Ni dhahiri kwamba Chama cha Mapinduzi (CCM) kimekamilisha mchakato wa kuwapata wagombea wake katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba, mwaka huu, ukiwa umefanyika mapema zaidi kuliko ilivyozoeleka.
Katika mkutano mkuu wa CCM uliofanyika uliofanyika Januari 18 na 19, mwaka huu, jijini Dodoma, wajumbe wa mkutano huo waliridhia kwa kauli moja kuwa Rais Samia Suluhu Hassan awe mgombea wa chama hicho katika nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wajumbe waliridhia pia Dk Emmanuel Nchimbi ambaye ni Katibu Mkuu wa CCM, kuwa mgombea mwenza wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huku Dk Hussein Mwinyi akiteuliwa kuwa mgombea urais wa Zanzibar.
Licha ya kwamba upitishaji wa wagombea haikuwa ajenda ya mkutano huo, lakini wajumbe walitoa hoja na viongozi wa mkutano huo wakiongozwa na mwenyekiti, Rais Samia, waliwasikiliza na hoja hiyo ikapitishwa kwa azimio maalumu la mkutano mkuu.
Namna mchakato huo ulivyoendeshwa umeibua maoni tofauti ya wadau wa demokrasia ambao baadhi yao wanaona uhuru na demokrasia ya kuchagua wagombea haikutolewa, huku wengine wakiona ni sahihi kwa kuwa waliopitisha azimio ni haohao wenye mamlaka hayo.
Hata hivyo, Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Stephen Wasira amefafanua kilichofanyika kwenye mkutano huo kwamba kilifuata katiba ya CCM na hakuna ukiukwaji wowote wa katiba au taratibu za chama.
Chanzo mabadiliko ya katiba
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Wakili Anna Henga anasema kinachowagharimu wanachama wa CCM ni mabadiliko ya katiba yao waliyofanya ambayo yanapoka uhuru wa nafasi hizo kushindanishwa.
“Inawezekana walifanya mabadiliko kwa kutokujua na kuitambua Katiba yao, lakini kwa ujumla demokrasia inakiukwa kuanzia kwenye katiba yao na taratibu za uchaguzi ambazo hazitoi nafasi wagombea zaidi ya mmoja,” anasema.
Anasema kuna wakati walifanya mabadiliko ya katiba yao na walio wengi wanajua kwamba anapopitisha mgombea kwa muhula wa kwanza, kwa muhula wa pili anakuwa yeye na hawekewi mshindani.
“Kiujumla katiba yao na taratibu zao za kiuchaguzi zina changamoto kama hawatabadilisha, hata akifika mwingine, mfumo utakuwa huohuo, labda wafanye mabadiliko kuanzia katika Katiba yao,” anasema.
Anasema kidemokrasia CCM kwa sasa inapitwa na vyama vingine vya upinzani kama Chadema na ACT Wazalendo kwani wamekuwa wawazi na michakato yao imekuwa inazingatia misingi ya haki.
Ni demokrasia ya aina yake
Mhadhiri wa sayansi ya siasa kutoka Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (Udsm), Dk Richard Mbunda anasema walichokifanya CCM kilikuwa na baraka ya kikao, hata kama kuna baadhi hawaridhiki lakini kuna demokrasia fulani imefanyika.
Anasema katika hali ya kawaida Mwinyi kwa upande wa Zanzibar anaendelea na uongozi na kwa utamaduni wa CCM, Rais anayeendelea muda wake siku zote huwa hashindanishwi na wagombea wengine.
“Nimewasikiliza wengi, kuna wanaodai ni uhuni umefanyika, demokrasia imepokwa au kuna watu wamenyimwa haki hasa wale waliokuwa wanataka kuchukua fomu, lakini lazima tujue kikao kilichofanya uamuzi ni sahihi,” anasema.
Anasema pamoja na mijadala yote ya lawama, kikao kilichopitisha ni halali na waliopitishwa walipitishwa kwa vigezo, ni watu waliotumikia nafasi zao na wamefanya vizuri, kwa mujibu wa wajumbe.
“Kwa mujibu wa CCM, Rais Samia amefanya vizuri katika kipindi cha miaka minne na wanadhani anastahili kupewa muhula mwingine wa kuongoza,” anasema.
Dk Mbunda anatolea mfano Marekani ambako Rais Joe Biden alitakiwa kuendelea kumalizia muhula wake wa pili lakini kutokana na umri wake, ikashindikana na dakika za mwisho akamteua makamu wake, Kamala Harris kugombea.
“Katika chama kilichopiga hatua kama Democrats, tulitegemea hizo hoja zingetoka, kwa nini ampendekeze makamu wake kugombea na kwa nini usingefanyika mchakato wanaohitaji nafasi waingie kupambana,” anasema.
