Kikosi cha Yanga juzi kilishuka uwanjani na kuifumua Copco kwa mabao 5-0 katika mechi ya Kombe la Shirikisho, huku mashabiki wakiachwa njia panda baada ya kumkosa uwanjani winga wao mpya Jonathan Ikangalombo ‘Ikanga Speed’, hata hivyo imefichuka sababu zilizomzuia nyota huyo kushindwa kucheza.
Kocha wa Yanga Sead Ramovic ameliambia Mwanaspoti, sababu ya kukosekana kwa winga huyo kwenye mchezo huo wa Kombe la Shirikisho imetokana na kuugua ghafla kabla ya pambano hilo lililopigwa Uwanja wa KMC Complex, jijini Dar es Salaam.
Ramovic alisema winga huyo asingeweza kuwa tayari kwa mchezo huo kutokana na kuwa na homa za mara kwa mara alizokumbana nazo wiki nzima iliyopita.
Kocha huyo alisema hata hivyo hali yake imekaa sawa ambapo huenda akaanza mazoezi na wenzake yatayoendelea leo Jumatatu.
“Asingeweza kucheza kwa vile alipata homa kali karibu wiki nzima hii jana ndio ameanza kuwa sawa hakukuwa na ulazima kumlazimisha kucheza hii mechi (dhidi ya Copco),” alisema Ramovic na kuongeza;
“Tutamwona maendeleo yake zaidi Jumatatu (leo) tutakapoendelea na mazoezi, hajafanya mazoezi sawasawa na timu nzima tangu amefika na sasa amepata hiyo shida ya afya.”
Aidha Ramovic aliwashusha presha mashabiki wanaomsubiria winga huyo Mkongomani akisema anahitaji kuingia kwenye mifumo ya timu yake na baada ya hapo ataonekana.
“Kuna kazi tunatakiwa kuifanya kwake (Ikanga Speed), huyu ni mchezaji mpya ambaye alifika hapa tukiwa kwenye mechi ngumu za Ligi ya Mabingwa Afrika, tunataka kwanza kumuona anaunganikaje na wenzake na anakuwa tayari kwa aina ya falsafa ya soka tunalotaka hapa,” alisema Ramovic aliyetua Yanga mwishoni mwa mwaka jana akichukua nafasi ya Miguel Gamondi aliyesitishiwa mkataba ghafla.
Ikanga Speed amesajiliwa na Yanga kupitia dirisha dogo la usajili akiwa staa pekee wa kigeni aliyeongezwa katika kikosi hicho akitokea AS Vita ya DR Congo akichukua nafasi ya Mkongomani mwenzie, Jean Baleke aliyesitishiwa mkataba, akiingia sambamba na beki Israel Mwenda aliyesajiliwa kutoka Singida BS.