UHONDO wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) unatarajia kuendelea Januari 31 wakati duru la pili litakapoanza, huku Junguni United ikiipiga mkwara Chipukizi itakayovaana nayo kwenye Uwanja wa Polisi FFU Finya, Pemba.
Junguni itavaana na Chipukizi ikiwa ni siku tatu tangu duru hilo kuanza huku Mlandege ikiwa kileleni mwa msimamo ikiwa na pointi 30 baada ya mechi 14 ikiwa na deni la kulipa kisasi baada ya kufungwa 1-0 katika mechi ya Desemba 10, 2024.
Timu hiyo inayoshiriki ZPL kwa mara ya kwanza baada ya kupanda msimu huu, ipo nafasi ya 11 ikiwa na pointi 18 – moja pungufu na ilizonazo Chipukizi ambao ni mabingwa wa Kombe la Shirikisho waliopo nafasi ya 10 kila moja ikicheza mechi 15.
Upinzani uliopo baina ya timu hizo za Pemba, umewafanya mabosi wa Junguni kupiga mkwara kwamba hawataki kupoteza tena mchezo mbele ya Chipukizi na kutamba duru la pili wanaanza kivingine.
Mtendaji Mkuu wa Junguni, Sultan Issa alisema kutokana na usajili walioufanya katika dirisha dogo kwa kuongeza wachezaji saba wanaamini watapata matokeo mazuri wakianza ngwe ya lalasalama.
Issa alisema Chupukizi ni wazoefu wa ligi na wanawaheshimu, lakini wamejipanga vizuri kukabiliana nao ikiwa ni tofauti na duru lililopita hawataki warudie makosa waliyoyafanya mzunguko wa kwanza.
Hata hivyo, Kocha wa Chipukizi, Mzee Ali Abdalla alisema hana hofu dhidi ya wapinzani wao hao kwani timu yake ni kubwa na vijana wazoefu watahakikisha wanaifunga Junguni kama walivyofanya duru la kwanza.
Kocha huyo alisema anajua mchezo utakuwa mgumu kutokana na timu nyingine kutumia mapumziko ya ligi kupisha michuano ya Kombe la Mapinduzi 2025, lakini bado anaamini watafanya vizuri ila anaacha dakika 90 za mchezo huo ziamue kuliko kupiga kelele mdomoni.