Dodoma. Wakati Shirika la Afya Duniani WHO likiweka uwiano wa madaktari 22.8 kutibu watu 10,000 kwa nchi zinazoendelea, Tanzania imebainika kuwa na uwiano wa madaktari 8.4 wanaotibu watu 10,000 sawa na theluthi moja.
Hayo yamesemwa leo Januari 28, 2025 na Naibu Waziri katika Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Stanslaus Nyongo kwa niaba ya Waziri wa Afya, wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalumu, (CCM) Husna Sekiboko.
Mbunge huyo alitaka kufahamu ni upi uwiano wa daktari na wagonjwa nchini.
Akijibu swali hilo, Nyongo amesema kwa sasa hapa nchini uwiano wa daktari na wagonjwa ni sawa na theluthi moja ya viwango vilivyopendekezwa na WHO kwa nchi zinazoendelea ambapo inapendekezwa uwepo wa uwiano wa madaktari 22.8 kwa kila watu 10,000.
Amesema kuwa katika nchi zilizoendelea uwiano ni madaktari 2.4 kwa watu 1,000.
Katika swali la nyongeza, Mbunge wa Mlalo (CCM) Rashid Shangazi amesema madaktari wengi wako katika ngazi ya shahada ya kwanza, lakini katika ngazi ya vituo vya afya na zahanati wako waganga wasaidizi na matabibu ambao wanahudumia jamii kubwa ya Watanzania.
“Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha katika ngazi za msingi tunakuwa na assistant medical officers (waganga wasaidizi) na clinical officers (matabibu) wengi zaidi kuliko hao madaktari ya ngazi ya shahada,” amesema.
Akijibu swali hilo, Nyongo amesema Serikali imeendelea na juhudi za kuajiri madaktari kwa maana wenye shahada ambapo mwaka 2022/23 iliajiri madaktari 1,200.
Amesema mwaka 2023/24 iliajiri madaktari 1,500 lakini inaendelea na kutoa vibali vya kuajiri madaktari wa kada ya chini yaani madaktari wasaidizi na matabibu kwa lengo la kutoa huduma kwa wananchi.
Amesema katika mwaka 2024/25, Serikali imetoa vibali 12,000.