Wasichana 10,239 waliokatisha masomo warejeshwa tena shule

Morogoro. Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima Tanzania (TEWW) kupitia Mradi wa Kuongeza Ubora wa Elimu ya Sekondari (Sequip-AEP) imefanikiwa kuwarejesha shule wanafunzi wa kike 10,239 kutoka nchi nzima walikatisha masomo yao.

Taarifa hiyo imetolewa na naibu mkuu wa taasisi hiyo anayeshughulikia taaluma, utafiti na ushauri, Profesa Philipo Sanga alipozungumza kwenye warsha ya watendaji wa taasisi hiyo.

 Profesa Sanga amesema wasichana hao waliorejeshwa shule mbali na sababu ya kupata ujauzito, lakini zipo zilizowafanya awali wakatishe masomo ikiwamo ya umaskini uliokithiri, kupata magonjwa yaliyowafanya washindwe kwenda shule kwa muda mrefu pamoja na  utoro.

Amesema mradi huo umetazama changamoto hizo na kuhakikisha kuwa, hazikwamishi tena ndoto za wanafunzi hao wa kike.

“Wakati mradi huu unaanza mwaka 2022, taasisi yetu tuliweka malengo ya kupokea na kusajili wanafunzi wa kike waliokatisha masomo wapato 12,000 katika kipindi cha miaka mitano ya mradi lakini cha kutia moyo mpaka sasa tayari tumeshapokea na kusajili wanafunzi 10,800 na tayari wanaendelea na masomo yao,” amesema Profesa Sanga.

Hata hivyo, amesema  baada ya kuona mwamko mkubwa wa wanafunzi wa kike kujitokeza kujisajili, mwaka huu wa nne wa mradi, Serikali imeona umuhimu wa kiwarejesha shule watoto wa kiume ambao nao walikatisha masomo yao kwa sababu mbalimbali ikiwamo ya utoro.

Amesema kazi hiyo ya kuwarejesha wanafunzi imeanza na inaendelea vizuri na mpaka sasa wanafunzi wa kiume 888 tayari wameshasajiliwa huku lengo ni kusajili wanafunzi 1,000 nchini.

“Mikoa inayoongeza kuwa na wanafunzi waliokatisha masomo ni Lindi, Mtwara, Shinyanga, Dodoma, Ruvuma na Dar es Salaam, na hii inatokana na sababu nyingi ikiwamo ya mila na desturi.

“Yapo makabila hayampi fursa na kipaumbele mtoto wa kike kusoma, na kwa upande wa watoto wa kiume zipo sababu nyingine ikiwamo ya umaskini, mtoto wa kiume ndio anaonekana kuwa kiongozi wa,” amesema Profesa Sanga.

Awali, akitoa taarifa ya kazi ya usajili inavyoendelea mratibu wa kitaifa wa mradi wa Sequip wa TEWW,  Baraka Kionywaki amesema kazi hiyo inakwenda vizuri na bado wanaendelea kupokea wanafunzi wa kiume waliokatisha masomo.

Mratibu huyo amesema  kwa Mkoa wa Morogoro tayari wameshapokea na kusajili wanafunzi wa kiume waliokatisha masomo wapato 35, hivyo amewataka wanafunzi wengine wanataka kurudi shule kufika kwenye vituo vya taasisi ya elimu ya watu wazima na kujisajili.

“Usajili huu utaendelea hadi Machi na hakuna masharti yoyote zaidi ya kuwa Mtanzania, tuna walimu wa kutosha na wenye ujuzi na pia tunazo huduma zote zinazotakiwa katika ufundishaji na kujifunza,” amesema Kionywaki.

Awali, Mwenyekiti wa Baraza la Usimamizi la Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, Profesa Zacharia Mganilwa amesema katika mwaka wa fedha 2024/25 taasisi hiyo imepanga kutekeleza ukarabati na ujenzi wa miradi ya majengo katika Kampasi ya Dar es Salaam, Morogoro, Ruvuma na Kilimanjaro.

Pia, katika mwaka huo wa fedha kupitia mradi huo majengo ya utawala yatajengwa katika Mkoa wa Geita, Njombe, Singida na Simiyu.

Kupitia mradi huo, Profesa Mganilwa ameishukuru Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kuniamini taasisi hiyo na kuiwezesha kutekeleza mradi wa huo wa kuimarisha ubora wa elimu.

Related Posts