Mambo 15 azimio la Dar es Salaam la nishati

Dar es Salaam. Wakuu wa Nchi za Afrika wameazimia kutengeneza mazingira bora ya kisera na kisheria ili kuwezesha ushiriki wa sekta binafsi katika uwekezaji kwenye mnyororo wa thamani wa sekta ya nishati.

Azimio hilo ni moja kati ya 15 yaliyotolewa jijini Dar es Salaam, katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika Kuhusu Nishati, uliwakutanisha marais 21 na viongozi wengine waliowakilisha mataifa yao.

Mkutano huo, ulitanguliwa na mkutano wa mawaziri wa kisekta uliofanyika jana ambao pamoja na mambo mengine, wadau waliibua hoja ya umuhimu wa maboresho ya kisera ili kurahisisha uwekezaji katika sekta ya nishati.

Maboresho ya kisera, yanatazamwa kuwa ufunguo wa mkwamo wa uwekezaji kwenye umeme na kufanya watu watu takriban milioni 600, kukosa huduma hiyo.

Maazimio hayo kwa pamoja, yanalenga kutimiza lengo la kufikisha huduma ya umeme kwa watu milioni 300 Afrika ifikapo mwaka 2030, ikiwa ni matokeo ya mkutano huo ulioratibiwa na Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).

Akisoma azimio hilo, Katibu Mkuu wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB), Profesa Vincent Nmehielle amesema wametambua uongozi wa Rais Samia kwa kuwa mwenyeji wa mkutano huo, kadhalika kuwa kinara wa ajenda ya nishati safi ya kupikia.

Sambamba na hilo, wameazimia kuutambua mchango wa Benki ya Dunia na AfDB kwa jitihada zao za kihistoria na mageuzi, kadhalika uongozi wa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU).

Pia, wameazimia kukubaliana kuwa, karibu Waafrika milioni 600 hawajafikiwa na umeme huku karibu bilioni moja hawatumii nishati safi ya kupikia, licha ya hatua zilizopigwa.

Kwa mujibu wa Profesa Nmehielle, wametambua ili kufikia lengo namba saba la Umoja wa Mataifa kuhusu nishati mbadala kwa gharama nafuu, linahitaji jitihada za pamoja na uwekezaji katika mnyororo wote wa thamani wa sekta ya nishati.

“Tunahitaji kuwa na mipango ya pamoja kama vile mkataba wa nishati ili kuhakikisha tunatekeleza hilo mwishoni mwa mwaka 2025,” alisema.

Amesema wameazimia kutambua umuhimu wa ushirikiano na kutafuta fedha kwa ajili ya Ajenda300.

“AfDB na Benki ya Dunia zimelenga kuhakikisha watu milioni 250 wanafikiwa na umeme kupitia mradi huo,” amesema.

Amesema kwa pamoja wamezipongeza taasisi hizo za fedha kwa ajili ya kutenga fedha za kufadhili mpango huo hadi mwaka 2030 na kuvutia mitaji kutoka sekta binafsi.

“Tunatambua fedha hizi zinahitaji kutumika kwenye malengo yaliyokusudiwa,” amesema.

Amezipongeza taasisi za fedha za kimataifa zilizoahidi kutoa fedha kwa ajili ya kuwezesha miradi ya upatikanaji wa umeme barani Afrika.

Azimio lingine amesema wanashukuru kwa mchango wa wadau kuhakikisha utekelezwaji wa Mpango wa IDA 21 na kupata fedha kwa ajili ya miradi ya muda mrefu ili kuwezesha upatikanaji wa nishati.

Kwa mujibu wa Profesa Nmehielle, wametambua juhudi za AU kwa ajili ya kupata huduma ya umeme, utangamano wa kikanda na majukumu ya kimkakati ili kuwa na soko la pamoja la nishati na mpango kabambe wa Ajenda300.

“Tunatambua sekta binafsi ina mchango mkubwa katika mnyororo wa thamani kwenye sekta ya nishati, hivyo kutengeneza mazingira wezeshi kwa sekta binafsi ni jambo la muhimu,” amesema.

Wamekubaliana maono ya kimataifa kwamba nishati ni sehemu muhimu ya kutokomeza umasikini, kuboresha afya na kuchochea ujenzi wa viwandani kuhamasisha maendeleo ya kiuchumi kupitia viwanda.

