Usajili wa Sowah, Pokou Singida BS washtua

KOCHA wa zamani wa Yanga, Hans Pluijm amesema kutua katika Ligi Kuu Bara kwa majina ya nyota wa kimataifa akiwamo Jonathan Sowah na Serge Pokou katika kikosi cha Singida Black Stars kutakiimarisha kikosi hicho.

Pluijm alisema amekua akiifuatilia Ligi Kuu Bara na naamini ndani ya misimu miwili au mitatu ijayo Singida Black Stars inaweza kuwa moja ya timu tishio kutokana na uwekezaji inaoufanya.

Pluijm aliyewahi kuifundisha Singida United kabla ya kutua Azam FC, alisema Singida imeonyesha uthubutu kufanya usajili mkubwa tangu mwanzo mwa msimu na miongoni mwa majina yaliyomshtua ni pamoja na Sowah na Pokou.

Licha ya kuwa na Elvis Rupia ambaye ni kinara wa mabao Ligi Kuu, Singida BS ilimuongeza katika dirisha lililopita Sowah (pichani) ambaye ni mmoja wa washambuliaji hatari kutoka Al-Nasr ya Libya aliyekuwa pia akimezewa mate Yanga.

“Inapendeza kuona timu nyingine zikiibuka na kuonyesha kuwa zinaweza kushindana, kikubwa ni kuendelea kuamini katika mipango yao, kiukweli kama ubora wa wachezaji nimeuona ni mkubwa.”

Kuhusu  Pokou, ambaye Simba ilikuwa ikimhitaji kabla ya kusajiliwa na Al Hilal ya Sudan, kocha huyo alisema: “Inatakiwa kuwepo kwa timu nyingine tatu hadi nne kama Singida. Uwepo wake utafanya ligi ya Tanzania kuendelea kukua na ushindani utakuwa mkubwa zaidi.”

Kocha huyo alieleza awali alijipa muda kuwatazama Singida kuona kile walifanya katika michezo ya mwanzoni mwa msimu lakini wamethibitisha kuwa wanaweza kupambania nafasi za juu.

Kwa sasa Singida ipo nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 33 kupitia michezo 16, pointi mbili pungufu na ilizonazo Azam iliyopo nafasi ya tatu ikimiliki 36 na sita pungufu na zile za Yanga yenye 39, wakati Simba inaongoza ikiwa na 40.

Related Posts