Kagera Sugar yaivutia kasi Yanga

KAGERA Sugar imetamba kwamba haiifuati Yanga jijini Dar es Salaam kinyonge, bali imejipanga kukabiliana ipasavyo na mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara katika mchezo utakaopigwa Jumamosi, wiki hii.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kagera Sugar, Thabity Kandoro alisema wamekuwa na maandalizi mazuri kwa ajili ya michezo ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara wakijivunia baadhi ya nyota wapya waliojiunga na timu hiyo katika dirisha dogo la usajili.

Miongoni wa nyota wapya waliojiunga na timu hiyo ni pamoja na mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara 2021-2022, George Mpole kutokea Pamba akiungana na Omary Buzungu (Mtibwa Sugar), Moubarack Amza (Namungo FC) na Saphan Siwa (Tusker FC ya Kenya).

“Wachezaji wote tuliowasajili waliingia kambini na kuendelea na programu mbalimbali za benchi la ufundi. Tunashukuru kwa kiasi kikubwa tuliowahitaji tulifanikiwa kuwapata sasa tunajipanga upya kwa ajili ya kuongeza ushindani kwa msimu huu,” alisema.

Kagera inacheza na Yanga huku ikiwa na kumbukumbu ya kuchapwa mabao 2-0 katika mechi ya mzunguko wa kwanza iliyopigwa Agosti 29, mwaka jana kwenye Uwanja wa Kaitaba-Bukoba yaliyofungwa na Maxi Nzengeli dakika ya 25 na Clement Mzize ile ya 89.

Katika hatua nyingine, Kandoro alisema kabla ya timu hiyo kuanza safari kuifuata Yanga walitarajia kucheza mchezo mmoja wa kirafiki ambapo walikipiga na Pamba Jiji mjini Mwanza na kufungana mabao 2-2.

Related Posts