WB, AfDB wataka ushirikiano kuongeza nishati Afrika

Dar es Salaam. Benki ya Dunia (WB) na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) zimesema ili Afrika ipate umeme wa uhakika, lazima kuwe na ushirikiano kati ya Serikali, mashirika ya fedha, na asasi za kiraia kwa kuweka mipango itakayoleta matokeo ya uhakika.

Hayo yameelezwa leo Jumatatu, Januari 27, 2025, katika mkutano wa Afrika wa nishati unaofanyika jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika mjadala ulioendeshwa na mwandishi wa habari wa CNN, Zain Asher, Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dk Akinumwi Adesina, amesema Bara la Afrika linapoteza kati ya asilimia 3 hadi 4 ya mapato yake ya ndani (GDP) kwa kukosa umeme, huku zaidi ya watu milioni 600 wakiwa hawana nishati ya umeme au safi ya kupikia.

“Ninachotaka kusema ni kwamba tunamhitaji kila mtu, tunawahitaji wakuu wa nchi na Serikali, tunahitaji Benki ya Dunia na asasi za kiraia,” amesema.

Amesema kwa hali ya sasa, nchi za Afrika hazipaswi kufanya kazi kwa mazoea au kugawanyika

“Hapa kuna Umoja wa Mataifa, Jumuiko la Nishati la Kimataifa, na Benki ya Kiislamu ya Maendeleo. Huu ni ubia mkubwa,” amesema.

Ametoa wito kwa viongozi wa nchi za Afrika, watakaokutana kesho siku ya pili ya mkutano huo, kuanisha miradi wanayoendesha katika nchi zao na kuongeza bajeti katika sekta ya nishati.

“Lazima kuwe na mfumo wa ugavi na ununuzi wa nishati utakaoonyesha ugawaji wa nishati wa kikanda. Kitu cha pili tunachotegemea ni kwamba baada ya nchi 12 za Afrika kusaini makubaliano, zaidi ya watu milioni 140 wataanza kunufaika.

“Katika mkutano huu, suala si kuzungumza tu. Mwisho wa yote, wananchi lazima wapate nishati,” amesema Dk Adesina.

Rais wa Benki ya Dunia, Ajay Banga, amesema mkutano huo unatarajiwa kutoka na sera zitakazohakikisha watu milioni 600 wanafikiwa na umeme.

“Sera zinahitajika ili kufanya jambo hili liwe wazi, ili benki za biashara na sekta binafsi ziweke fedha zao na kupata matokeo yanayotabirika katika upatikanaji wa fedha,” amesema.

Amesema ili kuwe na matokeo yanayotabirika, miradi ya umeme haipaswi kuishia tu kuzalisha nishati, bali pia kuhakikisha umeme unawafikia wananchi.

Katika upatikanaji wa fedha za kuendesha miradi ya umeme, amesema wamelialika Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ili kuziwezesha Serikali za Afrika kufanikisha miradi yao.

“Tumewaleta IMF hapa ili tuandae mifumo itakayofanya utoaji wa huduma hizi kuwa na tija zaidi. Kuna wabia waliojitokeza kuleta utabirika wa fedha kwa ajili ya miundombinu na ufadhili.

“Sehemu ya mwisho ni masoko ya nishati ya kikanda. Nadhani Tanzania imesema wana ubia na nchi nne na wanataka kuleta nchi ya tano. Hili ni jambo tunalotaka lianze kutekelezwa barani Afrika,” amesema.

Rais wa Rockefeller Foundation, Dk Rajiv Shah, amesema juhudi za kuongeza nishati Afrika zinapaswa kuanzia ndani ya bara hilo.

“Kwanza, kila mtu anafahamu kwamba ili tuwe na fursa ya kufanikiwa, jitihada hizo ni lazima ziongozwe kutoka Afrika. Idadi kubwa ya viongozi wa Afrika watakuja hapa na kutia saini makubaliano yatakayoleta mabadiliko ya sera na miundombinu. Nadhani haya ni mafanikio makubwa,” amesema.

Dk Shah amesema jambo la kutia moyo ni kuona tayari kuna wabia walioonyesha nia ya kuwekeza Dola bilioni 43 za Marekani katika nishati tangu Mei 2024.

Pia, amesema katika mkutano huo kuna wawekezaji zaidi ya 200 waliokuja kuangalia fursa za kuwekeza katika sekta ya nishati.

“Hii inatupa matumaini kwamba Kusini mwa Jangwa la Sahara kutakuwa na juhudi za kusaidia uwekezaji ili kuimarisha taasisi za umma,” amesema.

Related Posts