Jinsi wanafunzi walivyopigwa na radi Bukombe

Bukombe. “Jana mchana tukiwa darasani mvua ilikuwa ikinyesha na radi nying, wanafunzi wenzangu wakawa wanapiga kelele nikatoka kwenye dawati nikasogea mbele kufika mbele, nageuka nikamuona niliyekuwa nimekaa naye ameungua shingoni na tumboni.”

Haya ni maneno ya Yohana Edward mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Businda aliyelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Bukombe baada ya kujeruhiwa na radi iliyopiga kwenye darasa lao na kusababisha vifo vya wanafunzi saba na majeruhi 82.

Tukio la radi lilitokea jana Januari 27,2025 baada ya mvua kubwa iliyoambatana na radi wilayani Bukombe wakati wanafunzi wa wakiwa darasani wakiendelea na masomo.

Mwanafunzi huo amesema baada ya kuona wenzake wawili wameungua, chumba cha darasa kilikuwa na harufu kali ya moto wa makuti, alianguka chini huku akisikia kelele ambazo hakuweza kujua ni za nini na badaye kuanza kutokwa na damu mgongoni.

Mkuu wa mkoa wa Geita, Martin Shigela akimjulia hali mwanafunzi Yohana Edward aliyelazwa katika hospitali ya Wilaya ya Bukombe baada ya yeye na wenzake 81 kujeruhiwa na radi wakati wakiwa darasani.

“Ni kama nilipigwa butwaa siwezi kuongea wala kujisogeza japo naona ndipo walimu walifika na kutubeba alafu sikuelewa tena kinachoendelea hadi nilipojikuta niko hapa hospitalini,”amesema Edward.

Edward amesema kwa sasa hali yake inaendelea vizuri japo ana maumivu kidogo ya mwili.

Mwalimu wa shule hiyo, Shukuru Isack amesema tukio hilo lililotokea mchana wakati walimu wakiwa kwenye kikao ofisini kwa mkuu wa shule.

“Bahati mbaya radi hii imepiga kwenye madarasa mawili ambayo ni kidato cha tatu B na E tulipoingia kwenye hayo madarasa watoto walikua kwenye hali mbaya tuliwapeleka hospitali ndio wakawa wengine wameshafariki dunia na hao majeruhi wakaendelea na matibabu,”amesema Mwalimu Isack.

Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Paskas Muragili amewataja wanafunzi waliopoteza maisha ni Erick Bugalama (18) Erick Akonay(18) Niacs Paul (17) na Peter Mkinga(18).

Wengine ni Gabriel Makoye (17) Asteria Mkina (16) na Doto Masasi (17).

Mkuu wa wilaya Bukombe, Paskas Muragili akiwajulia hali wanafunzi wa shule ya Sekondari Businda waliolazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Bukombe kwa matibabu baada ya kupigwa na radi wakati wakiwa darasani.

Mkuu huyo wa wilaya amesema kati ya wanafunzi hao, waliopoteza maisha sita ni wavulana na mmoja ni msichana.

Muragili amesema tayari Serikali imewasiliana na familia za watoto hao na wataagwa kwa pamoja Alhamisi katika viwanja vya shule hiyo ili wanafunzi wenzao na jamii iwaage kwa pamoja.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela amesema Serikali itagharamia gharama za mazishi kwa kushirikiana na familia. “Watoto wetu walioko hospitali watatibiwa na Serikali itabeba gharama, vilevile wale waliopoteza ndugu zao tutaongea na familia juu ya taratibu za mazishi ambao wanautaka na tutaona namna ya kusaidia,”amesema Shigella.

Amesema kati ya majeruhi 82 waliokuwa wamelazwa hospitalini 73 kati yao wameruhusiwa na waliobaki wakiendelea na matibabu ni tisa.

Amesema uchunguzi wa awali umebaini mfumo wa kuzuia radi unaowekwa chini ya ardhi, kwenye madarasa yaliyopigwa na radi hayakuwa yamewekwa mfumo wa radi.

Amezitaka halmashauri,taasisi zote za umma kwa kushirikiana na wataalamu wa mfumo wa kuzuia radi kupitia majengo yote na kuhakikisha yanafungwa mfumo wa kuzuia radi ili kuepuka madhara.

Related Posts