Hivi karibuni nimeona pendekezo la mtalaa ulio na mabadiliko makubwa katika elimu.
Mabadiliko makubwa niliyoona ni haya: kwanza kuingiza humo elimu ya ufundi kuanzia madarasa ya chini, pili, kupunguza masomo ili mwanafunzi asiwe na kazi kubwa mno ya kukariri, tatu, kuwa na somo la historia ya Tanzania na maadili.
Hoja yangu leo ni kuhusu somo hilo la historia ya Tanzania na maadili, ambalo litafundishwa kuanzia elimu ya msingi hadi chuo kikuu.
Hili ni pendekezo zuri sana.Kufundishwa kwa somo hili ni uamuzi mzuri ambao nimekuwa nikiandika juu ya umuhimu wake mara nyingi katika gazeti hili.
Napendekeza na nashauri kwamba somo la maadili lisimame peke yake, yaani lisiwe sehemu ya somo lingine kama historia ya Tanzania.
Kwanza kabisa, sioni kwamba kuna uhusiano wa msingi kati ya historia ya Tanzania na maadili. Kwa nini tuunganishe haya masomo mawili?
Naamini kwa dhati kwamba somo la maadili ni la msingi sana katika elimu yoyote ile au malezi yoyote yale.
Kulichanganya somo hili na historia ya Tanzania au na somo lingine lolote lile, ni kutozingatia uzito wa somo la maadili; ni kusahau kwamba somo la maadili ndilo somo mama.
Uzoefu wangu hapa nchini na nje ya nchi, ni kwamba somo hili ni lazima lisimame lenyewe, kwanza kwa sababu ni somo mama.
Pili kwa sababu mtalaa wake ni mpana na mzito, hivyo kwamba hatutalitendea haki somo hili kwa kulifundisha kama sehemu ya somo lingine.
Kwa miaka karibu 50 nimefundisho somo hili hapa Tanzania, Kenya, Marekani na Finland, na hata sasa nafundisha somo hili mtandaoni (online teaching and learning) katika chuo kikuu kimoja kilichopo Chicago, Marekani
Nimefundisha somo hili kwa miaka mitatu Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia na wanafunzi wangu wa ngazi ya uzamili na uzamivu walielewa vizuri na ndio maana nasisitiza somo hili halina budi kusimama lenyewe.
Katika gazeti hili nimeandika makala nyingi nikipendekeza mitalaa ya somo la maadili kuanzia chekechea hadi chuo kikuu.
Itakuwa vizuri sote tukafanya rejea katika makala hizo, na hapo baadaye natumaini kuzitumia katika kubuni mtalaa, ambao sasa hivi utahitajika hapa nchini katika ufundishaji na ujifunzaji wa somo hili.
Nimekwishapendekeza pia katika gazeti hili kwamba somo la maadili linapaswa kufundishwa bila kuegemea sana dini hii au ile. Hii haina maana kwamba busara za dini mbalimbali hazitatumika katika somo hili.
La hasha! Maandiko matakatifu ya dini zote yanatuasa tuwapende na kuwaheshimu binadamu wenzetu. Kila dini inafundisha hili.
Ni lazima lifundishwe katika somo la maadili, Lakini hoja yangu hapa ni kwamba mwalimu wa somo hili, anapaswa kuwa na uwezo wa kufundisha kuhusu heshima na upendo kwa jirani kwa wanafunzi darasani mwake, ambao ni mchanganyiko wa dini mbalimbali.
Hapa ndipo tunahitaji mwalimu ambaye ana uwezo wa kufundisha jambo hili kwa wanafunzi hao bila hata yeye mwenyewe kutambulisha dini yake.
Wakati fulani nilifundisha somo hili kwa wanafunzi wa kidato cha nne na ungewauliza dini ya huyu mwalimu ni ipi, hawangeweza kusema ni hii au ni ile. Hii ni kwa sababu nilifundisha maadili ya msingi yanayopatikana katika kila dini.
Wakati fulani nilifundisha somo hili kwa wanafunzi wa kidato cha nne na ungewauliza dini ya huyu mwalimu ni ipi, hawangeweza kusema ni hii au ni ile. Hii ni kwa sababu nilifundisha maadili ya
Kila dini inafundisha tuheshimu na tulinde uhai wa watu wengine na mali zao. Kila dini inafundisha umuhimu wa kuwasaidia walio na shida.
Kila dini inafundisha kwamba Mungu Mwenyezi ndiye Muumba wa ulimwengu na kila kitu kilichomo.
Kila dini inafundisha kwamba kila kitu kinapita, na hivyo binadamu utumie muda wako vizuri hapa duniani.
Hivyo inawezekana kabisa kufundisha somo hili bila kuegemea dini yoyote, lakini mwalimu afanye rejea akilini mwake katika misingi ya dini.
Misingi ya dini zote inafanana kama tulivyoona hapo juu. Wabobezi wa dini na wa somo la maadili watakuambia kwamba kuna dini ndani ya dini.
Yaani misingi ya dini inafanana lakini mambo mengine kama ibada yanatofautiana.
Kwa mfano, kiongozi wa dini anavaa mavazi gani wakati wa ibada si jambo la msingi la dini. Viongozi wa dini mbalimbali wanavaa mavazi tofauti katika ibada zao.
Kama wanaoabudu wanaelekea kusini au kaskazini katika ibada yao si jambo la msingi la dini.
Kama wanaoabudu wanachukua saa moja na wengine siku nzima si jambo la msingi katika dini. Baadhi ya mambo ya msingi katika dini yameainishwa hapo juu.
Mwalimu wa somo la maadili aliye makini atatumia misingi hiyo ya dini kufundisha somo hilo.
Ndio maana nikasema inawezekana mwanafunzi asijue dini ya mwalimu huyo kwa sababu mwalimu huyo anajikita tu katika busara lukuki zilizo katika dini zote. Ni mwalimu wa aina hii anatakiwa kufundisha somo la maadili.
Mwanafalsafa wa Kigiriki, Plato (428-348 B.C.), anasema: ‘’Kila jambo, kila kitu, kila kinachosemwa au kunachofundishwa kina uhusiano na maadili. ‘’
Ni hoja hii inayoniongoza niseme kwamba masomo yote darasani ni lazima yahusishwe kwa namna fulani na maadili.
Somo la lugha lina vipengele vingi na hadithi nyingi zinazohusu maadili. Somo la mazingira halitakamilika kama maadili si sehemu yake.
Ukifundisha historia utakutana na watu waadilifu waliogusa jamii zao kama kina Mwalimu Nyerere, Nelson Mandela na wengineo.
Huwezi kujijfunza historia ya Mwalimu Nyerere bila kuguswa na uadilifu wake. Huwezi kujifunza historia ya Adolf Hitler bila kuona ukatili wake.
Ni kwa sababu hizo hapo juu nathubutu kusema kwamba somo lolote lile linalofundishwa darasani, halitakamilika kama halitahusishwa na maadili.
Ni katika kuzingatia ukweli huu tunaona kwamba Plato yuko sahihi kusema kwamba kila jambo lina uhusiano na maadili. Hivyo walimu wote, wa masomo yote, ni lazima wahusishe somo lao na maadili.
Nihitimishe kwa kusema kwamba yote yaliyosemwa hapo juu yanadhihirisha kwamba somo la maadili ni pana na halina budi kupewa hadhi na heshima linalostahili kwa kusimama lenyewe kama somo.
Kulifanya lifundishwe pamoja na somo lingine kama historia, ni kukosa kuelewa uzito na umuhimu wa somo hili katika kujenga Taifa adilifu na makini.