Lissu kuanza kazi rasmi ya uenyekiti Chadema kesho

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Tundu Lissu anatarajiwa kuripoti makao makuu ya chama yaliyopo Mikocheni, Dar es Salaam kesho Januari 29, 2025 saa tano asubuhi na kuanza rasmi majukumu yake mapya.

Lissu ataambatana na Makamu Mwenyekiti Bara, John Heche na Naibu Katibu Mkuu Bara, Amani Golugwa.

Katika uchaguzi mkuu wa chama hicho uliofanyika Januari 21 na 22, 2025 jijini Dar es Salaam, Lissu alishinda nafasi ya uenyekiti kwa kupata kura 513 sawa na asilimia 51.5, akimshinda aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe aliyepata kura 482 sawa na asilimia 48.3 huku Odero Charles Odero akipata kura 1 sawa na asilimia 0.1.

Taarifa iliyotolewa leo Januari 28, 2025 na Msaidizi wa Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya nje, Apolinary Margwe inaeleza kuwa, Lissu na ujumbe wake utapokewa na Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika pamoja na watendaji wa makao makuu.

“Chama kinawakaribisha viongozi wakuu wa chama kutoka Zanzibar, viongozi wakuu wa mabaraza ya chama, viongozi wa Kanda ya Pwani na viongozi kutoka maeneo mengine kumsindikiza mwenyekiti wa chama akiripoti rasmi makao makuu ya chama,” amesema.

Margwe pia, amesema Lissu atazungumza na waandishi wa habari ikiwa ni siku ya kwanza kuingia kazini.

Related Posts