Dar es Salaam. Viongozi wa juu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wamesema wanakwenda kujifungia kwa wiki moja kupanga mikakati ya kushinikiza mabadiliko ya mifumo ya uchaguzi kabla ya kuushiriki.
Oktoba mwaka huu, Tanzania inatarajia kufanya uchaguzi wake mkuu wa kuwachagua, madiwani, wabunge na Rais.
Akizungumza leo Jumatano, Januari 29, 2025 baada ya kuripoti kwa mara ya kwanza kwenye ofisi za chama hicho, Mikocheni jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu amesema mpaka hapa walipofikia, Chadema sasa kinakwenda kuendesha siasa za kushurutisha mageuzi ya kisiasa.
Lissu aliyefika ofisi hapo kwa mara ya kwanza tangu alipochaguliwa wiki moja iliyopita, amesema chama hicho hakitafanya siasa za kawaida.
Viongozi wengine walioambatana naye ni pamoja na Makamu Mwenyekiti (Bara) John Heche na Makamu Mwenyekiti (Zanzibar), Said Mzee, Katibu Mkuu John Mnyika na Naibu Katibu Mkuu (Bara), Amani Golugwa.
“Mimi ninaamini na nina ushahidi wa kutosha wa chaguzi tatu zilizopita zinaunga mkono kauli ya ‘No reforms, No election’ (Hakuna Mabadiliko, Hakuna uchaguzi). Tukisema hivyo tunazungumzia njia za kushurutisha mageuzi, si njia ya kawaida kwenda kuwaomba walete mageuzi. ndivyo walivyofanya Kenya, Malawi na Zambia,” amesema Lissu alipoulizwa swali kuhusu kaulimbiu yao ya ‘No reforms, No election.’
Akijibu swali aliloulizwa na waandishi wa habari kama muda wa kufanya mabadiliko hayo unatosha? amesema, “Bunge linaweza kuitwa wakati wowote.”
“Hamjui historia ya nchi hii? Bunge liliwahi kukutana Jumamosi Aprili 25, 1964 wabunge wakaitwa walikokuwa wakaambiwa mkataba huu hapa, wakapitisha na Muungano,” amesema.
Lissu amesema kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano, Bunge linaweza kuitishwa wakati wowote.
Akieleza sababu ya kufanya siasa za shuruti, Lissu amesema katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Novemba 2019, asilimia 36 ya wagombea wa Chadema walienguliwa na hata uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 pia haukuwa wa haki.
“Kwa hiyo tukisema twende na wao wanajua na Mungu anajua tunakwenda kuumizwa…Tutakuwa sawa na makondoo yanayokwenda kuchinjwa.”
Huku akirejea maneno ya Makamu wa Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche, mwenyekiti huyo amesema katika utendaji wao hawatanyamaza hata wapelekwe gerezani.
“Utanyamaza ukiwa umekufa, ukiwa gerezani huwezi kunyamaza. Tukifanya harakati sawa sawa na tukifanya shuruti sawa sawa tutakwenda kuleta mageuzi kwenye uchaguzi,” amesema.
Akifafanua zaidi kuhusu kauli ya No reforms No Election, Lissu amesema hawamaanishi kwamba watasusia uchaguzi.
“Siyo kwamba tutasusia uchaguzi, siyo boycotting (gomea). Lazima tuzugumze hayo mambo mawili, tuone tutakwenda na yote kwa pamoja au moja,” amesema Lissu huku akisisitiza kuwa hilo litategemea uamuzi wa vikao.
“Tunakwenda kujifungia, haitakuwa ya mwenyekiti, tutakuwa na retreat (tafakuri), tutajifungia.
“Tutazungumza lugha anayoweza kuielewa Samia (Rais Samia Suluhu Hassan). Nani anataka uchaguzi kama wa mwaka uliopita au wa 2020?” amehoji.
Akizungumzia mwelekeo wa siasa za chama hicho, Makamu Mwenyekiti (Bara), Heche amesema kuna mambo mengi ya kufanya kuleta mabadiliko na kuiondoa CCM madarakani.
“Sisi tutaongoza wananchi kuwakumbusha na kuwaondoa madarakani,” amesema.
Akieleza mpango wa viongozi wa chama hicho kujifungia wiki nzima kupanga mikakati, Katibu Mkuu, John Mnyika amesema kuanzia kesho Januari 30 watakuwa na kikao cha wiki nzima kujipanga.
“Kwa hiyo kwa wiki nzima kuanzia kesho, tutajifungia viongozi wote wa juu, sekretarieti mpya na ya zamani, tutatoka na mwelekeo mpya tutaendesha chama chetu.
“Mwaka huu ni wa reforms (mabadiliko), Mwenyekiti atatuongoza. Reforms hizi ni kuongoza nguvu za pamoja, baada ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa, tulitafakati kwenye mkutano mkuu tukatoka na maazimio, yakapelekwa kamati kuu,” amesema.
Amesema moja ya maazimio ni kutaka kuwa na mabadiliko ya Katiba ya kuwa na mfumo mpya wa chaguzi ikiwemo kauli ya No reforms no election.
