Kinshasa. Baadhi ya wananchi wameandamana jijini Kinshasa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na kuchoma moto balozi za mataifa ya Ufaransa, Ubelgiji na Rwanda.
Balozi nyingine zilizolengwa na waandamanaji hao leo Jumanne Januari 28, 2025, ni ya Uganda na Kenya.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Noel Barrot ameandika kwenye akaunti yake ya X kuwa ubalozi wa Ufaransa uliopo jijini Kinshasa umeshambuliwa kwa kuchomwa moto, huku akidokeza kuwa moto huo umeshadhibitiwa.
“Yote haya yanasababishwa na Rwanda. Kitu ambacho Rwanda inakifanya kinaigharimu Ufaransa, Marekani na mataifa mengine. Watu wa DRC wamechoka. Hivi tutasubiria kufa hadi lini,” mmoja wa waandamanaji amelieleza Shirika la Habari la Reuters.
Waandamanaji wamesambaa katika mitaa mbalimbali jijini humo wakipambana na polisi, huku wengine wakichoma matairi barabarani.
Akizungumza kupitia televisheni ya taifa hilo, Waziri wa Mawasiliano wa DRC, Patrick Muyaya amewataka waandamanaji kuachana na uamuzi wao wa kushambulia balozi hizo.
Pia, amesema maandamano hayo tayari yamedhibitiwa kwa baadhi ya maeneo ya jiji hilo.
“Tuna kila haki ya kuonyesha hasira zetu ila naomba basi tueleze hisia zetu kwa njia ya amani. Naomba tusishambulie miundombinu ya balozi za wenzetu,” amesema Muyaya.
Maandamano hayo yanatajwa kuchangiwa na mapigano mazito yanayoendelea kati ya kundi la M23 na vikosi vya Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ambayo yamesababisha vifo vya watu 25 huku 375 wakijeruhiwa katika Mji wa Goma.
Reuters imeripoti kuwa, watu hao walifariki dunia na wengine kujeruhiwa kwenye mapigano yaliyotokea kuanzia jana Jumatatu hadi leo Jumanne Januari 28, 2025 huku hospitali zilizopo Mji wa Goma zikitajwa kuelemewa na majeruhi wa mapigano hayo.
M23 kuutwaa Mji wa Goma ni pigo kwa Serikali ya Rais Felix Tshisekedi kufuatia mapigano yaliyodumu kwa miezi kadhaa kati ya M23 na askari wa Jeshi la nchi hiyo FARDC, huku Mji wa Goma ukiwa kitovu cha biashara katika miji iliyopo mashariki mwa DRC.
Waziri wa Maendeleo ya Vijijini wa DRC, Muhindo Nzangi amethibitisha leo kuwa waasi hao wameshauteka Mji wa Goma kwa asilimia zaidi ya 80, huku akidai kuwa vikosi vya Jeshi la Rwanda vimeweka kambi katika maeneo mengine ya mji huo.
“Hadi sasa kuna mamia ya watu waliojeruhiwa eneo la Goma, wengi wao wamelazwa wakiuguza majeraha ya risasi walizopigwa na waasi hao,” amesema Adelheid Marschang, ambaye ni Mratibu wa Shughuli za Dharura wa kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) DRC.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.