Ndege pori watajwa chanzo ajali ya ndege Iliyoua 179 Korea Kusini

Seoul. Ripoti ya uchunguzi wa awali wa tukio la ajali ya ndege ya Shirika la Jeju, iliyosababisha vifo vya watu 179 huku wawili wakinusurika, imebaini uwepo wa vinasaba (DNA) na manyoya ya ndege pori kwenye mabaki ya injini ya ndege hiyo.

Ajali hiyo, inayotajwa kuwa mbaya zaidi nchini Korea Kusini, ilitokea Desemba 29, 2024, katika Uwanja wa Muan.

Ndege hiyo ilikuwa imebeba abiria waliokuwa wakitoka kusherehekea sikukuu ya Krismasi mjini Bangkok, Thailand.

Ripoti ya awali ya uchunguzi wa tukio hilo, yenye kurasa sita, imewasilishwa leo, Jumatatu, Januari 27, 2025, na mamlaka nchini Korea Kusini. Ripoti hiyo inaonyesha kuwa katika mabaki ya injini zote za ndege hiyo aina ya Boeing 737-800, kulikutwa vinasaba vya batapori aina ya Baikal Teals.

Baikal Teals ni ndege pori jamii ya bata wenye manyoya ya kijani, maarufu kwa kusafiri umbali mrefu kutafuta mazingira bora ya kuzaliana na chakula. Ndege hao wanapatikana kwa wingi Korea Kusini, hasa katika maeneo yenye fukwe za bahari.

“Mabaki ya damu na mabawa yalikutwa kwenye injini zote za ndege,” imeeleza Al Jazeera ikinukuu ripoti hiyo.

Hata hivyo, ripoti hiyo haikutoa maelezo ya kilichosababisha ndege hiyo kushindwa kutua kwa gia ya kutua na badala yake kutumia uvungu (tumbo) kutua ardhini. Pia haikueleza sababu za vifaa vya kurekodi mwenendo wa ndege hiyo (Black Box) kukoma kurekodi dakika nne kabla ya ajali kutokea.

Uchunguzi zaidi wa tukio hilo unaendelea, ukihusisha maofisa kutoka Korea Kusini na Marekani, ambako sanduku la kuhifadhi taarifa za ndege hiyo lilitumwa kwa uchambuzi wa kina.

Ndege hiyo, iliyokuwa ikitokea Bangkok, Thailand kuelekea Uwanja wa Muan nchini Korea Kusini, ilipata changamoto za kutua baada ya gia ya kutua kugoma. Badala yake, ilitua kwa kutumia uvungu na kuserereka, kisha kugonga nguzo zilizokuwa mwishoni mwa njia ya kurukia.

Ajali hiyo ilisababisha vifo vya abiria na wahudumu 179, huku wahudumu wawili waliokuwa sehemu ya mkia wa ndege hiyo wakinusurika japo walipata majeraha makubwa na wanaendelea na matibabu.

Rubani wa ndege hiyo alibaini uwepo wa kundi la ndege pori wakati wa kushuka. Kamera za usalama zilirekodi kundi hilo likisogelea ndege kabla ya kuanza kutua. Baada ya mnara wa kuongozea ndege kuruhusu ndege hiyo kutua, rubani aliombwa kufanya tathmini ya usalama dhidi ya ndege pori hao.

Dakika moja baadaye, vifaa vya kurekodi mwenendo wa ndege viliacha kufanya kazi ndege hiyo ilipokuwa mita 152 (futi 500) juu ya ardhi na kilometa mbili (maili 1.2) kutoka njia ya kutua. Sekunde chache baadaye, rubani aliita Mayday kabla ya kutua kwa dharura.

Ajali hiyo ilisababisha ndege hiyo kugonga nguzo, jambo lililoibua maswali mitandaoni juu ya uwepo wa nguzo hizo. Watu walidai kuwa endapo nguzo hizo zisingekuwepo, madhara ya ajali hiyo yangeweza kupunguzwa.

Kutokana na ajali hiyo, mamlaka ya anga nchini Korea Kusini imesema itafanya maboresho katika viwanja vya ndege kwa kuweka uzio unaoweza kuvunjika kwa dharura.

Ripoti hiyo pia imebainisha kuwa rubani alikuwa na masaa 6,800 ya uendeshaji wa ndege kabla ya kutakiwa kupumzika, huku ofisa wa kwanza akiwa na masaa 1,650 ya uzoefu. Marubani wote walifariki dunia katika ajali hiyo.

Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO) linazitaka mamlaka kuwasilisha ripoti ya awali ya uchunguzi ndani ya siku 30 na ripoti kamili ndani ya miezi miwili tangu kutokea kwa ajali.

Kwa mujibu wa Al Jazeera, mamlaka ya Korea Kusini tayari imewasilisha ripoti hiyo kwa ICAO na nchi nyingine zinazohusika na utengenezaji wa ndege hiyo.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.

Related Posts