Azimio lingine ilikuwa ahadi ya kuhakikisha wana imarisha na kuboresha miundombinu ya uzalishaji, usambazaji na kufikisha umeme kwa wateja kwa gharama nafuu.

Alieleza hilo litatekelezwa sio tu kwa kutumia rasilimali za ndani bali mifumo shindani ya manunuzi kwa kuwavutia wazabuni wenye uwezo.

“Kuleta msawazo katika utafutaji fedha kwa kuimarisha mifumo na mipango katika masuala ya bei na viwango na kuimarisha ushirikiano ili kunufaika na fursa ya uwepo wa vyanzo mbalimbali vya umeme,” amesema.

Amesema wanaahidi kutoa vivutio kwa sekta binafsi kwa kutengeneza mazingira ya kisera na hasa kujikita katika chambuzi za hasara na faida.

Wameahidi kuchukua hatua madhubuti za kuzijengea uwezo taasisi na kutengeneza ushirikiano na wadau na kuzingatia usawa wa jinsia.

Kuwekeza katika utengaji wa bajeti za ndani na kuunganisha na msaada wa fedha kutoka kwa wadau wa kimataifa katia kutekeleza mipango hiyo.

Maazimio 15 wameiomba AU kuwezesha uwasilishaji wa azimio hilo katika Baraza Kuu la Umoja wa Afrika kwa ajili ya kuridhia azimio.

Chimbuko la Azimio la Dar es Salaam

Katika Mkutano wa Nishati Safi ya Kupikia Afrika uliofanyika Mei 2024 katika makao makuu ya Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO), Paris nchini Ufaransa, Rais Samia alitoa wito wa kuongeza ufadhili wa Mfuko wa Maendeleo ya Afrika (African Development Fund) ili kufanikisha azma ya kuhakikisha nishati safi ya kupikia kwa wote ifikapo mwaka 2030.

Alisisitiza kuwa changamoto kama ukosefu wa fedha za kutosha na uelewa mdogo kuhusu fursa za kiuchumi ndani ya sekta ya nishati safi zinakwamisha juhudi za kuboresha teknolojia za kupikia.

“Ukosefu wa utafiti wa kina na ubunifu vinachangia kuzuia maendeleo ya suluhisho bora za nishati safi ya kupikia,” alisema Rais Samia.

Pia, aliitaka jamii ya kimataifa kuweka juhudi zaidi katika kutatua changamoto hizi kwa lengo la kuleta mabadiliko chanya kwa sayari na maisha ya watu.

Mkutano huo, ulioratibiwa na Clean Cooking Alliance (CCA) kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Nishati (IEA), ulikuwa sehemu ya juhudi za kufanya mwaka 2024 kuwa hatua muhimu katika kufanikisha upatikanaji wa nishati safi kwa wote.

“Zaidi ya Waafrika milioni 900 wanategemea suluhisho zisizo salama za kupikia, hali inayosababisha uharibifu wa mazingira, kupotea kwa bioanuwai na hatari kubwa za kiafya,” alisema Rais Samia.

Rais Samia alitaja changamoto tatu kuu zinazokwamisha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia barani Afrika kuwa ni ukosefu wa suluhisho bora, nafuu na endelevu, ukosefu wa umakini wa kimataifa juu ya suala hili na ukosefu wa ushirikiano wa kimkakati.

Kwa kukabiliana na changamoto hizi, Rais Samia alisisitiza utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Kupikia kwa Njia Safi wa miaka kumi, unaolenga kufanikisha asilimia 80 ya Watanzania kutumia suluhisho safi za kupikia ifikapo mwaka 2034. Aidha, Tanzania itaendeleza Programu ya Msaada wa Wanawake wa Afrika kwa Nishati Safi ya Kupikia (AWCCSP) ili kuwawezesha wanawake kama mawakala wa mabadiliko ya kijamii na kiuchumi.

Mwito kwa viongozi wa Dunia

Rais Samia aliwataka viongozi wa dunia kuhakikisha kwamba nishati safi ya kupikia inakuwa sehemu muhimu ya mabadiliko ya haki ya nishati.

“Hili ni suala linalohitaji kipaumbele si tu kwa ajili ya Afrika bali pia kwa mustakabali wa sayari yetu. Tunahitaji kuchukua hatua za pamoja kuhakikisha kuwa kila mtu anapata fursa ya kutumia nishati safi ya kupikia ambayo ni salama kwa afya na mazingira,” alihitimisha Rais Samia.

Related Posts