Mwanza. Shangwe imeibuka baada ya abiria waliokuwa wakisubiri kuvuka eneo la Kigongo wilayani Misungwi kwenda Busisi wilayani Sengerema mkoani Mwanza kuruhusiwa kupita kwa miguu juu ya Ziwa Victoria kupitia daraja la muda linalotumiwa na mkandarasi anayejenga daraja la JPM.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu, Januari 27, 2025, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Mwanza, Pascal Ambrose, amesema: “Uamuzi wa kuwaruhusu kutembea kwa miguu juu ya daraja hilo ulifikiwa baada ya vivuko vya MV Mwanza na MV Misungwi vinavyotoa huduma eneo hilo kusitisha huduma kwa muda.”
“Hawakuvunja mageti, ila tuliwaruhusu baada ya kuona vivuko vimesimama kwa muda kutokana na magugu maji yaliyo eneo vinapopita, hivyo tukaona kuliko waendelee kusubiri kwa muda mrefu basi tuwaruhusu na magari,” amesema Ambrose.
Ambrose amesema uamuzi huo ulilenga siku ya jana (Jumapili) pekee huku akisisitiza baada ya huduma ya vivuko kurejea, mageti yalifungwa na wasafiri kuendelea kutumia vivuko hivyo.
Akizungumza na NewsUpdates jana, Meneja wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (Temesa) Kanda ya Ziwa, Vitalis Bilauli, alisema vivuko hivyo vililazimika kusitisha huduma kwa muda kutokana na kuzingirwa na magugu maji.
“Tatizo letu kubwa ni magugu maji, unajua kwenye lile eneo kuna magugu maji ya aina mbili, yale ya vichaka na yale laini yalikuwa yametanda hapa (eneo) la vivuko kupita na kuhatarisha sehemu yenye boksi la kupoza injini ya kivuko (cooling box),” alisema Bilauli.
Furaha hiyo itaendelea mwezi ujao baada ya Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, kusema kuwa daraja hilo litaanza kutumika.
Ulega alitoa kauli hiyo Ijumaa, Januari 24, 2025, baada ya kukagua mradi huo wenye thamani ya Sh669 bilioni. Utakapokamilika utapunguza muda wa kuvuka eneo la Kigongo kwenda Busisi kutoka wastani wa saa moja na nusu kwa kutumia vivuko hadi wastani wa dakika 10.
“Ujenzi wa daraja hili umefikia asilimia 96.4 kuelekea mwishoni, hongereni sana. Jambo la pili, wakati Rais Samia Suluhu Hassan anashika madaraka, ujenzi ulikuwa asilimia 25, wakati ukivuka na kivuko, nguzo hazikuwa zikionekana, leo daraja limesimama,” alisema.
Daraja hilo litakapokamilika, litakuwa refu kuliko yote katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, litakuwa na njia mbili za magari zenye upana wa mita saba kila upande, njia ya waenda kwa miguu yenye upana wa mita 2.5 kila upande, maegesho ya dharura yenye upana wa mita 2.5 kila upande na njia ya waenda kwa miguu yenye upana wa mita 2.5.
Daraja la JPM litakuwa la sita kwa urefu katika Bara la Afrika, likiwa na urefu wa kilomita 3, upana wa mita 28.45 na barabara unganishi zenye urefu wa kilomita 1.66.
Kwenye daraja hilo lililopewa jina la JPM kama sehemu ya kutambua, kuenzi na kumbukumbu Rais wa awamu ya tano, hayati John Magufuli aliyeasisi wazo na kuanza utekelezaji wa mradi huo aliouacha kwa asilimia 25 ya ujenzi, kuna nguzo za msingi 804, vitako vya nguzo za madaraja 65, nguzo 64 na nguzo za mialo 806.
Usanifu wa daraja hilo ulitumia teknolojia ya madaraja marefu, inayoitwa ‘Extra Dosed Bridge’ ambapo kutakuwa na nguzo kuu tatu zenye kimo cha mita 40 na umbali mita 160 kutoka nguzo moja hadi nyingine.
Kwenye hizo nguzo 64, mbili kati ya hizo zitakuwa umbali wa mita 100 kutoka nguzo moja hadi nguzo kuu, wakati zilizobaki zitakuwa umbali wa mita 40 kutoka nguzo moja hadi nyingine. Kwenye kila nguzo ya daraja kuna nguzo za msingi (pile foundations) zilizochimbiwa ardhini kwa urefu wa kati ya mita 11.5 na mita 66.
Hivyo, daraja hilo lina upenyo mita 120 kati ya nguzo zake kuu, kuruhusu meli na vyombo vingine vya usafirishaji majini kupita, na hivyo kuwa daraja lenye upenyo mkubwa zaidi nchini kulinganisha na daraja la Tanzanite na Kigamboni ya jijini Dar es Salaam.