Prof. Mganilwa Atoa Wito wa Ujenzi wa Hosteli Katika Vituo vya Mradi wa SEQUIP-AEP

Katika juhudi za kuboresha elimu ya sekondari kwa njia mbadala kwa wanafunzi waliokatiza masomo kwa sababu mbalimbali, Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) imetakiwa kuongeza jitihada katika ujenzi wa hosteli katika vituo vya mradi wa SEQUIP-AEP.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Baraza la Usimamizi wa Taasisi hiyo, Prof. Zacharia Mganilwa, wakati wa ufunguzi wa warsha ya siku tano kuhusu matumizi ya force account kwa utekelezaji wa miradi ya ujenzi na ukarabati wa majengo ya TEWW. Warsha hiyo ilianza Januari 27, 2025, na inatarajiwa kuhitimishwa Januari 31, 2025.

Prof. Mganilwa alibainisha kuwa ujenzi wa hosteli ni muhimu sana kwa wanafunzi wanaosoma kupitia mfumo wa elimu ya sekondari mbadala, kwani utapunguza changamoto zinazowakabili, hasa wale wanaoishi katika mazingira magumu.

“Wanafunzi hawa wanakabiliana na mazingira magumu sana wanakotoka. Ikiwa tutaongeza upatikanaji wa hosteli kwa wale wenye mahitaji makubwa, tutakuwa tumewasaidia sana kufanikisha masomo yao kwa mazingira bora zaidi,” alisema Prof. Mganilwa.

Aidha, alihimiza uongozi wa Taasisi kuhakikisha wanatafuta njia mbalimbali za kufanikisha ujenzi wa hosteli katika vituo vyote vya mradi wa SEQUIP-AEP. Alisisitiza kuwa juhudi hizi ni muhimu katika kuwasaidia wanafunzi wanaosoma kupitia mfumo wa elimu mbadala ili waweze kupata mazingira mazuri ya kujifunza.

Warsha hiyo inalenga kuwajengea uwezo washiriki kuhusu mbinu za ujenzi na ukarabati wa majengo kwa gharama nafuu kupitia force account, mbinu inayolenga kuboresha uwazi na ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi.

Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), Prof. Michael  Ng’umbi akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa elimu ya Sekondari kwa njia mbadala  (SEQUIP-AEP) muda mfupi kabla ya kumkaribisha Mwenyekiti wa Baraza la Usimamizi wa TEWW, Prof. Zacharia Mganilwa kufungua warsha ya Matumizi ya “Force Account” katika ujenzi na ukarabati wa majengo ya TEWW leo Januari 27, 2025. Warsha hiyo ya siku tano (5) inafanyika Ofisi za TEWW mjini Morogoro.

Washiriki wakifuatilia kwa makini wasilisho kwenye warsha ya Matumizi ya ‘force account’ katika ukumbi wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima Kampasi ya Morogoro-WAMO

Related Posts