Othman: Zanzibar itapata mabadiliko iwapo wananchi watashirikiana

Unguja. Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman, amesema upo uwezekano mkubwa kwa Zanzibar kwenda mbele kimaendeleo na kila kijana kuwa na ajira ya staha, iwapo wananchi watashirikiana kuleta mageuzi ya kisiasa kupitia uchaguzi wa kidemokrasia.

Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar,  ameyasema hayo  Januari 26, 2025 huko viwanja vya Gombani ya Kale Wilaya ya Chake Chake Mkoa wa Kusini Pemba alipokuwa akizungumza katika mkutano wa hadhara wa chama hicho kuhusu mwelekeo wa uchaguzi mkuu ujao.

“Wakati muafaka kwa wafuasi wa chama pamoja na wananchi kwa jumla kujipanga kuelekea mabadiliko kwenye uchaguzi ujao na kukipatia ushindi ACT-Wazalendo ambacho kimejipambanua katika kutetea Zanzibar mpya na yenye mamlaka kamili,” amesema.

Amesema hakuna uwezekano wowote kwa Taifa kusonga mbele kiuchumi na kimaendeleo iwapo haina mamlaka katika nyenzo muhimu za kiuchumi kama vile kodi , bandari na rasilimali nyingine zilizomo ndani ya nchi  kutumika kuisaidia nchi husika.

Amewataka wananchi wa Zanzibar kutambua kwamba uchaguzi  ujao ni muhimu  kwa Zanzibar na kutumia fursa hiyo kukichagua chama cha  ACT-Wazalendo.

Amewaahidi wanachama hao kwamba viongozi wa chama hicho wataendelea kushirikiana na wananchi wa Zanzibar kupigania mageuzi ya kisiasa na maendeleo ili kuhakikisha Zanzibar inasonga mbele kimaendeleo kama zilivyo nchi nyingine.

“Tusonge mbele kimaendeleo kama nchi ambazo hazikupata maendeleo kwa miujiza bali kwa kuwa na uongozi wenye maono.”

Kiongozi wa Chama hicho, Doroth Semu amewashukuru wananchi wa Zanzibar kwa kukiunga mkono chama hicho.

Amesema pia ni vema  kama nchi  kujitahidi kutumia fursa zilizopo kuhakikisha kunakuwepo na uchaguzi wa huru na wa haki katika pande mbili za muungano.

Katibu  Mkuu wa Chama hicho, Ado Shaibu amewataka vijana kuwa tayari kupigania mageuzi na mapambano ya kimageuzi yanaanzia kwao,  hivyo wasivunjike moyo wakiungana nao watapata ushindi.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana wa ACT,  Nasor Maruhuni amewataka vijana kuwa tayari katika kuhakikisha wanaunga mkono chama hicho na kuwa pamoja katika kupigania mageuzi ya kisiasa Zanzibar, kwa kukipa ushindi wa kura muda wa uchaguzi utakapowadia.

Naibu Katibu Mkuu mstaafu wa chama hicho,  Nassor Ahmed Mazrui amewataka Wazanzibari hasa vijana kuwa tayari na kushirikiana bila kujali itikadi za siasa katika kuleta mabadiliko.

 “Hali ni ngumu na umaskini umezonga sana wananchi japokuwa Zanzibar si mahala pa kuwa maskini kiasi hicho, ni ushindi wa ACT pekee itakayoondoa mashaka ya kiuchumi,” amesema

Related Posts