Na. Mwandishi wetu – Dar es Salaam
Tanzania imepongezwa kwa kufikisha nishati ya umeme hadi ngazi ya vijiji hali inayoendelea kuchochea maendeleo na ustawi kwa wananchi vijijini.
Hayo yamesemwa na Rais wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) Dkt. Akinumwi Adesina wakati wa mkutano wa nishati Afrika leo Januari 27, 2025 jijini Dar es Salaam.
Amesema Tanzania ni mfano wa kuigwa na nchi nyingine za Afrika kwa kufanya vizuri katika uwekezaji wa miundombinu na miradi ya usambazaji iliyoiwezesha nchi hiyo kusambaza umeme katika vijiji vyote 12,318.
” Naomba nitumie fursa hii kumpongeza Rais wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha wananchi wa Tanzania kufikiwa na nishati ya umeme katika vijiji vyote, jambo hili linastahili kupongezwa kutokana na umuhimu wa nishati hii katika maendeleo ” amesisitiza Dkt. Adesina.
Kuhusu mkutano wa nishati Afrika Dkt. Adesina amesema kuwa lengo ni kuwafikishia umeme watu Waafrika milioni 300 wanaoishi chini ya ukanda wa Jangwa la Sahara akisisitiza kuwa lengo hilo linakwenda kufanikiwa akisisitiza uwazi na uwajibikaji.
“Mkutano huu unalenga kuifungua Afrika kwenye eneo la nishati ya umeme, kuhakikisha wananchi katika nchi za Afrika wanaunganishwa na umeme”.
Kwa upande wake Waziri wa Fedha na Mipango wa Zambia Mhe. Dkt. Situmbeko Musokotwane ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuiuzia umeme nchi yake kutokana na nchi hiyo kuwa na upungufu wa nishati hiyo.
“Tunashukuru Serikali ya Tanzania kwa kutuuzia umeme kwa sababu nchi yetu imekua na changamoto ya upungufu wa umeme”, amesema Dkt. Musokotwane
Mkutano wa nishati Afrika unafanyika kwa mara ya kwanza jijini Dar es Salaam, Tanzania ukiwakutanisha wakuu wa nchi za Afrika kwa lengo la kuwafikishia nishati ya umeme Waafrika milioni 300 ifikapo mwaka 2030.