NA VICTOR MASANGU,
Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini Silvestry Koka ameungana kwa pamoja na umoja wa wanawake wa (UWT) Wilaya ya Kibaha mjini katika kumuunga mkono Rais wa awamu ya sita Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kupitishwa na mkutano mkuu wa chama kuweza kugombea tena nafasi ya Rais katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu 2025.
Koka ameyasema hayo wakati akifungua kikao cha baraza la UWT Wilaya ya Kibaha mjini ambapo amesema kuwa Rais Samia ameweza kufanya mambo makubwa katika kutekeleza Ilani ya chama kwa vitendo ikiwemo kutoa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mbali mbali ya maendeleo na kuwataka wanawake hao kuachana na migogoro na makundi ambayo hayana faida ndani ya chama.
Aidha Koka alisema kwamba anatambua wanawake ni jeshi kubwa hivyo wanapaswa kuhakikisha wanajipanga kwa kuwa na umoja na mshikamano wa pamoja katika kumpa sapoti ya kutosha ili aweze kushinda kwa kishindo katika uchaguzi mkuu wa nafasi ya Urais na kwamba wanatakiwa kuwa mstari wa mbele na kuachana na wote wowote katika kumpambania Rais Samia.
“Kwa upande wangu mimi kama Mbunge wenu namshukuru sana kwa dhati Rais wetu kwani ameweza kufanya mambo mengi hivyo wanawake wa UWT wa Jimbo la Kibaha mjini pamoja na maeneo mengine mnapaswa kutokufanya makosa na mnapaswa kuunga mkono juhudi za Rais na kuhakikisha anashinda kwa kishindo kwa asilimia kubwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Kadhalika Koka alimpongeza kwa dhati Rais Dkt, Samia kwa kuweza kuridhia maombi ya Halmashauri ya Kibaha mji na kuipa adhi ya kuwa Manispaa hivyo kutokana na kazi nzuri za utekelezaji wa majukumu yake ipasavyo ya anapaswa kupewa sapoti na ushirikiano wa hali na mali ili aweze kuendelea kuwatumikia wananchi na kutatua changamoto zao wanazozikabili.
Naye Mwenyekiti wa umoja wa wanawake (UWT) Wilaya ya Kibaha mjini Elina Mgonja ametumia kikao hicho kuwakumbusha wajumbe kwamba hawezi kuvumilia hata kidogo baadhi ya vikundi vya watu wachache ambao wenye tabia ya kukihujumu chama na kwamba endapo wakibainika watachukuliwa hatua kali za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine.
Alibainisha kwamba kumekuwepo na tabia ya baadhi ya wanawake kukichafua chama kwa kuvunja sheria na taratibu kwa kuendesha mipango kinyemela ambayo ni nje kabisa na miongozi ya chama na kwamba kwa sasa wamejipanga na kujizatiti ili kuweza kuwaandikia barua kwa lengo la kuwaonya.
Naye Katibu wa UWT Kibaha mjini Cecilia Ndaro akisoma taarifa ya utekelezaji kwa mgeni rasmi amesema kwamba hali ya kisiasa katika Halmashauri ya Kibaha mjini ni shwari na kwa sasa wanajipanga kwa ajili ya uchaguzi mkuu amabo unatarajiwa kufanyika mwaka huu wa 2025 na kuongeza kwamba wataendelea kuongeza idadi ya wanachama.
Mke wa Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mama Selina Koka ambaye pia ni mlezi wa UWT Wilaya ya Kibaha mjini aliwaomba wanawake hao kuendelea kumpa ushirikiano wa kutosha katika suala zima la kukijenga chama ikiwemo kuachana kabisa na kuwa na tofauti na makandokando na badala yake wawe kitu kimoja katika kuimarisha umoja wao.
Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kibaha mjini Mwalimu Mwajuma Nyamka amewataka wanachama wote kuweka misingi ya kuzingatia taratibu za chama na kuachana kabisa na tabia ya kuwa na propaganda na badala yake wajipange kwa ajili ya uchagzui mkuu wa mwaka 2025.
Kwa upande wake Katibu wa chama cha mapinduzi (CCM) Isack Kaleiya amebainisha kwamba kuna baadhi ya wanachama bado ni tatizo hivyo watahakikisha wale wote ambao wamekuwa wakienda kinyume na taratibu za chama watawajibishwa ipasavyo kwani chama hakitomuonea huruma hata kidogo mtu ambaye atakwenda kinyume.