‘Sekta binafsi ipewe nafasi kuzalisha umeme’

Dar es Salaam. Wakati kukosekana kwa miundombinu ya usambazaji umeme ikitajwa kuwa sababu ya maeneo mengi Afrika kukosa nishati ya uhakika, wadau wameshauri sekta binafsi iandaliwe mazingira ili iweze kuwekeza katika miradi mikubwa ya uzalishaji nishati.

Pia, nchi zimeshauriwa kuangalia namna ya kutumia mifuko ya pensheni na hifadhi ya jamii kwa ajili ya uendeshaji wa miradi ya nishati pamoja na kuvutia uwekezaji kwa kampuni za kusambaza umeme pekee.

Haya wamesema wakati wakitoa maoni yao katika mdahalo wa kuangazia changamoto zinazoikabili sekta ya nishati katika Bara la Afrika na kuangazia njia gani zinaweza kutumika ili kuhakikisha kunakuwapo na nishati ya uhakika.

Mdahalo huo ni miongoni mwa sehemu ya kile kilichofanyika katika siku ya pili ya mkutano wa Nishati Afrika ulioanza jana Januari 27 na unafikia tamati leo Januari 28, 2025.

Akizungumza katika mdahalo huo, Shirika la Kimataifa la Fedha la Benki ya Dunia (IFC), Makhtar Diop amesema umefika wakati sasa kwa nchi za Afrika kuacha kuona umeme kama sekta ya kimkakati inayopaswa kuzalishwa na Serikali badala yake ialike sekta binafsi.

“Tunapaswa kuhusisha sekta binafsi katika utafutaji fedha kwa ajili ya usambazaji umeme na uzalishaji, tubadili mifumo iliyozoeleka na kuruhusu vyanzo mbalimbali vya fedha kama mifuko ya pensheni na mifuko ya hifadhi ya jamii kugharamia miradi ya usambazaji wa umeme,” amesema.

Katika hili amesema mbali na kuita sekta binafsi kwa ajili ya kuwekeza katika uzalishaji wa umeme, ni muda wa kuangalia namna gani umeme huo utafika kwa wananchi kwa kuwa kampuni nyingi hazina uwezo wa kusimamia usambazaji umeme.

“Kwa Afrika wengi wanawekeza katika uzalishaji, lakini hakuna ufungamanishaji mzuri kati ya kuzalisha na kusambaza hivyo tunahitaji kuwa na kampuni zitakazojiwekeza katika kusambaza umeme peke yake,” amesema.

Hilo litawezekana ikiwa mitazamo ya nchi itabadilishwa na kufungua milango ya kutafuta mitaji na kuanzisha kampuni za kusambaza umeme kwa wananchi kwa kuruhusu uwekezaji wa umeme ndani ya nchi.

Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa TotalEnergies, Patrick Pouyanné amesema ni wakati sasa kwa nchi za Afrika kuanza kuwekeza katika mifumo ya kusambaza nishati kwa kuwa zinapokuwa na mikakati ya kuzalisha nishati jadidifu ni lazima umeme huo kuunganishwa katika gridi.

“Leo hii ukisema uwe na kampuni inayosafirisha na kufanya ugavi si rahisi kwa sababu ni mtaji mkubwa unahitaji ili kukamilisha hilo,” amesema.

Amesema kukosekana kwa mifumo imara ya usambazaji umeme, inaweka ugumu katika kuvutia uwekezaji wa kimataifa na binafsi katika uzalishaji.

“Mfumo wa usambazaji umeme ni miundombinu na lazima iweze kusimamiwa kwa namna ya kuvutia uwekezaji wa umeme mkubwa zaidi, lakini nina hofu kubwa sana.  Pia, ni vizuri kuwa mradi ambao benki wanaweza kuufadhili, kama unataka kuanzisha mfumo wa mradi jadidifu ni lazima uweze uende kwenye benki za biashara,” amesema Pouyanné.

Kwa upande wake, Hussain Al Nowais ambaye ni Mwenyekiti wa AlNowais Investment and AMEA Power alizishauri nchi kuwa na vituo jumuishi kwa ajili ya wawekezaji ambavyo vitakuwa vikiwarahisishia upataji wa huduma na vibali vyote pamoja na huduma zote zinazohusu mashirika ya serikali.

“Tuwe na kituo kimoja jumuishi ili tusipoteze muda, nikifika hapo nashughulikia changamoto zote. Togo ni nchi ndogo lakini wamefanya vizuri sana unaenda katika kituo kimoja jumuishi changamoto zako zote zinashughulikiwa unaenda mbele,” amesema.

Amesema hali hiyo iliwafanya hata wao ndani ya miezi 12 wakiwa ndani ya Togo kutoka hatua A hadi Z kwa sababu mifumo iliwaruhusu kufanya hivyo jambo linalorahisisha maisha kwa upande wao.

Related Posts