*Ni baada ya Jiji hilo kuzindua mitambo ya kuchonga barabara ya Bilioni 1.7
Na Seif Mangwangi, Arusha
MKURUGENZI wa Jiji la Arusha, John Kayombo amesema kuanzia sasa hakuna diwani ndani ya Jiji la Arusha atakayedhalilishwa kwa kutembezwa na wananchi kwenye madimbwi ya maji kutokana na ubovu wa barabara kama ilivyotokea kwa diwani wa kata ya Murieti Francis Mbise kufuatia jiji hilo kununua mitambo mipya ya kuchonga barabara.
Disemba 16 mwishoni mwa mwaka jana 2024, wananchi wa kata ya murieti waliwakamata viongozi wa kata hiyo akiwemo Diwani wa kata hiyo Francis Mbise na kuwatembeza kwenye madimbwi makubwa ya maji katikati mwa barabara zinazokatiza katika kata hiyo wakishinikiza Serikali kuwachongea barabara.
Kayombo amesema tatizo kubwa la barabara mbovu na korofi ndani ya Jiji la Arusha linaenda kumalizwa kabisa baada ya Halmashauri ya Jiji hilo kununua mitambo yake binafsi ya kuchonga barabara za mitaa yenye thamani ya bilioni 1.7.
Akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa mitambo hiyo leo Januari 28, 2025
Mkurugenzi wa Jiji la Arusha John Kayombo amesema mitambo hiyo imenunuliwa kwa fedha zilizotokana na mapato ya ndani ya Jiji la Arusha ambapo jumla ya bilioni2 zilitengwa huku bilioni 300 zilizosalia zikigawanywa kwa kila kata ili kununulia vifusi.
“ Mitambo hii tumenunua kwa fedha zetu za ndani, hivyo ni jukumu la kila mkazi wa Arusha kujivunia uwepo wa mitambo hii, na hivyo napenda kutoa rai kwa kila mwana Arusha kuwa mlinzi wa mitambo hii,”amesema.
Amesema katika ununuzi huo, greda la kuchonga barabara limegharimu zaidi ya bilioni 1.3, malori makubwa mawili yamenunuliwa kwa zaidi ya milioni 400 ambapo jumla ya mitaa 154 katika kata 25 zinatarajiwa kufikiwa.
Meya wa Jiji la Arusha Maximilian Iraghe amesema Jiji hilo liliamua kuweka bajeti ya kununua mitambo hiyo ambayo ni greda la kuchonga barabara pamoja na malori makubwa matatu kwa kuwa barabara nyingi ndani ya Jiji hilo ni mbovu na haziko kwenye mpango wa kutengenezwa na Tarura.
Amesema barabara zinazotengenezwa na Tarura ni zile zenye upana wa mita 12 huku barabara nyingi zinazokatiza mitaani zina upana wa mita 4 hadi 8 na hivyo kuzifanya zisiweze kupitika na kuleta kero kwa wananchi.
Meya Iraghe amewataka madiwani pamoja na watendaji wa mitaa ndani ya jiji hilo kuhakikisha wanaelekeza wananchi kutofanya shughuli za ujenzi ndani ya hifadhi za barabara zinazokatiza kwenye mitaa yao ili kuwapa urahisi wajenzi pindi watakapopita kuchonga barabara mitaani kwao.