Chunya. Mkuu wa Wilaya ya Chunya Mkoa wa Mbeya, Mbarak Batenga amesema timu ya wataalamu kutoka Mfuko wa Fursa ya Maendeleo kwa Wote ( UCSAF), imewasili kwa ajili ya kufanya utafiti wa kina kubaini sababu za kata 17 kati ya 20 kukosa mawasiliano.
Timu hiyo iliwasili Januari 27, 2025 ikiwa ni siku kadhaa baada ya Naibu Waziri wa Mawasiliano Teknolojia ya Habari, Mhandisi Maryprisca Mahundi kufanya ziara ya kukagua Kituo cha Mkongo wa Taifa kilichojengwa katika Kata ya Makongorosi wilayani humo.
Batenga ametoa kauli hiyo leo Januari 28, 2025 kwenye Kikao cha Baraza la Madiwani kilicholenga kutoa taarifa ya fedha kwa mwaka 2024/25 na kupitia rasimu ya mapendekezo ya bajeti ya Sh9 bilioni za miradi ya maendeleo kwa mwaka 2025/26.
Amesema kumekuwepo na changamoto kubwa ya mawasiliano katika vijiji vya pembezoni vilivyopo katika kata 17 wilayani humo hali inayosababisha wananchi kutembea umbali mrefu kupata mawasiliano.
“Changamoto hiyo si kwa wananchi pekee bali hata katika utendaji wa makusanyo ya mapato ya Serikali kwa kutumia mifumo ya mashine za POS hali inayosababisha upotevu wa mapato kwa baadhi ya watu wasio waaminifu kukusanyia mifukoni,”amesema.
Batenga amesema ujio wa wataalamu hao, utaleta suluhisho kwa wananchi na kudhibiti makusanyo ya fedha za Serikali kwa kutumia mashine za teknolojia za kisasa kwa visingizio vya kukosekana kwa mtandao katika baadhi ya maeneo.
“Serikali imekuja na mpango mzuri wa matumizi ya mashine za POS na tayari kila kata zinatumika kukusanya fedha za vyanzo mbalimbali, lakini kuna baadhi ya maeneo mifumo ya makusanyo haisomi kwa kukosa mawasiliano,” amesema Batenga.
Katika hatua nyingine Batenge amewataka madiwani kuendelea kusaka vyanzo vipya vya mapato sambamba na kujiandaa katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.
“Niwapongeza kwa namna mlivyoshiriki vizuri katika uchaguzi mdogo wa Serikali za mitaa, kimsingi kwa Mkoa wa Mbeya tulifanya vizuri, natarajia katika uchaguzi mkuu wa 2025 sura hizi zirejee ili kuendeleza hapo mlipoishia,”amesema.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Bosco Mwanginde amesema kwa mwaka 2025/26 wanatarajia kuongeza mapato ya ndani kutoka Sh8.7 bilioni mpaka Sh9 bilioni na kuelekeza kwenye miradi ya kimkakati.
Amesema baraza la madiwani limepitisha rasimu ya matumizi ya Sh38.7 bilioni ya mapato ya ndani kwa mwaka wa fedha 2025/26.
Mwanginde amesema kupitia bajeti hiyo, madiwani wakawe chachu ya kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuondoa ukakasi unaoweza kujitokeza hususani katika uanzishwaji holela wa shule shikizi bila kufuata utaratibu.
Ofisa Mipango Miji na Uratibu Wilaya ya Chunya, Janeth Mwaigoga amesema kupitia mapato ya halmashauri Sh6.6 milioni zilitumika kununua taulo za kike zilizotolewa kwa wanafunzi 3,300 wa shule za msingi na sekondari.
Diwani wa Lupa, Daniel Mwafyela amesema bajeti iliyopitishwa itagusa miradi mbalimbali ya kimkakati kwa lengo la kusogeza huduma kwa wananchi.