Ukimya watawala kufunguliwa Soko la Kariakoo, wafanyabiashara wang’aka

Dar es Salaam. Wakati ukimya ukitawala juu ya hatma ya kufunguliwa kwa Soko la Kimataifa la Kariakoo jijini Dar es Salaam, wafanyabiashara wameiomba Serikali kutoa kauli kinachoendelea ili kuondokana na changamoto wanazopitia ikiwamo mvutano na mgambo na kupoteza mitaji yao.

Ni miaka minne sasa imepita tangu soko hilo lilipoanza kukarabatiwa baada ya kutokea tukio la moto na kuteketeza mali za wafanyabiashara zilizokuwa sokoni humo Julai 10, 2021.

Baada ya kutokea tukio hilo, Serikali ilitoa Sh28 bilioni kwa ajili ya kulikarabati, shughuli ambayo ilianza tangu Januari 2022.

Ukarabati huo pia ulikwenda sambamba na ujenzi mpya wa soko dogo litakalokuwa na ghorofa sita kwenda juu na mbili kwenda chini kusaidia shughuli za kibiashara kufanyika kwa ufanisi.

Katika kipindi hicho cha ujenzi wafanyabiashara waliokuwepo sokoni hapo, walihamishiwa kwa muda katika masoko ya Kisutu, Machinga Complex na Karume.

Pamoja na vikao vya mara kwa mara vilivyofanyika baina ya uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam, wataalamu na taasisi za kiserikali ikiwamo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na wafanyabiashara, lakini hakuna mrejesho wowote juu ya hatma ya kufunguliwa kwa soko hilo.

Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti, baadhi ya wafanyabiashara na viongozi wa masoko madogo wamesema bado hawaelewi kinachoendelea licha ya matumaini waliyopewa na Mamlaka za Serikali.

Pia baadhi ya wafanyabiashara waliokuwa kwenye soko hilo, wamesema bado hawajapewa taarifa yoyote ni lini watarejea, jambo linalowasukuma kujipanga kwenda kumuona Mkuu wa Mkoa huo, Albert Chalamila.

“Kumetawala ukimya tangu tulivyofanyiwa uhakiki kwa mara nyingine na pia tumesikia mkuu wa mkoa alishapokea ripoti, sasa mbona hakuna tunachoambiwa nini kinaendelea na kilichobainika katika ripoti ile wakati ni haki yetu kujua,” anasema akishangaa mmoja wa wafanyabiashara ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.

Mwenyekiti wa soko dogo, Minja Msuya anasema  wana mpango wa kwenda kuuona uongozi wa mkoa kujua kinachoendelea, kwa kuwa hawajapewa mrejesho wowote mpaka sasa.

“Tulikuwa tunasubiri hii Januari iishe kwa kuwa mambo yamekuwa mengi ikiwemo watu kupeleka watoto shule nadhani mwisho wa mwezi huu au Februari tutakutana na uongozi wa juu wa mkoa,” anasema Msuya.

Mmoja wa wafanyabiashara aliyejitambulisha kwa jina moja la Elibariki, anasema mara kadhaa wamesikia Chalamila akitangaza eneo la soko hilo kuanza kufanya biashara saa 24, lakini hajawahi kusikia ushirikishwaji wa wafanyabiashara waliokuwa katika soko la Kariakoo lililoungua na kukarabatiwa,  ambalo ndilo limebeba jina la eneo hilo.

“Kama kweli wamedhamiria Kariakoo ifanye kazi saa 24, huwezi kuliacha soko lile na nilitegemea mpaka sasa wale waliokuwepo kule sokoni wangekuwa wameshapangwa au kukutana nao kwa vikao kadhaa kujua namna watakavyofanya shughuli zao pindi watakaporejea,” anasema Elibariki.

Husna Chaurembo anasema wamesubiri kwa muda mrefu soko hilo kurejea kwani lilikuwa likiwasaidia kupata wateja wa chakula kuliko kuvizia wateja barabarani.

“Soko lirudi, kwani tumebaki kuvizia wapita njia na wanaokuja kufanya manunuzi ya bidhaa nyingine huku Kariakoo, lakini wa sokoni walikuwa uhakika kwa kuwa ni lazima kila siku wale kuanzia asubuhi, mchana na jioni tunaomba Chalamila aseme neno” analalama Husna.

Rashid Kabwali wa soko la mzunguko anasema mara ya mwisho wamefanya kikao na Takukuru na Shirika la masoko Septemba, 2024 kuombwa wasifanye tena vurugu.

Anasema walidokezwa kati ya vitu ambavyo watapaswa kuwa navyo wakati wa kurejea sokoni hapo ambapo hata hivyo hawakuambiwa ni lini ni  TIN namba na kitambulisho cha Taifa (Nida).

“Tulipoitwa kwenye kikao hicho tulionywa tusifanye tena vurugu, tutulie hadi tutakaporejeshwa na hata tulipotaka kujua ni lini tutarudi tulijibiwa suala hilo lipo ngazi ya mkoa wenyewe ndio watatoa taarifa,” anasema na kuongeza:

“Ombi letu tunaomba soko hilo lifunguliwe mapema mwaka huu kwa kuwa wengi tulipohamishiwa kufanya biashara haswa sisi wa Karume, mtaji umekata, kutokana na kutokuwa na biashara eneo lile” anasema.

Amina Kipozi, anasema tangu soko hilo kuwa kwenye ukarabati, alibaki kufanya biashara pembezoni mwa uzio uliowekwa wakati wa ujenzi licha ya kuwa kila wakati wanakimbizana na mgambo wa jiji, lakini ndio sehemu anapata riziki na ndio kuna wateja waliomzoea.

