Dar es Salaam. Rais wa Benki ya Dunia, Ajay Banga, amesema nishati ya umeme ni haki ya binadamu kwani huwezesha watu kufanya wanachokitaka katika nyanja nyingine za maisha ya kila siku.
Banga amesema hayo leo Jumatatu, Januari 27, 2025, katika siku ya kwanza ya kongamano la nishati linalofanyika hapa nchini kwa siku mbili, lilikutanisha wakuu wa nchi karibu 30 na maelfu ya wadau kutoka ndani na nje ya Bara la Afrika.
Alipoulizwa kuhusu matarajio yake katika mkutano huo, Banga amesema hivi sasa kuna ongezeko la watu katika bara hili (Afrika) na kuwa vijana wanahitaji ajira, na ajira ambayo alisema si tu ni tiketi ya kutoka kwenye umaskini, bali ni tiketi ya utu na fikra huru.
Bosi huyo wa taasisi kubwa ya fedha duniani amesema hauwezi kuwa na kazi bila kuwa na umeme. “Umeme ni haki ya binadamu kwa kuwa unakuwa na uwezo wa kufanya unachotaka katika nyanja tofauti ikiwemo elimu, afya, ujuzi na maisha ya kidijitali,” amesema.
Ameongeza kuwa, “Tukiweza kuwaunganisha watu milioni 300 kwa miaka ijayo, si tu kwenye umeme bali pia na huduma za kidijitali, tutafungua fursa za Afrika hususan ajira kwa miongo ijayo, na tunaweza kufanikisha hilo kwa siku hizi mbili, na haya sio bila shaka, sio mazungumzo matupu.”
Endelea kufuatilia Mwananchi.