Rais Samia ataja mikakati kuongeza umeme nchini

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ametaja mikakati minne itakayowezesha kuongeza upatikanaji wa nishati ya umeme barani Afrika ifikapo mwaka 2030.

Mikakati hiyo ni kuzalisha umeme kwa nishati mchanganyiko, kuongeza bishara ya umeme Afrika, kusambaza umeme vitongoji vyote Tanzania na kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Amesema hayo leo Jumanne Januari 28,  2025 katika mkutano wa nishati wa Afrika wenye kauli mbiu ya Ajenda 300.

Samia amesema unahitajika uwekezaji wenye thamani ya Dola 13 bilioni za Marekani (Sh32.79 trilioni) na kati ya hizo, Dola 5 bilioni (Sh12.61 trilioni) zitapatikana kupitia sekta binafsi nchini.

Akizungumzia uzalishaji wa umeme kwa nishati mchanganyiko, Samia amesema hadi sasa Tanzania ina uwezo wa kuzalisha megawati 3,431 na asilimia 58 ya hizo inatokana na vyanzo vya maji, asilimia 35 gesi asilia na asilimia saba vyanzo vingine.

“Shabaha yetu ni kuongeza megawati 2,463 za nishati kutokana na nishati ya jua, gesi ya asilia, upepo joto ardhi na vyanzo vingine,” amesema. 

Kuhusu biashara ya umeme Afrika, Samia amesema kijiografia Tanzania ni kiungo muhimu cha kuunganisha umeme Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika (Eastern Africa Power pool na Southern Africa Power pool),  hivyo kuwezesha biashara ya umeme kutoka Afrika Kuisini hadi Misri.

“Tayari tumeshaunganisha miundombinu ya umeme na nchi za Burundi, Kenya na Rwanda na sasa tunaendelea kuunganisha miundombinu ya umeme na nchi ya Zambia na Uganda.

“Kuwepo kwa miundombinu hiyo kutawezesha biashara ya nishati kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC),” amesema Rais Samia.

Amesema Tanzania ina nafasi ya kuuza umeme ikizingatiwa kuwa, mahitaji yake hadi kufikia Novemba 2024 yalikuwa megawati 1,888 wakati uzalishaji wake ni megawati 3,431.

Katika mkakati wa kufikisha umeme kwenye vitongoji vyote, amesema tayari Tanzania imeshafikisha umeme kwenye vijiji vyote.

“Mwelekeo wetu ni kufikia vitongoji vyote 64,359 hadi sasa tumeshavifikia 32,827 na kazi inaendelea katika vitongoji vingine. Hivyo, kupitia mpango huu tutaweza kufikia vitongoji 11,532 vilivyobakia,” amesema.

Kuhusu nishati safi ya kupikia, Samia amesema kwa Afrika watu milioni 950 barani Afrika wanakosa nishati hiyo.

“Hali hii inaligharimu sana bara letu na inahusishwa na kuongezeka kwa umaskini, vitisho vya afya, uharibifu wa mazingira, kuongezeka kwa kaboni kupotea baioanuai na kukosekana kwa usawa wa kijisia,” amesema.

Amesema kwa Tanzania utegemezi wa kuni na mkaa kupikia ni zaidi ya asilimia 90 jambo linalohatarisha afya na ustawi wa wanawake.

“Katika kukabiliana na hili,  Tanzania tumeweka mkakati wa nishati safi ya kupikia unaolenga kupandisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kutoka asilimia 10 ya sasa hadi asilimia 80 ifikapo mwaka 2034,” amesema.

Kuhusu mkutano huo, Samia amesema Tanzania ni moja kati ya nchi 12 zitakazozindua Mpango wa Nishati (National Energy Compact).

Amesema Tanzania inatarajia kuongeza kasi ya kuunganisha umeme nchini hadi kufikia asilimia 72 ifikapo mwaka 2030.

Awali, akizungumza katika mkutano huo, Rais wa Benki ya Dunia (WB), Ajay Banga amewataka wakuu wa nchi za Afrika kushirikiana na benki hiyo kuibua fursa za ajira kwa kuongeza nishati ya umeme.

“Mwelekeo wetu ni kubadili maisha ya watu hawa na kuwapa matumaini na maono yetu ni kuhakikisha kwamba, tunatoa umeme kwa nusu ya watu wa bara hili wapatao milioni 300 (ambao hawapati umeme) na hicho kitakuwa kichocheo kikubwa cha kupata ajira,” amesema.

Akisisitiza zaidi ushirikiano, Banga amesema, “hakuna anayeweza kufanya peke yake, kidole kimoja hakivunji chawa, tunahitaji kushirikiana, mashirika ya utu hayawezi kufanya peke yake, Benki ya Dunia haiwezi kufanya peke yake, Benki ya Maendeleo ya Afrika haiwezi kufanya peke yake tunahitaji kushirikiana.”

Ameeleza pia haja ya kuisaidia sekta binafsi ili kuwezesha kupata umeme wa bei nafuu, akisema benki hizo za kimataifa ndizo zenye jukumu la kusaidia.

“Sekta binafsi ni wadau muhimu wanaopaswa kuwekeza katika mazingira ambayo watajiamini, wanahitaji kuwekeza kwenye mazingira bora ya uwekezaji,” amesema.

Naye, Rais wa Rockefeller Foundation, Dk Rajiv Shah amesema mkutano huo umerejesha historia ya Tanzania kupata umeme, akisema taa ya kwanza nchini humo iliwashwa mwaka 1908.

“Afrika imekuwa ikitafuta umeme kwa miaka 140, taa kwa mara ya kwanza zilikuja Dar es Salaam mwaka 1908, katika jitihada za kuleta nguvu ya pamoja, ninyi viongozi mmekuwa mkiweka baadhi ya mikakati ya kuhakikisha nyaya zinawekwa ili kupata umeme,” amesema Dk Shah.

Amesema karibu milioni 600 ya Waafrika hawana umeme na milioni 500 bado hawawezi kupata umeme wa bei nafuu kwa ajili ya uzalishaji ambao unahitaji kutengeneza ajira katika ulimwengu wa kidijitali.

Amesema Ajenda 300 itafanikiwa kwa sababu viongozi wa Afrika ndio wanaosimamia, hivyo kujitoa kwao na utashi wao wa kisiasa, kutawezesha usimamizi wa sera na kutoa mwongozo.

“Mission 300 inachagiza nchi tulizonazo katika kipindi ambacho tuna uhitaji mkubwa fedha na hasa kwako Ajay (Rais wa WB) kwa kutuleta pamoja na kusukuma gurudumu hili. Nadhani tutahitaji sekta binafsi ili kufanikiwa,” amesema Dk Shah.

Ametaja pia, uhusiano kati ya sekta binafsi na sekta ya umma akisema ni kichocheo cha mafanikio ya miradi ya umeme.

Related Posts