“Hili soko lirudi, maana hatupendi kukimbizana na mgambo wa jiji lakini utafanyaje na familia inataka kula na watoto kwenda shule, tunaomba uongozi wa mkoa utoke hadharani na kutuambia lini tunarudi,  hata tujiandae ukizingatia tulishaambiwa kutakuwa na mabadiliko ya ufanyaji biashara” anasema Amina.

Sintofahamu Soko la Kariakoo ilianzia hapa

Aprili 2024, uongozi wa Shirika la Masoko Kariakoo ambao ndio waendeshaji wa soko hilo, katika mkutano na wanahabari ulisema ujenzi wake umeshafikia asilimia 98 na kueleza lingeanza kazi rasmi Mei, 2024.

Pia, uongozi huo ulitoa utaratibu wa namna wafanyabiashara waliokuwepo hapo watakavyorejea na wengine wapya watakavyoingia.

Baadaye shirika hilo lilitoa majina ya watu waliopitishwa kurejea sokoni hapo, hatua ambayo wafanyabiashara hawakukubaliana nayo kwa kile walichodai wengi walikatwa katika orodha hiyo, kwa kigezo cha kuwa na mkataba wa moja kwa moja na shirika.

Wiki moja baada ya orodha ya waliotakiwa kurudi ilikuwa ni 819 kati ya wafanyabiashara zaidi ya 1,600 waliokuwepo awali, jambo ambalo lilipingwa na wafanyabiashara hao na kueleza wengi wao walikuwa wapangaji japo wana risiti zote za kufanya malipo kwa shirika.

Kutokana na kutoridhika na maamuzi hayo ya Julai 12, 2024 wafanyabiashara hao walifanya maandamano ya kupinga hilo, yaliyoanzia viwanja vya Mnazi Mmoja hadi Ofisi ndogo za Chama cha Mapinduzi (CCM) zilizopo Lumumba.

Julai 13, 2024 Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila alikutana na wafanyabiashara hao katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa uliopo Ilala Boma na kusikiliza malalamiko yao, ambapo alikubaliana na hoja walizozitoa.

Miongoni mwa hoja zao ni  pamoja na viongozi wao kutoshirikishwa katika uhakiki wa mwisho kabla kutoa orodha hiyo, kwa kuwa wao ndio wanaowajua.

Hoja nyingine zilizoibuliwa katika kikao hicho ni baadhi ya watu kupewa vizimba zaidi ya kimoja na maduka, ilihali baadhi yao  hawakuwahi kuwa wafanyabiashara katika soko hilo.

Hata hivyo, muda mchache baada ya kumaliza kikao na wafanyabiashara hao, Chalamila alikutana na uongozi wa Shirika la Masoko Kariakoo na kuagiza majina yote ya wanaopaswa kurejea yaliyowekwa kwenye mfumo kuondolewa mara moja na kuhakikiwa upya.

Aidha Chalamila katika maagizo hayo pia aliitaka Taasisi ya Kuzua na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kufanya uchunguzi wake wa namna majina hayo yalivyopatikana na endapo kutabainika kuwepo kwa harufu yoyote ya rushwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wahusika, huku akilitaka shirika hilo lisijishughulishe na kitu chochote katika soko hilo wala kuzungumzia maendeleo yake.

Pia Chalamila alitaka wafanyabiashara ambao hawakuwa kwenye orodha hiyo ya awali wahakikiwe na wao kwa kuwashirikisha viongozi wao, na baada ya hapo majina yatakayopitishwa yataunganishwa na orodha ya awamu ya kwanza na kurudishwa tena kwenye mfumo.

Safari hii alisema orodha ya majina hayo yatapandishwa mara baada ya kuidhinishwa na ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Tamisemi na Ofisi ya Rais, kazi hiyo ya kurudiwa kwa uhakiki ilifanywa na kamati maalumu aliyoundwa ikiongozwa na Mwenyekiti wake Aman Mafuru.

Septemba 4, 2024 Kamati hiyo ilimkabidhi ripoti yake mkuu huyo wa mkoa, hafla ambayo ilifanyika katika ukumbi wa mikutano wa Arnatoglo jijini hapa.

Akipokea ripoti hiyo, Chalamila alisema alilazimika kuunda kamati hiyo ili kujiridhisha juu ya mchakato uliotumika kupata orodha ya majina ya awali ya wafanyabiashara hao, hatua ambayo imechochewa na unyeti wa eneo la Soko la Kariakoo kwa masilahi ya jiji la Dar es Salaam na Taifa kwa ujumla.

Sambamba na kupokea ripoti hiyo, Chalamila alipokea maoni kutoka kwa wajumbe wa kamati hiyo ili kuwa na uelewa wa pamoja.

Hata hivyo, hadi sasa imepita miezi minne tangu Chalamila alipopokea ripoti hiyo, huku ukimya ukiendelea kutawala kuhusu lini hasa soko hilo litafunguliwa rasmi na kuzua sintofahamu kwa wafanyabiashara.

Kwa nyakati tofauti, Mwananchi iliutafuta uongozi wa serikali mkoani humo, akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, Katibu Tawala wa Mkoa, Dk Toba Nguvila ambao majibu yao ni kuwa suala hilo analishughulikia Chalamila.

Januari 20, 2025, alipotafutwa Chalamila kwa njia ya simu, iliita bila kupokelewa na alipotumiwa ujumbe mfupi kuuliziwa suala hilo, aliahidi akitulia angejibu lakini hakufanya hivyo hata aliporudiwa kwa mara nyingine kukumbushwa.

Related Posts