Wakali wa namba kikapu Dar

SUPASTAA wa Christ The King, Davidson Evarist anawaburuza wenzake katika utupiaji nyavuni kwenye mashindano ya Ligi Daraja la Kwanza Mkoa wa Dar es Salaam yanayoendelea kwenye viwanja vya Bandari, Kurasini.

Davidson amegeuka kuwa tishio kutokana na namna anavyokabiliana na timu pinzani na pia wepesi wake katika kuzamisha mipira nyavuni hadi sasa akiwa amejikusanyia pointi 406.

Nafasi ya uongozi wa Davidson inatokana na michezo 17 aliyocheza akifuatiwa na Fahmi Hamad wa Polisi mwenye 287. Wengine na alama walizokusanya ni George Mwakyanjala (Yellow Jacket) 248, Lawi Mwambasi (Polisi) 248, Martin Rodgers (Mlimani BC) 244, Ally Songoro (Magone) 233, Adam Ramadhan (Mbezi Beach) 214 na Dickson Thomas (Kigamboni Heroes).

Upande wa mitupo ya pointi tatu maarufu kama three points kuna Omary Njota wa Yellow Jacket anayeongoza kwa kutupia pointi 41 akifuatiwa na Jacob Marenga aliyefunga 35 huku wengine ni George Mwakyanjala  (Yellow Jacket) 30, Dominic Zacharia (Kurasini Heat) 29 na Daud Daud (Kurasini Heat) 29.

Wachezaji wengine ni Dickson Thomas (Kigamboni Heroes) 28, Calvin Mushi (Premier Academy) 26, Bright (PTW) 23, Abbas Omary (Stein Warriors) 23 na Kelvin Mbogo (Dar King) 23.

Pia katika kinyang’anyiro cha namba kuna mastaa waliozuia vizuri katika mechi mbalimbali wakiongozwa na Hillary Felix wa Kurasini Heat aliyezuia mipira  mara 31 akifuatiwa na Mwinyipembe Jumbe wa Stein Warriors 29, John Magembe (Premier Academy) 16 na Baraka Kweka (Mlimani B.C) 16.

Wengine ni Anold (Mbenzi Beach) 15, Isihaka Kienda (PTW) 14, Lawrence James (Dar King) 13, Luis Nyoni (Stein Warriors) 12, Francis Mallya (Mgulani Warriors) 12 na Franko Frank (Premier Academy) 10.

Wakati wakali wa namba wakiendeleza ligi yao, timu ya Polisi iliinyuka Kurasini Heat kwa pointi 79-43.

Kwa matokeo hayo Polisi inaongoza msimamo wa mashindano hayo ikiwa na pointi 34 kutokana na matokeo ya ushindi wa michezo 17.

Katika mchezo huo Polisi iliongoza katika robo zote nne kwa pointi 18-13, 15-7, 19-14 na 27-9, huku nyota wake Noel Mwazembe akiongoza kwa kufunga pointi 26 akifuatiwa na Fahmi Hamad aliyefunga 25.

Kwa upande wa Kurasini Heat alikuwa ni Daud Daud aliyefunga pointi 18 akifuatiwa na Anset Maliselo  aliyefunga pointi 10. Wakati huohuo timu tatu  zinagombea nafasi mbili kucheza robo fainali baada ya kulingana pointi.

Timu hizo ni Yellow Jacket yenye pointi 27, Kibada Heroes 27 na Kibada Riders 27.

Kamishna wa Ufundi na Mashindano wa Shirikisho la Kikapu Dar es Salaam (BD), Haleluya Kavalambi alisema timu mbili zitapatikana kwa kuangalia pointi za kufunga na kufungwa.

Timu mbili zitakazopatikana zitaungana na sita  zilizotiga robo fainali ambazo ni Polisi yenye pointi 34, Stein Warriors (30), Chang’ombe Boys (29), Kurasini Heat (29), Mlimani B.C (28) na Mbezi Beach (27).

SABABU MBILI ZAIVURUGA KING

Kufanya vibaya kwa Dar King katika ligi hiyo kumemuibua nahodha wa timu hiyo, Isaya Lunyungu akitaja sababu zilizochangia ishindwe kutinga robo fainali.   

Lunyungu anayecheza namba moja maarufu kama point guard alisema sababu ya kwanza ni baadhi ya wachezaji  kuchelewa kufika uwanjani kwa wakati.

Alisema wachezaji wengi nyota wa timu hiyo hutokea kazini jambo lililofanya wawe wanafika mchezo ukiwa unaendelea, hivyo kukosa muda mzuri wa maandalizi ya mechi.

“Kwa kweli ilitufanya tupambane hivyo hivyo na wachezaji waliochelewa walipata nafasi ya kucheza katika robo ya pili (ya mechi),” alisema Lunyungu na kwamba ndiyo maana katika michezo miwili walipoteza dhidi ya Kurasini Heat kwa pointi 60-49 na Kibada Riders 78-62.

Alisema sababu nyingine ilitokana na baadhi ya wachezaji kukabiliwa na mitihani chuoni, jambo lililochangia wafungwe na Stein Warriors kwa pointi 118-41.

Katika mchezo huo Stein Warriors iliongoza katika robo zote nne kwa pointi 28-10, 22-9, 31-12 na 37-10.

Kwa upande wa ufungaji Nassir Missaji wa Stein Warriors alifunga pointi 25 akifuatiwa na Luis Nyoni 20, huku ule wa Dar King ulibebwa na Edward Bugai aliyefunga pointi 10 sawa na Lunyungu.

Mzunguko wa mwisho wa ligi hiyo ukimalizika, timu ya  Magnet iliifumua Donbosco VTC kwa pointi 58-52 ukiwa ni ushindi wake wa pili kati ya michezo 17 iliyocheza.

Kwa ushindi huo Magnet imeshika 16 katika ligi hiyo ikiwa na pointi 18. Katika mchezo huo Donbosco VTC iliongoza robo ya kwanza kwa pointi 10-8, 14-14 hadi kufikia mapumziko ilikuwa mbele kwa pointi 24-22.

Robo ya tatu Magnet iliongoza kwa pointi 18-12 na ile ya nne ikishinda 18-16.

Katika mchezo huo Denis Jomalema wa Magnet aliongoza kwa kufunga pointi 31 kati ya pointi hizo alifunga  eneo la three pointi tisa, akifuatiwa na Brian Mwale aliyefunga pointi 12 ilhali upande Donbosco VTC alikuwa Junior Ngowo aliyefunga pointi 17 akifuatiwa na Kibwana Johnson pointi 14.

Related Posts