katika vituo vyao vya kazi, ikiwemo watumishi wa vyombo vya ulinzi na usalama, sekta ya afya, na usafiri.
Katika kesi ya msingi, kesi ya jinai namba 993 ya mwaka 2025, Dk Slaa anakabiliwa na shtaka la kuchapisha taarifa za uongo katika mtandao wa X (zamani Twitter), kinyume cha kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao namba 14 ya mwaka 2015.
Anadaiwa kuwa Januari 9, 2025, kupitia jukwaa la mtandao wa kijamii wa X, zamani Twitter, katika akaunti ya Maria Sarungi @MariaSTsehai, aliandika ujumbe uliosomeka kama ifuatavyo: “Wakubwa wametafutana, nikisema wakubwa namaanisha Mwamba na Samia, na wala hatuna maneno ya kumung’unya,…na kimsingi wamekubaliana Suluhu Samia amekubali atatoa pesa, Suluhu Samia amekubali ataongeza nguvu ya pesa ni dhahiri atatoa pesa…hizo ni hela za Watanzania wanazichezea Samia na watu wake.”
Pia anadaiwa kuwa aliandika katika akaunti maneno yalisomeka kama; “Samia toka muda mrefu haangaikii tena maendeleo ya nchi anahangaikia namna ya kurudi Ikulu, na namna yake ya kurudi Ikulu ni kwa njia hizo kama kumsaidia mtu kama Mbowe,” wakati akijua taarifa hizo ni za uongo.
Alipandishwa kizimbani mahakamani Kisutu kwa mara ya kwanza na kusomewa shtaka hilo Januari 10, mwaka huu, ambalo alilikana.
Upande wa mashtaka ulieleza upelelezi haujakamilika na mawakili wake wakaomba Mahakama impe dhamana, lakini waendesha mashtaka wakasema wamewasilisha maombi ya kupinga dhamana yake.
Hakimu Mkazi Mkuu Beda Nyaki aliahirisha kesi hadi Januari 23 kwa ajili ya maombi hayo ya Jamhuri kupinga dhamana.
Januari 13, jopo la mawakili wa Dk Slaa nalo likaibua pingamizi dhidi ya uhalali wa kesi hiyo na Mahakama ikapanga kusikiliza pingamizi hilo la Dk Slaa la uhalali wa kesi pamoja na maombi ya Jamhuri kupinga dhamana Januari 17.
Januari 17 Mahakama ilianza kusikiliza pingamizi la Dk Slaa kuhusu uhalali wa kesi ambapo mawakili wake walidai kesi hiyo ni batili na haipaswi kuwepo mahakamani kwani imefunguliwa kinyume na masharti ya sheria.
Walidai kwa mujibu wa kifungu cha 131A (1) na (4), shtaka linalomkabili mteja wao ni miongoni mwa mashtaka ambayo hayapaswi kufunguliwa mahakamani kabla upelelezi haujakamilika.
Upande wa mashtaka ulipinga hoja hiyo wakidai kuwa shtaka hilo kwa tafsiri yake liko katika kundi la mashtaka ambayo yanaweza kufunguliwa mahakamani hata kabla upelelezi haujakamilika. Hakimu Nyaki alipanga kulitolea uamuzi pingamizi hilo Januari 23, 2025.
Waendesha mashtaka walitoa hoja ya ahirisho la usikilizwaji wa shauri la maombi ya kupinga dhamana kusubiri kwanza uamuzi wa Mahakama kuhusiana na pingamizi la Dk Slaa. Hoja hiyo ilipingwa vikali na mawakili wa Dk Slaa wakitaka maombi hayo yasikilizwe siku hiyohiyo kama walivyokuwa wameshakubaliana ili kuokoa muda.
Hata hivyo, Hakimu Nyaki alikubaliana na hoja ya upande wa mashtaka akaamua kuwa maombi ya Jamhuri kupinga dhamana yatasikilizwa baada ya kutoa uamuzi wa pingamizi la Dk Slaa kuhusu uhalali wa kesi hiyo, uamuzi ambao ndio umemfanya Dk Slaa kwenda Mahakama Kuu kufungua mashauri hayo.