Afrika Inapoteza Dola Bilioni 18 Kisa Mizozo – Global Publishers



Rais William Ruto wa Kenya

Rais William Ruto wa Kenya ambaye yuko mstari wa mbele katika kupigania mageuzi ya kitaasisi ndani ya Umoja wa Afrika (AU), alisema jana Jumatatu Januari 27, 2025 kwamba mizozo inaendelea kuinyima Afrika uwezo wake na inalitia hasara kubwa bara hilo.

Hasara hiyo inakadiriwa kufikia dola bilioni 18 kila mwaka na kuwafanya mamilioni ya Waafrika kuwa wakimbizi.
Rais Ruto amesema hayo kwenye mkutano muhimu wa AU uliofanyika jana mjini Nairobi na kuongeza kuwa, Afrika hivi sasa ina wakimbizi wa ndani milioni 35, wakimbizi milioni 8.9 wanaotafuta hifadhi nje ya nchi zao na milioni 1.1 ya watu wasio na utaifa.

Amesema: “Kati ya Aprili na Juni 2024 pekee, jumla ya matukio 1,000 ya ugaidi yalirekodiwa barani Afrika na kusababisha vifo vya watu 4,818.”
Mkutano huo wa siku nzima uliwaleta pamoja marais kutoka Guinea-Bissau, Ethiopia, Ghana na Comoro pamoja na Moussa Faki, mwenyekiti wa Kamisheni ya AU, ili kuharakisha mageuzi ndani ya Umoja wa Afrika AU wenye wanachama 55.

Rais Ruto amebainisha kuwa, Umoja wa Afrika kwa hivi sasa hauna uwezo wa kushughulikia changamoto changamano za bara hilo na kuna haja ya kuchukuliwa hatua za dharura za kubuniwa mara moja mbinu mpya za kuleta amani na usalama.

Pia amesema kuwa, ushiriki wa Umoja wa Afrika katika utatuzi wa migogoro mingi ya kikanda bado ni dhaifu, hakuna umoja na hakuna pia rasilimali za kutosha.

Rais huyo wa Kenya ameongeza kuwa, malengo ya maendeleo ya bara la Afrika yanatatizwa na nguvu kinzani zinazovuruga mambo.











Related Posts