Dar es Salaam. Wakuu wa nchi 21 kutoka mataifa ya Afrika wamekutana jijini Dar es Salaam leo Januari 28, 2025 kuhitimisha Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu nishati.
Idadi hiyo ya wakuu wa nchi waliohudhuria mkutano huo ni kati ya wale 25 waliothibitisha kushiriki na wengine wamewakilishwa na viongozi wengine wa juu wa Serikali zao.
Marais hao 21 waliohudhuria wanawakilisha mataifa ya Tanzania, Lesotho, Djibouti, Jamhuri ya Congo Brazzaville, Visiwa vya Comoro, Madagascar, Somalia, Sierra Liane na Mauritania.
Wengine ni kutoka Burundi, Guinea Bissau, Malawi, Libya, Zambia, Kenya, Nigeria, Gabon, Liberia, Ethiopia, Botswana na Ghana.
Wakuu hao wa mataifa 21, watakuwa na jukumu la kuazimia kile kilichojadiliwa na mawaziri wa kisekta katika mkutano huo jana, kadhalika watatakiwa kuahidi mabadiliko ya sera na sheria kurahisisha uwekezaji wa sekta binafsi katika nishati.
Sambamba na hayo, watashuhudia utiaji saini wa mkataba wa utekelezaji wa Ajenda300 inayolenga kuhakikisha mwaka 2030, Waafrika milioni 300 watafikiwa na huduma ya umeme.
Mkutano wa wakuu hao wa nchi, ndio unaotazamwa kutoka na kauli moja kuhusu mustakabali wa upatikanaji wa nishati ya umeme kwa wakazi wa Afrika ambao milioni 600 wapo gizani.
Chimbuko la mkutano huo ni maazimio ya Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB), zilizokubaliana kuhakikisha mataifa ya Afrika yanaondokana na giza.
Hata hivyo, hatua ya kuanza na nchi 14 ni mwanzo tu, lakini kadri siku zinavyokwenda idadi ya nchi zinatarajiwa kuongezwa, hadi umaskini wa nishati utakapokoma barani humo.
Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania ndiye mwenyeji wa mkutano huo, ambaye katika Taifa lake angalau uzalishaji wa umeme unazidi mahitaji ya wananchi.
Tanzania inazalisha zaidi ya Megawati 3,000 za nishati hiyo, huku mahitaji ni 1,800 ingawa ni asilimia 78 tu ya wananchi ndiyo wanaopata huduma hiyo kwa sasa.
Juhudi zinazohitajika ni kutengeneza uwiano kati ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme nchini na Afrika, hilo ndilo linalojadiliwa na wakuu hao wa nchi na watatoka na kauli moja.
Mkutano wa nishati barani Afrika umevunja rekodi ya kuwa tukio lililohudhuriwa na marais wengi zaidi kwa wakati mmoja.
Tukio la kihistoria lililowahi kushuhudiwa awali lilikuwa mazishi ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, mwaka 1999, yaliyohudhuriwa na wakuu wa nchi 19.
Pia, tukio la pili lilikuwa Mkutano wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wa mwaka 2019 ulioshirikisha wakuu wa nchi 15, lakini safari hii idadi imepanda maradufu.