KIKOSI cha KenGold kinaendelea kujifua kabla ya kuanza ngwe ya lala salama ya Ligi Kuu Bara, huku kipa namba moja wa timu hiyo, Castor Mhagama akisema ujio wa wachezaji wapya waliosajiliwa dirisha dogo akiwamo Bernard Morrison ‘BM’ , Kelvin Yondani na wengine umeongeza mzuka kikosini.
Mhagama alisema ujio wa wachezaji hao utasaidia kuinusuru timu hiyo, kwani wengi wa mastaa wapya waliotua ni wazoefu wa ligi hiyo.
Timu hiyo iliyopanda daraja msimu huu kutoka Ligi ya Championship na kushindwa kufurukuta katika mechi za duru la kwanza ilivuna pointi sita katika michezo 16.
KenGold hawakuwa na matokeo mazuri duru la kwanza, hivyo kuongezeka kwa kina Morrison na Yondani kutawatoa sehemu moja kwenda nyingine baada ya mechi 16 wakishinda mara moja na kutoka sare tatu, huku wakipoteza 13, wakifunga mabao 12.
“Hatupo pazuri katika msimamo wa Ligi Kuu, naamini wachezaji wapya walioungana na sisi kuna kitu watakiongeza na tutaibakiza timu isishuke daraja,” alisema Mhagama.
“Mbali na hao sisi tuliokuwepo na timu tangu msimu unaanza, tayari kocha alianza kufanyia kazi upungufu uliotufikisha hapa, hivyo tutarejea katika ligi tukiwa bora na kuongeza ushindani dhidi ya wapinzani wetu.”
Katika dirisha dogo lililofungwa katikati ya mwezi huu, KenGold ilifanya usajili wa wachezaji wapya 24, huku ikitema 16 ikiwa ni moja ya njia ya kujiimarisha na wakati Ligi Kuu ikirudi wikiendi hii itaanzia ugenini kwa kuifuata Yanga kwenye Uwanja wa KMC Complex, mechi itakayopigwa Februari 5.
Katika mchezo wa kwanza baina ya timu hizo uliopigwa Mbeya, Yanga ilishinda kwa bao 1-0 lililowekwa kimiani na beki wa kati, Ibrahim Bacca, huku kipa Mhagama akifanya kazi kubwa kuokoa michomo.