Dar es Salaam. Jumla ya Sh115.15 trilioni zimeahidiwa na wadau mbalimbali ikiwamo Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) na Benki ya Dunia (WB) kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa ajenda 300 ambayo ni lengo kuu la mkutano wa kimataifa wa nishati Afrika.
Fedha hizo zinalenga kuanza kuchochea ufikishaji wa umeme kwa Waafrika milioni 300 hadi kufikia mwaka 2030.
Hayo yamesemwa na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dk Akinumwi Adesina wakati akitoa taarifa ya benki hiyo kwa wakuu wa nchi waliohudhuria siku ya pili ya mkutano wa nishati unaofanyika jijini Dar es Salaam.
Dk Adesina amesema upatikanaji wa umeme ni jambo la muhimu katika ukuaji wa uchumi Afrika huku akisema kukosekana kwake kunapunguza ukuaji wa uchumi wa Afrika kwa asilimia 2.4.
Kutokana na hilo, Benki ya AfDB ilizindua mpango wa kuboresha upatikanaji wa nishati mwaka 2016 kwa kushirikiana na WB ambao wameonyesha mafanikio kwa kuongeza upatikanaji wa umeme kutoka asilimia 39 mwaka 2015 hadi asilimia 52 mwaka 2024.
Pamoja na mafanikio yaliyopatikana amesema bado watu milioni 571 Afrika hawana umeme ambao ni sawa asilimia 83 ya watu wasiokuwa na umeme duniani huku zaidi ya watu bilioni moja wakiwa hawana uwezo wa kufikia nishati safi ya kupikia jambo linaloathiri afya ya kinamama, watoto na maisha ya watu kwa jumla.
“Hivyo, lazima tuchukue hatua za haraka ili kupunguza idadi hii na ndiyo maana Rais wa Benki ya Dunia na mimi tumeungana pamoja kuzindua Mission 300 ili kusaidia watu milioni 300 kupata umeme mwaka 2030,” amesema Dk Adesina.
Katika kufanikisha lengo hilo, AfDB na WB kwa pamoja zitachangia Sh102 trilioni kaika utekelezaji wa ajenda hiyo na Sh46.41 trilioni zitatolea na AfDB na WB ikitoa Sh56.1 trilioni.
Hata hivyo, ajenda hii imetajwa kugusa wadau mbalimbali duniani jambo ambalo limewafanya kuunga mkono na kutoa ahadi zao katika siku ya kwanza ya mkutano huu (Januari 27, 2025).
Katika siku hiyo ya kwanza Benki ya Maendeleo Kiislamu iliahidi Dola 2.65 bilioni za Marekani (Sh6.68 trilioni), Rais wa Benki ya Maendeleo ya Miundombinu Asia ameahidi Dola 1.5 bilioni za Marekani (Sh3.82 trilioni), Rais wa OPEC aliahidi Dola 1 bilioni za Marekani(Sh2.5 trilioni).
“Tuna imani kwamba washirika wengine wa maendeleo hapa na kwingineko watajiunga na sisi na kutangaza ahadi zao husika leo na baadaye. Pamoja, tutumie Mission 300 (ajenda) kwa ufanisi ili kuwapatia watu milioni 300 Afrika umeme katika nchi zenu zote ifikapo mwaka 2030,” amesema.
Hata hivyo, amesema ni ngumu kutimiza malengo hayo bila kushirikiana na sekta binafsi ndiyo maana waliwakaribisha ili kuhakikisha wanaboresha upatikanaji wa nishati jadidifu kwa kuimarisha uwazi katika vibali na leseni, kupunguza gharama za umeme ili kusaidia gharama za uzalishaji viwandani.
“Lengo ni kupanua mifumo ya gridi ndogo na mifumo isiyo ya gridi ili kuwafikia mamilioni ya watu ambao hawana umeme wa gridi katika maeneo ya vijijini.
“AfDB itawasaidia wakuu wa nchi na Serikali kuchukua hatua za pamoja kwa ajili ya kuwa na mikataba na mipango ya pamoja ya uzalishaji nishati ili kutekeleza na kutimiza maono yenu,” amesema.