Amesema kutokana na kazi nzito iliyo mbele yao, hawatarajii kuona migawanyiko ndani ya chama.
“Katika wakati huu ambao tunatafuta Reforms za kikanuni na kikatiba, hatupaswi kuendeleza tofauti zetu za kiuchaguzi. Stronger together (nguvu kwa pamoja),” amesema.
Akizungumzia umpoja katika chama hicho, Mwenyekiti Tundu Lissu amewataka wanachama na viongozi wote kuungana kukijenga chama chao na kuepuka migawanyiko.
Lissu amesema uchaguzi mkuu wa chama hicho uliokwisha ulikuwa wa kihistoria na kuwezesha uongozi wao kukabidhiwa ofisi kwa amani.
“Kwa sababu ya uchaguzi wenyewe ulileta maneno mengi sana, tumevutana sana, tumesemana sana, mara nyingi hatukusifiana, tumezungumza yaliyo mabaya yetu.
“Sasa uchaguzi umepita, hiyo sababu iliyotufanya tuvutane imepita na imepita kwa namna ambayo nchi nzima inatusifia.
“Kwa hiyo kwa sababu tumefanya jambo la kihistoria, bado tuna sababu ya kuendelea kuvutana? Kunyoosheana vidole?” amehoji.
Ameongeza, “Tunarudi nyumbani, wote ni wa nyumba moja, palipobomoka tupajenge, palipopasuka tuparudishe wote. Tumeshinda wote, sasa huyu mtoto tumlee wote kwa sababu ni mtoto wetu. Tusikubali maneno ya “haya tutaona watafanyaje kazi.” Wote ni wa nyumba moja,” amsema.
Huku akirejelea hotuba ya aliyekuwa Rais wa Marekani, Abraham Lincoln aliyoitoa Machi 4, 1964 baada ya kushindwa urais, huku majimbo manne ya nchi hiyo yakijitenga naye na kuanzisha vita.
“Kwenye uapisho akahutubia akasema, “hatupaswi kuwa maadui, japokuwa yapo yaliyotuumiza, yanayotuunganisha yana nguvu kuliko yanatotutenganisha.”
Katika hatua nyingine, Lissu amesema uongozi wake utatenda kwa wanachama wote bila kujali waliomuunga mkono au wasiomuunga mkono.
“Sisi ni viongozi wa haki, nanyi mwajua haki huinua Taifa, hivyo haki itainua chama. Hatutaonea mtu na hatutakubali kuona mtu anaonewa. Tegemeeni mabadiliko kwa haki,” amesema.
Katika hilo, Makamu mwenyekiti Bara, Heche amesema uteuzi wa watendaji wa chama hicho utazingatia sifa na sio upendeleo.
“Uchaguzi umekwisha wanachama mtembee kifua mbele, hatutapendelea mtu eti kwa sababu ulituunga mkono. We will choose people on merits (tutachagua mtu kulingana na sifa).
“Hatutachagua watu kwa sababu ya uchawa. Eti una sifa halafu nisikupendekeze kwa sababu hukutuunga mkono, hiyo haipo,” amesema.
Amewataka wananchi wenye mapenzi mema na chama hicho kukiunga mkono chama hicho kwa hali zote.
“Naomba nikaribishe wote ambao sio wanachama wetu, niwakaribishe wajiunge na chama tunahitaji jeshi kubwa mara tatu ya tulilonalo. Kila mtu alete karama yake, talanta zake kwenye hii kazi tuliyonayo.
“Kuna watu wengi wanatuunga mkono, kama walikiwa wanasita kutusaidia, tunaomba watusaidie, walete misaada, mwenye kuleta kreti ya maji alete, mafuta alete. Hii kazi itafanyika kwa kila baraka ya kila Mtanzania anayeitakia mema nchi yetu,” amesema.
Sababu Mnyika kukabidhi ofisi
Lissu na viongozi wenzake walifika ofisi za makao makuu saa 5:00 na kulakiwa na Katibu Mkuu John Mnyika na kisha kufanya kikao kifupi kabola ya kuja kuzungumza na waandishi wa habari.
Akizungumza sababu ya Mwenyekiti mstaafu Freeman Mbowe kutokuwepo kukabidhi ofisi, Mnyika amesema kwa mujibu wa Katiba na kanuni za chama hicho, yeye ndye msimamizi mkuu wa ofisi.
“Kwa kuwa hakukuwa na mabadiliko ya katibu mkuu, mimi ndio nimewapokea mwenyekiti na makamu na viongozi wengine.
“Kwa katiba ya Chadema, mwenyekiti sio mtendaji, mtendaji ni katibu mkuu, mafaili yote anayo. Kwa hiyo hata Mwenyekiti hata angekuja ingekuwa ceremonial (kutimiza wajibu) tu,” amesema.
Ameongeza, “Hakuna kipindi cha mpito kwa katiba yetu, wala hakuna kuapishwa, hivyo Mbowe alishakabishi uenyekiti pale Mlimani City.”