Wazambia kunogesha Makarasha | Mwanaspoti

WAKATI KenGold ikitarajia kufanya tamasha leo, Jumatano kutambulisha wachezaji na benchi la ufundi, kikosi hicho kinatarajia kucheza mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Real Nakonde ya Zambia.

Tamasha hilo lililopewa jina la Makarasha Day lenye kauli mbiu ya Saga Mwagia linalenga kutengeneza upya timu hiyo ikiwa ni ishara ya kujipanga na michezo ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara kwa lengo la kukinusuru kikosi hicho kutoka mkiani.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Habari na Mawasiliano wa KenGold, Joseph Mkoko alisema wanatarajia kucheza mchezo huo na Wazambia likiwa ni pendekezo la kocha mpya Vladislav Heric.

“Kesho (leo) kutakuwa na shughuli nyingi kwa ajili ya kunogesha tamasha letu. Burudani zitakuwepo na mashabiki watapata nafasi ya kuona kikosi chetu kipya kilichobeba matumaini mapya. Tunaamini mzunguko wa pili utakuwa bora zaidi kwetu,” alisema.

Hivi karibuni, Ofisa Mtendaji wa KenGold, Benson Mkocha alinukuliwa na gazeti hili akisema walikuwa na mialiko ya timu nyingi za nje ili kunogesha tamasha hilo.

Tamasha hilo litashuhudia mastaa wapya waliotamba Yanga na Simba wakiwemo Bernard Morrison, Obrey Chirwa, Kelvin Yondani na Zawadi Mauya.

Kipimo cha kwanza cha kocha huyo katika ligi  kitakuwa dhidi ya Yanga Februari 5 kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam akiwa na kazi ya kuipambania timu kutoka mkiani baada ya kukusanya pointi sita katika michezo 16.

Kocha huyo aliwahi kufundisha Club Africain (Tunisia), Chippa United, Maritzburg United, Ubuntu Cape Town, Bay United, Polokwane City na Cape Town zote za Afrika Kusini.

Related Posts