Dodoma. Usaili wa walimu wa daraja la 3C Kiswahili uliopaswa kufanyika Januari 28, 2025, umesogezwa mbele hadi Januari 30, 2025, ili kupisha mkutano wa siku mbili wa nishati wa wakuu wa nchi za Afrika unaoanza leo, Jumatatu, Januari 27, 2025, jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana, Jumapili, Januari 26, 2025, na Katibu wa Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Lynn Chawala, mabadiliko hayo yametokana na kufungwa kwa baadhi ya barabara jijini Dar es Salaam kwa muda. Amesema hali hiyo inaweza kusababisha changamoto kwa wasailiwa kufika katika vituo vyao vya usaili kwa wakati.
“Usaili wa walimu wa daraja la 3C Kiswahili uliopangwa kufanyika Januari 28, 2025, katika vituo mbalimbali nchini sasa utafanyika Januari 30, kuanzia saa 1:00 asubuhi.
”Mabadiliko hayo yametokana na uwepo wa mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika kuhusu nishati, utakaofanyika jijini Dar es Salaam, uliosababisha kufungwa kwa baadhi ya barabara Januari 27 na 28, 2025,” imeeleza taarifa hiyo.
Amesema mabadiliko hayo yanalenga kuepusha changamoto ya usafiri kwa wasailiwa wanaotoka Dar es Salaam, ili kuhakikisha wanawahi kufika vituoni kwa wakati.
Hata hivyo, tarehe nyingine za usaili, mahali pa kufanyia usaili, na muda wa usaili, vimebaki kama ilivyoainishwa kwenye matangazo ya awali ya kuitwa kwenye usaili.
Usaili wa walimu walioomba ajira serikalini ulianza Januari 14, 2025, na unatarajiwa kumalizika Februari 24, 2025. Serikali ilitangaza nafasi za ajira 14,648, huku walioomba nafasi hizo wakiwa 201,707.