Radi yaua wanafunzi saba, yajeruhi 82 wakiwa darasani Geita

Geita. Wanafunzi saba wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Businda, iliyopo wilayani Bukombe, Mkoa wa Geita, wamefariki dunia na wengine 82 kujeruhiwa baada ya kupigwa na radi wakiwa darasani.

Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Paskas Muragili, akizungumza na Mwananchi, amesema tukio hilo limetokea leo Jumatatu, Januari 27, 2025, akieleza kuwa miongoni mwa majeruhi 82, wawili wana hali mbaya.

“Wakiwa darasani wakati mvua inanyesha, ilipiga radi na saba wamepoteza maisha. Kwa muonekano, sita ni wavulana na mmoja ni msichana, lakini bado tunafuatilia kujua majina yao kwani mimi sijaingia kwenye mochwari.

“”Bado hatujawatambua waliopoteza maisha, lakini baadhi ya majeruhi tayari wameongea na kutuambia majina yao. Kadri hali inavyoendelea, tutapata taarifa rasmi,” ameongeza.

Mkuu huyo wa wilaya amesema kwamba, baada ya tukio hilo, madaktari walifika haraka shuleni hapo.

Hilo ni tukio la tatu kutokea mkoani Geita. Oktoba 18, 2019, wanafunzi 39 wa Shule ya Msingi Ihumilo, wilayani Geita, walijeruhiwa kwa kupigwa na radi, na Oktoba 17, 2018, wanafunzi sita wa Shule ya Msingi Emaco Vision walifariki dunia na wengine 23 kujeruhiwa kwa kupigwa na radi wakiwa darasani.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari zaidi.

Related Posts