Arusha. Halmashauri ya Jiji la Arusha imenunua mitambo mipya mitatu yenye thamani ya Sh1.7 bilioni kwa ajili ya ukarabati wa barabara za ndani.
Mitambo hiyo iliyozinduliwa leo Januari 28,2025 na Meya wa Jiji la Arusha Maxmillian Iranghe ni greda aina ya Catapiler -Model 140GC pamoja na malori mawili (SINOTRUK-ModI HOWO) yaliyonunuliwa kwa fedha ya mapato ya ndani ya mwaka wa fedha 2024/25.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mitambo hiyo, Mkurugenzi wa Jiji la Arusha John Kayombo amesema inakwenda kujibu kilio cha muda mrefu cha wananchi ikiwamo changamoto ya barabara korofi hasa zinazoharibiwa na mvua.
Amesema halmashauri hiyo ilitenga Sh2 bilioni kwa ajili ya ununuzi wa mitambo na malori.
“Kwa neema ya Mungu tumeweza kununua nyenzo hizo kwa thamani ya Sh1.7 bilioni na fedha zilizobaki zitagawanywa kwa kila kata, kiasi cha shilingi milioni nne kwa ajili ya ununuzi wa vifusi,” amesema.
“Madiwani wangu walikuwa kwenye wakati mgumu sana kwa tatizo la ubovu wa barabara, tena wengine waliburuzwa kwenye matope ila kwa sasa madiwani wangu tembeeni vifua mbele hakuna diwani atakayepata shida tena.”
Awali, mhandisi wa jiji hilo, Jacob Mwakiambiki amesema mitambo na malori hayo mawili yamenunuliwa kwa fedha za ndani baada ya halmashauri hiyo kutenga Sh2 bilioni kupitia bajeti yake ya mapato ya ndani kwa mwaka wa fedha 2024/25.
“Ndani ya mwaka huu wa fedha, Jiji la Arusha limefanikiwa kununua mtambo mmoja na malori mawili kwa ajili ya kutatua ukarabati na matengenezo ya barabara za ndani,” amesema Mwakiambiki.
“Catapiler ni Sh1.3 bilioni na gharama za malori mawili ni Sh413.2 milioni pamoja na VAT,” amesema.
Kwa upande wa Meya Iranghe amewataka wananchi na madiwani kutunza mitambo hiyo ili iweze kudumu na kufanya kazi iliyokusudiwa.
” Naomba jamani tutunze mitambo hii na tusikubali kunyamaza pale tunapoona inachepushwa kufanya kazi isiyo ya malengo yetu, kwani Arusha tunakwenda kutangaza sasa kero ya barabara imekwisha na kuwa na hadhi ya jiji la kitalii,” amesema.
Diwani wa Terrat, Francis Mbise amesema kero ya barabara ndani ya Jiji la Arusha ni changamoto kubwa sana, hivyo wanaishukuru Serikali kuridhia kupitishwa kwa bajeti ya ununuzi wa mitambo hiyo.