Mbunge CCM ahoji utekaji bungeni, Spika Tulia ampa utaratibu

Dodoma. Mbunge wa Iringa Mjini (CCM), Jesca Msambatavangu ameihoji Serikali imejipangaje kudhibiti wizi wa binadamu maarufu utekaji.

Swali hilo limekuja wakati ambao kuna matukio ya utekaji yaliyotokea mwaka 2023 na 2024 huku baadhi ya wanasiasa na wafanyabiashara wakidaiwa kutekwa na watu wasiojulikana.

Matukio hayo yaliyotikisa ni mauaji ya kada wa mjumbe wa sekretarieti ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Ali Kibao aliyetekwa Septemba 6, 2024 akiwa katika basi la Tashriff akielekea nyumbani kwao mkoani Tanga kutoka Dar es Salaam.

Septemba 8, 2024, mwili wake uliokotwa eneo la Ununio ukiwa umeharibika.

Novemba 13, 2024 mfanyabiashara wa Kiluvya jijini Dar es Salaam, Deogratius Tarimo alinusurika kutekwa na watu wasiojulikana baada ya jaribio la kumwingiza kwa nguvu ndani ya gari yao kushindikana. Wahusika walikamatwa na kesi inaendelea mahakamani.

Desemba 1, 2024, pia Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana wa Chama cha ACT Wazalendo, Abdul Nondo alitekwa na watu wasiojulikana katika Kituo cha Mabasi cha Magufuli kilichopo Mbezi Luis Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam.

Leo Jumanne, Januari 28, 2025, akiuliza swali la nyongeza bungeni, Msambatavangu amesema kuna vijana wawili wa mkoani Iringa wamepotea katika matukio ya utekaji.

“Serikali imejipangaje kudhibiti wizi wa binadamu maarufu utekaji kwa kuwa, sisi Iringa tumeshapoteza vijana wetu wawili Danes Nyato na kijana mmoja anaitwa Ali kwa kutekwa sasa Serikali imejipangaje kudhibiti wizi wa binadamu,” amesema.

Hata hivyo, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amemtaka kuleta swali hilo kama msingi ili Serikali iweze kujibu kikamilifu.

“Mheshimiwa Jesca Msambatavangu lete kama swali la msingi ili Serikali iweze kujibu kikamilifu,” amesema Dk Tulia.

Katika swali la msingi, Mbunge wa Rorya (CCM), Jafari Chege amehoji ni lini wizi wa mifugo utadhibitiwa wilayani Rorya.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Daniel Sillo amesema Jeshi la Polisi lina wajibu wa kudhibiti wizi wa mifugo Rorya.

“Jitihada zinazofanywa na Jeshi la Polisi ni pamoja na kutoa elimu juu ya ulinzi jirani, kuanzisha vikundi vya ulinzi shirikishi na mazizi salama,” amesema.

Amesema jitihada nyingine ni kuimarisha kikosi cha kupambana na wizi wa mifugo STPU (Stoke Theft Prevention Unit) kwa kuongeza askari na vitendea kazi.

Pia, kufanya mikutano ya ujirani mwema na polisi Wilaya ya Nyatike ya nchini Kenya juu ya udhibiti wa makosa yanayovuka mipaka na jitihada zote hizi ni endelevu na zimepunguza kwa kiasi kikubwa wizi wa mifugo.

Amesema takwimu zinaonyesha Desemba, 2023 na Januari, 2024 kumeripotiwa matukio 26 na kipindi kama hicho Desemba, 2024 na Januari, 2025 kumeripotiwa matukio 9, sawa na upungufu wa matukio 17.

Katika swali la nyongeza, Chege amesema pamoja na jitihada zinazofanywa na Serikali za kudhibiti wizi wa mifugo bado upo na unawaathiri wananchi kiuchumi.

“Kama Serikali haioni kuwa ni wakati muwafaka wakuja na mbinu mbadala badala ya zilizozoeleka kwa sababu, wizi umechukua zaidi ya miaka 20 kwenye eneo lile,”amehoji Chege.

Akijibu swali, Sillo amesema kwa sasa njia wanayopendekeza ni kuimarisha ulinzi shirikishi na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu suala zima la wizi wa mifugo Wilaya ya Rorya.

Related Posts