Mcolombia afichua jambo Azam | Mwanaspoti

MSHAMBULIAJI wa zamani wa Azam FC, Franklin Navarro (25), amesema sababu iliyochochea kushindwa kuonyesha makali katika Ligi Kuu Bara akiwa na matajiri hao wa Chamazi ni majeraha ya kifundo cha mguu.

Navarro ambaye alikuwa akisumbuliwa na kifundo cha mguu, siku chache zilizopita alitangazwa kujiunga na Union Magdalena ya Colombia baada ya kuachana na Azam FC kwa makubaliano ya pande mbili.

Nyota huyo alisema alikumbwa na maumivu katika mchezo dhidi ya Simba uliochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza Februari 9, 2024, na majeraha hayo ndiyo yaliyochangia kushindwa kuonyesha makali.

Navarro ambaye aliyejiunga na Azam FC, Januari mwaka jana akitokea Colombia kwa matarajio makubwa, alisema kuwa alijua ni wakati wa kuchukua nafasi na kujitokeza kama mshambuliaji mwenye uwezo wa kufanya mabadiliko katika timu hiyo.

Hata hivyo, alikiri kwamba hali ya majeraha ilimkwamisha na alishindwa kufanya kile alichotarajia.

“Nikiwa Azam FC nilijua mashabiki wangenitegemea kutengeneza mabao na kuwa na mchango mkubwa katika ushindi wa timu. Lakini, wakati nilianza kuzoeana na wachezaji wenzangu na kujipanga, majeraha ya kifundo cha mguu yalinirudisha nyuma na kimsingi nilishindwa kufikia kiwango cha juu,” alieleza Navarro.

Alisema alijitahidi kufanya mazoezi, lakini hali ya majeraha ilimtesa.

“Kama mchezaji unapojikuta na majeraha yanayokukwamisha kufanya kile ambacho unaweza ni vigumu sana. Nilijua ili nifanikiwe lazima nipate muda wa kupumzika na kurejea kwa nguvu mpya,” aliongeza mchezaji huyo.

Alidai kuchukizwa kwa kushindwa kuonyesha kile ambacho mashabiki walikuwa wanakitaka, jambo lililomvuruga kiakili na kumfanya kuona amekosa nafasi nzuri katika historia ya Azam FC.

Related Posts