Vijana wa Kijiji cha Masoko Kata ya Mlangali Wilaya ya Mbozi Mkoa wa Songwe wametakiwa kuacha kucheza au kujiingiza katika uchezaji wa kamari ambao kwa asilimia kubwa unapelekea matatizo ya changamoto ya afya ya akili.
Kauli hiyo ilitolewa Januari 27, 2025 na Polisi Kata ya Mlangali Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Robart Kasunga alipofanya kikao na vijana hao na kuwaeleza kuwa ni lazima kila kijana kujitambua na kutumia ujana wake kwa hekima na kuacha kujitafutia kipato cha kusadikika ambacho mara nyinyi hupelekea changamoto ya afya ya akili ambayo huathiri mfumo wa maisha ya mtu katika mipangilio yake ya maisha ya kila siku.
“Vijana ni taifa la leo jitafutieni kipato cha halali ambacho kitawakwamua katika maisha yenu kama vile biashara na kilimo na acheni tabia ya kucheza kamari za mabonanza ikiwa ni pamoja na kubet kwani vitendo hivyo vitawapelekea kujiingiza katika vitendo vya kihalifu na kusababisha kupoteza dira yenu ya maisha na wengi wenu mtaishia jela na kuziacha familia zenu zikiwa tegemezi ikiwa ni pamoja na kuzalisha watoto wa mtaani” alisema Mkaguzi Kasunga.
Mkaguzi Kasunga aliwaasa kuacha tabia ya kuwa na tamaa na wanafunzi ambayo itasababisha kuwafanyia vitendo vya ukatili, pia aliwataka kuheshimu haki na Sheria za Nchi na kujituma kwa kufanya kazi halali ili kuweza kujitafutia kipato endelevu kitakacho wakwamua katika maisha yao.