Dar es Salaam. Afrika sio maskini wa idadi ya megawati za umeme, bali ukata unaoyakabili mataifa ya bara hilo ni wa uwezo wa kusafirisha na hatimaye kuwafikishia wananchi nishati hiyo.
Msingi wa hoja hiyo ni ukweli kwamba baadhi ya mataifa ya Afrika ama yanazalisha umeme kuzidi mahitaji yao, au yana vyanzo vyenye uwezo wa kuzalisha zaidi ya mahitaji ya sasa.
Mathalan, hadi Desemba mwaka jana, Tanzania ilikuwa inazalisha megawati 3,091.71 za umeme, ikiwa ni zaidi ya mahitaji yake ya ndani ambayo ni megawati 1,800, kwa mujibu wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
Ingawa uzalishaji umezidi mahitaji, ni asilimia 78 pekee ya wananchi wanaofikiwa na huduma ya umeme, kama inavyoelezwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko.
Tatizo la usafirishaji na uunganishaji wa umeme kwa wananchi, linathibitishwa pia na Dk Biteko katika mazungumzo yake na gazeti hili.
“Kwa kweli tatizo kubwa ni kuzalisha, na tatizo la pili ni kusafirisha, huku uunganishaji ukiwa ni tatizo la tatu,” amesema Dk Biteko akijibu kuhusu nini Afrika ifanye kufikisha nishati hiyo kwa wananchi kama inavyozalisha.
Hali kama hiyo inashuhudiwa pia katika mataifa mengine ya Afrika, yakiwemo Msumbiji inayozalisha megawati 2,075, huku mahitaji yake yakiwa takriban megawati 1,000, na Ghana inayozalisha megawati 4,399, zaidi ya mahitaji ya ndani ambayo ni karibu megawati 2,700.
Hata hivyo, Afrika ina takriban terawati 11 za nishati ya jua, gigawati 350 za nishati ya maji, na akiba ya gesi asilia ya kutosheleza mahitaji ya bara lote.
Kutokana na uhalisia huo, hoja ya kwa nini kunakosekana uwiano wa uzalishaji, usafirishaji, na usambazaji wa umeme kwa mataifa ya Afrika inaibuka, na wadau wanataja mbinu za kulikabili hilo.
Hayo yanakuja wakati wakuu wa nchi za Afrika wanakutana kwa siku mbili jijini Dar es Salaam kujadili kuhusu uharakishaji wa nishati kwa wananchi milioni 300 ifikapo mwaka 2030.
Akizungumza na Mwananchi, Meneja Mauzo wa Kampuni binafsi ya Nishati, Asas Energies Co. Ltd, Abdulfatah Lyeme, amesema kinachokwamisha usafirishaji na uunganishaji wa umeme kwa wananchi ni jiografia za maeneo ya nchi za Afrika.
Amesema wananchi wa mataifa hayo, hasa wa vijijini, kwa mujibu wa Lyeme, wametawanyika, hivyo gharama za kuwasafirishia na kuwafikishia umeme huwa kubwa kuliko mauzo yanayoweza kufanyika.
“Ndio maana Tanzania tupo kwenye programu ya Ascent inayohusisha uharakishaji wa mabadiliko ya kudumu ya nishati safi inayofikika, ambayo kimsingi inalenga kurahisisha ufikishaji wa huduma,” amesema.
Amesema programu hiyo inapendekeza kwa maeneo yenye makazi yaliyogawanyika, itumike nishati inayotokana na chanzo cha eneo husika.
“Kwa mfano, kama kijiji kina watu 200 na kuwapelekea umeme ni gharama kubwa, ni vema sekta binafsi ishirikishwe kuwafungia umeme wa jua kama eneo hilo lina jua au kutumia chanzo kingine. Hii itarahisisha kuwafikia wananchi kwa gharama nafuu,” ameeleza.
Kwa mujibu wa Lyeme, tatizo kubwa linalozikabili nchi za Afrika ni uhaba wa fedha za kugharimia usafirishaji na ufikishaji wa umeme, hivyo ni vema kuwekeza kwenye vyanzo rahisi kulingana na eneo husika.
Mtendaji Mkuu wa Kampuni inayozalisha nishati mbadala ya Scatec Release ya Norway, Hans Olav, amesema Serikali za Afrika hazipaswi kujikita katika usambazaji wa nishati kupitia gridi kubwa pekee.
Ameeleza kuwa kunahitajika mpango wa usambazaji wa nishati kupitia gridi ndogo, hasa kwa maeneo yasiyofikika kwa haraka kutokana na jiografia zake.
“Serikali za Afrika zisijilazimishe kusambaza umeme kwa nchi nzima. Itakuwa vigumu kwa sababu inahitaji fedha nyingi. Kuwe na ‘mini grid’ kwa ajili ya maeneo yaliyopo mbali na umeme unakozalishwa,” amesisitiza.
Sambamba na hilo, amesema misaada ya washirika wa kimataifa haiepukiki katika kuwezesha miradi ya usafirishaji na usambazaji wa umeme kwa wananchi.
Kwa upande wa Dk Biteko, amesema ili Afrika iondokane na changamoto za sasa, ni muhimu nchi zake zisiridhike kwa vyanzo vya umeme vinavyotumiwa kwa sasa.
Amesema ni lazima kuongeza vyanzo vya uzalishaji ili kugawanya huduma katika maeneo mbalimbali.
“Muhimu ni kutokuridhika. Lazima kuongeza vyanzo vya uzalishaji. Ndiyo maana tuna mipango ya kujenga vyanzo zaidi, vya maji, jua, upepo, na jotoardhi,” amesema Dk Biteko.
Mwanauchumi mwandamizi, Profesa Mark Mwandosya, amesema Afrika itaondoka gizani iwapo itaruhusu sekta binafsi kuwekeza katika kuzalisha na kusambaza umeme kwa wananchi.
Mwandosya, ambaye ni Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), amesema katika utekelezaji wa hilo, ni muhimu kwa mamlaka za udhibiti kuweka mazingira rahisi kwa wawekezaji ili kuhakikisha wanazalisha na kufikisha huduma kwa wananchi bila kuathiri faida kwa mwekezaji wala kumuumiza mwananchi..