Goma. Kundi la waasi wa M23 wanaotajwa kufadhiliwa na Serikali ya Rwanda wanadaiwa kuuteka Mji wa Goma nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) baada ya mapigano yaliyodumu kwa wiki kadhaa dhidi ya vikosi vya jeshi la nchi hiyo (FARDC).
Kwa mujibu wa tovuti ya The Guardian, eneo lililotawaliwa na mapigano hayo lenye majimbo ya Ituri, Kivu Kusini na Kivu Kaskazini yanaundwa na makundi 129, kundi kuu ni la waasi wa M23.
Kwa mujibu wa The Guardian, ni vigumu kuzungumzia waasi wa M23 bila kutazama historia ya jamii ya Watutsi eneo la mashariki mwa DRC, jamii hiyo pia inapatikana nchini Rwanda.
Mwaka 2006 liliundwa Kundi la National Congress for the Defence of the People (CNDP) na viongozi wa Watutsi waliopo mashariki mwa DRC.
Kundi hilo liliibuka kutokana na kuibuka mvutano wa kikabila kati ya Watutsi na makabila mengine, hasusan baada ya mauaji ya Kimbari ya Rwanda mwaka 1994 na mgogoro wa wakimbizi nchini DRC.
Kundi la waasi la RCD, lililokuwa limedhibiti eneo la mashariki mwa DRC, lilikata tamaa kupata mwafaka wa kuingia kwenye maridhiano ya amani na Rais Joseph Kabila, wakihofia kupoteza ushawishi wao eneo hilo.
Wakiongozwa na Laurent Nkunda, CNDP ililenga kuwalinda raia wa Kitutsi dhidi ya mashambulizi ya makundi ya wanamgambo wa Kihutu na kupata uwakilishi bora wa kisiasa kwa Watutsi katika Serikali ya DRC chini ya Rais Kabila.
Kuundwa kwa CNDP kwa kiasi kikubwa kulitokana na kushindwa kwa mchakato wa amani na kutozingatiwa kwa mahitaji na usalama wa jamii ya Watutsi.
Vita vya kwanza na ya pili vya DRC kati ya mwaka 1996 hadi 2003 ziliingilia kati kisha mtandao tata wa ushirikiano wa kukabiliana na makundi hayo.
Mtandao ulilenga kukabiliana na makundi ikiwamo Congress of the National Congress for the Defence of the People (CNDP) na M23 ambayo ni mrithi wa CNDP.
Makundi hayo yanatuhumiwa kunufaika na mizozo ya ndani ya Serikali na biashara haramu ya madini kutoka migodi iliyopo mashariki mwa DRC.
CNDP, kikiongozwa na Laurent Nkunda, awali iliundwa ili kulinda jamii za Watutsi lakini ilijulikana kwa ukiukwaji wa haki za binadamu na biashara haramu.
Mnamo 2009, makubaliano ya amani yalitaka kuunganisha vikosi vya CNDP katika jeshi la DRC, lakini mvutano uliendelea na kusababisha kuundwa kwa M23 mnamo 2012.
Kundi hilo lilipewa jina baada ya makubaliano ya amani ya Machi 23, 2009 yaliyoahidi kuunganishwa kwa wapiganaji wa CNDP katika jeshi la DRC na kutambua mrengo wao wa kisiasa.
Hata hivyo, kikundi cha CNDP kilidai kuwa, makubaliano hayo hayakutekelezwa vyema na kuzaliwa kwa M23 ili kushinikiza madai yao.
M23 inadai kulinda jamii za Watutsi na wanaozungumza Kinyarwanda nchini DRC, ikitaja vitisho kutoka kwa wanamgambo wa Kihutu na kushindwa kwa Serikali kulinda usalama wao.
Licha ya madai hayo, kundi hilo limekuwa likishutumiwa kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu, ikiwamo mashambulizi dhidi ya raia.
Ripoti ya Umoja wa Mataifa (UN) inakadiria kuwa, kufikia Januari 2025, kundi la M23 lilikuwa na wapiganaji kati ya 3,000 na 4,000.
Hata hivyo, UN imekuwa ikiishutumu Rwanda kwa kufadhili kundi hilo tuhuma ambazo Rwanda imekuwa ikikanusha kila mara.
Balozi wa Rwanda katika Umoja wa Mataifa, Ernest Rwamucyo, jana alipokuwa akihutubia mkutano wa Baraza la Usalama la Afrika hakukanusha wala kuthibitisha madai hayo ya kuwa na mkono wao katika uvamizi huo wa M23.
Aidha, Rwanda imeendeleza madai kwamba, kundi la wapiganaji la FDRL lililotajwa kuhusika katika vita vya kimbari ya mwaka 1994, lilikimbilia DRC na linatumiwa na taifa hilo kuendeleza mauaji ya kimbari eneo la Mashariki mwa DRC, jambo ambalo Serikali ya DRC imekuwa ikikanusha.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Olivier Nduhungirehe aliieleza Associated Press (AP) kuwa uamuzi wa DRC kukatisha uhusiano wake na Rwanda ni kukiuka makubaliano ya kimataifa.
