ASKARI MKOANI SONGWE WAPEWA MAFUNZO MAALUMU NA MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI.

Na Issa Mwadangala

Joyce Njisya Meneja Usajili na Ukaguzi wa Maabara za Vinasaba na Sayansi Jinai kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali mkoani Dodoma akiwa ameambatana na Daud Yakobo ambaye ni Mkuu wa Maabara ya Uchunguzi wa Sayansi Jinai ya Baiolojia na Vinasaba kutoka Makao Makuu Dar-es salaam, wameendesha mafunzo maalumu kwa Maofisa, Wakaguzi na Askari wa vyeo mbalimbali mkoani Songwe Januari 28, 2025.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Bi.Joyce Njisya aliwajengea uelewa askari kuhusu kufuata sheria na usimamizi wa uchukuaji wa vinasaba ikiwa ni pamoja na kemikali na milipuko ambazo ni muhimu katika taratibu za kisheria ili kupata mafanikio ya kesi mahakamani.

Aliongeza kuwa, mafunzo hayo yanalenga kuongeza weledi na utendaji wa askari hao katika mchakato wa kisheria katika uchunguzi wa kisayansi pindi tunapochukua sampuli kwa ajili ya vielelezo.

Bi. Joyce alisisitiza kuwa Jeshi la Polisi ni wadau muhimu na alieleza kuwa ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na Mamlaka hiyo ni muhimu sana katika kufanya uchunguzi wa kina na kitaalamu wa kesi za jinai ambao unaleta mafanikio mengi mahakamani kutokana na kesi hizo.

Kwa Upande wake, Daud Yakobo alilipongeza Jeshi la Polisi kwa ushirikiano mkubwa na mamlaka hiyo, hasa katika uchukuaji wa sampuli mbalimbali ikiwemo vinasaba (DNA).

Vilevile Bw. Daud alibainisha kuwa mchango wa Jeshi la Polisi ni muhimu katika kusaidia uchunguzi wa kisayansi kufanyika kwa weledi na kwa wakati muafaka.

“Tunatambua na kuthamini mchango wenu mkubwa katika kusaidia uchunguzi wa kisayansi kwa njia ya kitaalamu na kwa wakati muafaka na jambo hilo limekuwa likisaidia kupata mafanikio mahakamani na imekuwa funzo kwa jamii na imefanya jamii kuogopa kufanya makosa hayo ya kikatili” alisema Bw.Daud.

Naye, Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Songwe Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Johnny Maro ameshukuru kwa mafunzo hayo na kueleza kuwa yamewaongezea ujuzi na maarifa zaidi na ameahidi kuwa kupitia mafunzo hayo, kutaongeza weledi zaidi katika utendaji kazi za kiuchunguzi wa makosa ya sayansi ya jinai na kuendelea kuleta mafanikio zaidi mahakamani.

Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uelewa na uwezo wa kiutendaji kazi za uchunguzi wa kisayansi na kuelewa majukumu ya kisheria na umuhimu wa kufuata taratibu sahihi katika utekelezaji wa matukio hayo

Related Posts