TRC yaongeza safari za treni, barabara Dar zikifungwa

Dar es Salaam. Shirika la Reli Tanzania (TRC) limetangaza kuongeza huduma za treni za mijini kati ya Stesheni ya Kamata na Pugu, jijini Dar es Salaam kwa siku ya leo Januari 27 na 28, 2025, kutokana na kufungwa kwa baadhi ya barabara za kuingia katikati ya jiji kutokana na mkutano wa nishati wa wakuu wa nchi za Afrika.

Taarifa iliyotolewa leo Jumatatu, Januari 27,2025 na Mkuu wa Kitengo cha Habari na Uhusiano, Fredy Mwanjala imezitaja treni hizo kuwa ni ya Stesheni ya Kamata na Pugu.

Mwanjala amesema treni zilizoongezwa ni ya saa 12.00 asubuhi kutoka Stesheni ya Kamata na treni ya saa 12.05 jioni kutoka Stesheni ya Pugu.

“Shirika la Reli Tanzania linapenda kuwatangazia kuwa kutokana na kufungwa kwa barabara za kuingia katikati ya Jiji la Dar es Salaam kufuatia mkutano wa nishati wa wakuu wa nchi za Afrika, shirika limeongeza treni mbili za mjini kati ya Stesheni ya Kamata na Pugu, Jijini Dar es Salaam kwa siku ya Januari 27 na 28, 2025,” imeeleza taarifa hiyo.

Hata hivyo, Mwanjala amesema pamoja na hatua hiyo ratiba za awali za treni zitabaki kama kawaida.

Endelea kufuatilia Mwananchi.

Related Posts