RC Macha azishukia shule binafsi kurudisha wanafunzi madarasa

Shinyanga. Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, amewaonya wamiliki wa shule binafsi kuacha tabia ya kuwarudisha madarasa wanafunzi wanaoshindwa kufikia alama wanazozitaka.

 Amesema hawana mamlaka hiyo, bali Serikali ndiyo inayoweza kufanya hivyo kupitia mtihani wa darasa la nne na kidato cha pili.

Mkuu huyo wa mkoa (RC), ametoa onyo hilo leo Jumatatu, Januari 27, 2025, wakati wa hafla ya kumuapisha Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Peter Masindi, katika ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga. Ameagiza wakuu wa wilaya na wakurugenzi kufuatilia suala hilo.

“Naagiza wakuu wa wilaya na wakurugenzi kufuatilia suala hili la kurudisha wanafunzi darasa, hasa kidato cha pili na nne. Mwenye mamlaka ya kurudisha kwa wastani wa mwanafunzi ni Serikali pekee, hata kama ni shule binafsi,” amesema Macha.

Agizo hilo linatolewa baada ya Mwananchi kuripoti baadhi ya shule binafsi kuwarudisha madarasa  wanafunzi waliopata madaraja ya pili, tatu, au nne, hasa kwenye matokeo ya kidato cha nne mwaka 2024.

Mmoja wa wazazi ambaye mtoto wake amehitimu katka moja ya shule mkoani Iringa, aliyeomba kutotajwa jina Amesema katika shule aliyokuwa akisema binti yake, tangu wameanza kidato cha kwanza walikuwa wanachunjwa.

“Wanafunzi waliokuwa wanapata madaraja ya pili au tatu wazazi wanapigiwa simu kwamba waje wawahamishe, lakini hii ni kinyume na sera ya elimu.

“Serikali inapaswa kufanya operesheni maalumu kwa shule hizi watabaini mengi,” amesema mzazi huyo alipozungumza na Mwananchi.

Katika uapisho huo, RC Macha ametumia fursa hiyo kumkaribisha Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Peter Masindi, akimuhimiza kushirikiana na wakuu wenzake wa wilaya na wakurugenzi katika utekelezaji wa majukumu yake.

Naye DC Masindi Amesema: “Napokea maelekezo niliopewa na mkuu wa mkoa na ninaahidi kufanya kazi kwa kuwatumikia wananchi na si kwa faida yangu binafsi.”

Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita, akizungumza kwa niaba ya wakuu wa wilaya, ameahidi kushirikiana na mkuu wa mkoa kushughulikia suala la shule binafsi kurudisha wanafunzi darasa kwa kigezo cha kutofikisha wastani wa shule.

Related Posts