Shinyanga. Wakazi 26,000 wa vijiji vinane vya kata za Masengwa, Samuye na Mwamala Halmashauri ya Shinyanga wanakutana na changamoto ya upatikanaji wa majisafi na salama.
Wakizungumza na gazeti hili leo Januari 28, 2025 baadhi ya wakazi wa vijiji vya Ibanda na Mwamala wamesema changamoto ya maji ni kubwa kutokana na kutumia maji ya chumvi.
Marco Daudi, mkazi wa Kijiji cha Ibanda amesema kilio chao kikubwa ni kupata majisafi na salama kutokana na kutumia maji ya visima vya wazi ambavyo usalama wake ni mdogo kutokana na kuchangia na wanyama.
Ameiomba Serikali kuwaondolea adha hiyo kwa kuhakikisha mradi wa maji ya Ziwa Victoria ambao umeanza kutekelezwa unakamilika haraka ili kuhakikisha tatizo la kukosekana huduma ya majisafi na salama linapatiwa ufumbuzi.
“Mambo mengi mazuri yamefanyika katika kijiji chetu lakini tatizo kubwa tulilonalo ni maji, tunaiomba sana Serikali itusaidie na sisi tupate maji ya bomba,”amesema Daudi.
Hata hivyo, changamoto hiyo inatarajia kukoma baada ya mradi mkubwa wa maji kuanza kutekelezwa katika maeneo hayo.
Diwani wa Mwamala, Hamis Masanja amesema vijiji vya Ibanda na Mwamala viko mbioni kupata maji kwa kuwa, tayari wameshaanza kuchimba mitaro na kulaza mabomba.
Amesema vituo vya kuchotea maji, tayari vimeshajengwa ili kuhakikisha tatizo la maji linakwisha na kuwawezesha wananchi kupata huduma karibu na kuacha kutumia maji yenye chumvi.
Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) Wilaya ya Shinyanga, Emael Nkopi amesema mradi huo unatekelezwa katika vijiji vinane na mkandarasi Mbeso Construction, ukikamilika utamaliza tatizo hilo.
Amesema mradi huo unatekelezwa kwa fedha za Serikali na unatarajiwa kugharimu Sh4.75 bilioni.
Mradi huo ulianza kutekelezwa Aprili 2022 na ulitarajia kukamilika Februari 2024 lakini kutokana na changamoto za fedha umechelewa kukamilika.