“Kwa upande wetu tumechukua hatua stahiki kuwaondoa wanadiplomasia wetu nchini DRC waliokuwa hatarini kudhuriwa na vikosi vya usalama vya Congo,” amesema Nduhungirehe.
Ripoti ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2022 iliangazia ushahidi wa vikosi vya ulinzi vya Rwanda kusaidia M23 na kuzidi kuzorotesha uhusiano kati ya Rwanda na DRC huku mzozo wa rasilimali ikiwamo madini ukitajwa kuwa sababu kuu ya vita hiyo.
M23 inaendelea kujitanua ndani ya DRC ambayo ni Taifa la nne kwa idadi kubwa ya watu barani Afrika, wanaokadiriwa kufika milioni 109 mwaka 2024.
Mashambulizi ya M23 yaliyoanza wiki moja iliyopita nchini DRC yamebadilisha upepo wa hali ya usalama Mashariki mwa DRC.
Tangu mwishoni mwa mwaka 2021, kundi hilo limeanzisha mashambulizi mapya, na kukamata maeneo ya kimkakati.
M23 ilitangaza kuuteka Mji wa Goma nchini DRC, Januari 27, 2025, kwa mujibu wa Al Jazeera, wapiganaji wa M23 waliteka Jiji la Goma ambalo ndio kubwa zaidi mashariki mwa DRC.
Mapigano ya silaha yalizuka karibu na uwanja wa ndege, kati ya vikosi vya FARDC vya DRC dhidi ya M23 na kuwalazimu maelfu ya raia kuyakimbia makazi yao kutafuta hifadhi.
Hili linaashiria mafanikio kwa M23, kwani Goma ni kitovu cha kiuchumi na kiutawala.
Mbali na Goma, M23 walianza kwa kuyateka majimbo la Sake, Masisi, Babmbiro na Luberoo, Desemba 2024 hadi Januari 27, mwaka huu. Mji wa mwisho kutwaliwa na wapiganaji hao ulikuwa Sake ambao uko takriban kilometa 23 kutoka Goma.
M23, pia imeukamata Mji wa Minova nchini DRC wiki kadhaa zilizopita na kujitwaliwa shughuli zote za kiuchumi katika eneo hilo.
Mbali na hilo, M23 ililiteka eneo la Rutshuru tangu mwaka 2022 linalojumuisha Mji wa Bunagana ulioko mpakani mwa Rwanda na DRC.
Mafanikio haya ya kimaeneo yameimarisha msimamo wa M23 huku yakivuruga uthibiti wa kikanda na kuutikisha utawala wa Rais Felix Tshisekedi.
Rais Tshisekedi amewataka raia kukataa matamko ya mgawanyiko, lakini wanasiasa na vyombo vya habari vinaendelea kusisitiza hisia hizi zipo bado, na kudhoofisha juhudi za amani za msingi.
Mashirika ya kikanda na kimataifa yamejaribu kupatanisha mzozo huo, ikiwamo Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyoandaa mazungumzo ya amani, ingawa M23 ilitengwa kwa vile inachukuliwa kuwa kundi la kigaidi na Serikali ya Congo.
Wakati huohuo, Umoja wa Mataifa na wahusika wengine wa kimataifa wametoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mapigano na mazungumzo ya kikanda ili kushughulikia mzozo huo.
Kuibuka upya kwa M23 kunaashiria changamoto zilizokita mizizi mashariki mwa DRC, ikiwa ni pamoja na utawala dhaifu, migawanyiko ya kikabila na ushindani wa masilahi ya kikanda.
Operesheni za kijeshi pekee zimeshindwa kuleta amani ya kudumu. Wataalamu wanahoji kuwa suluhu ya muda mrefu inahitajika kushughulikia malalamiko ya ndani, kuimarisha taasisi za Serikali, na kuendeleza mazungumzo kati ya DRC na majirani zake.
Majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini yanakadiriwa kuwa wakazi milioni 4.6 wameyakimbia makazi yao kukwepa vita hiyo huku ikitajwa kuathiri maeneo yenye wakazi zaidi ya milioni sita.
Mwaka 2025, pekee, raia zaidi ya 400,000 waliyakimbia makazi yao kukepwa mapigano kati ya M23 dhidi ya FARDC na vikosi vya walinda amani vya Monusco.
Wakati hali inavyoendelea, raia wa DRC wakiwamo wanawake na watoto ndiyo wanaoteseka kwa kukimbia mashambulizi ya risasi na mabomu na kuhamishia makazi kwenye kambi za wakimbizi na mataifa jirani.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.