Dk Mbunda anasema kama ni uhuni ulianza kufanywa na Democrats, kuliko hata uliofanywa na CCM. “Siwatetei, lakini Democrats walifanya uhuni mkubwa, Biden alijua hagombei kabisa, akasubiri dakika za mwisho kusema hagombei,” anasema.
Mtazamo huo unakinzana na uliotolewa na mchambuzi wa siasa, Bubelwa Kaiza anasema utaratibu wa kuteua wagombea nafasi ya urais upo kisheria na kikatiba na hata katika vyama vya siasa.
“Walichokifanya CCM hakikuwa sahihi, kwanza utaratibu uliozoeleka kwa ni kiwango kikubwa, watu wa kwenye vyama wanashindana na kunakuwa na ajenda inatangazwa tangu mwanzo na inaeleweka na watu wanajadili,” anasema.
Kaiza anasema katika mkutano ule, ajenda ya CCM ilikuwa ni kumchagua makamu wa mwenyekiti wa Tanzania Bara na kujadili taarifa ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi, lakini ghafla walileta hoja nyingine ambayo haikuwepo.
“Sasa huwezi kupata kiongozi wa nchi anayeheshimika na kusimamia maslahi ya Taifa anayepatikana kwa kuteuliwa kutoka uchochoroni, wamekosea sana,” anasema.
Kaiza anasema hata sheria na Katiba yao ibara ya 102 ibara (1)B inayoelekeza namna mgombea wa nafasi ya urais anavyotakiwa kuteuliwa hawajaifuata.
“Sasa wanaanza kuzungumza chama chetu na wajumbe ni wale wale lakini kimsingi ni uswahili umetumika, nafikiri wamekata tamaa, lakini inaonekana kuna mgongano ndani ya CCM na wanafanya ujanja ujanja,” anasema.
Kaiza anasema athari ya kitendo hicho kwanza wanaanza kuvunja sheria kabla ya kuingia kwenye uchaguzi wenyewe na matokea yake anatamani hata Tume ya Uchaguzi impendelee.
“Atapenda kushinda bila kupingwa na kimsingi si mtu anayefahamu kuwa kiongozi kwa kuwa anakosa umahiri wa kushindana na wengine,” anasema.
Mchambuzi wa masuala ya siasa Zanzibar, Ali Makame anasema uamuzi uliofanywa na CCM ulikuwa wenye busara kwa aina ya mkutano wenyewe, lakini jamii imepokea kwa hisia tofauti.
“Kuna baadhi wanataka kwenda mahakamani kupinga uamuzi huo na wanatafuta kuungwa mkono na wenzao, ndiyo maana nasema uamuzi ulikuwa sahihi lakini wengine wamepokea tofauti kwa kuamini demokrasia inaanza kufa ndani ya CCM,” anasema Makame.
“Ukweli usemwe, CCM ni chama kikubwa, viongozi waliopo wamefanya makubwa kwa kutekeleza ilani ya uchaguzi zaidi ya ilivyotakiwa, leo kuna haja gani ya kukimbiza kupitisha uamuzi kama huo,” anasema.
Makame anasema wakati wanatangaza ajenda ya mkutano unaoenda kufanyika hawakusema na wanapaswa kufahamu CCM ina zaidi ya wanachama milioni 13 na waliokwenda kwenye mkutano mkuu walikuwa wajumbe takribani 2,000.
“Ingekuwa jambo la busara kwa sababu uongozi uliopo unajiamini wamefanya vizuri ili kuipa nafasi demokrasia hata ingekuwa katika ule mkutano mkuu wangetoa nafasi hata kwa siku moja kwa anayetaka kugombea achukue fomu,” anasema.
Anasema anaamini kweli wangeshinda waliopo, lakini yale maneno ya pembeni yasingekuwepo, huku akieleza walitegemea demokrasia inakuwa na utekelezaji wa ilani unafanyika inakuwaje demokrasi inapindishwa.
“Demokrasia ni sawasawa na maji, yanapita katika njia yake, ikiwa unayazuia yatatafuta njia nyingine kupita sasa, kiukweli uamuzi wa CCM ni mzuri, lakini yanatafsiriwa tofauti kwamba tunakoelekea demokrasia inapindishwa,” anasema.
Hakukuwa na ushirikishwaji
Mkurugenzi wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa anasema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inataka watu wote washirikishwe katika mambo ya msingi na anayetaka kugombea lazima apitie kwenye chama.
“Watanzania hawana njia nyingine ya kidemokrasia ya kugombea bila kupitia kwenye vyama na michakato ya ndani lazima itoe nafasi sawa kwa wanachama kushiriki katika nafasi za kugombea,” anasema.
Onesmo anasema mchakato wa CCM uliofanyika Dodoma ni wazi mambo ya ushirikishwaji yalirukwa ambayo yanaleta maswali mengi kuhusu hatima ya demokrasia katika chama hicho.
“Kimsingi michakato ya CCM pamoja na kwamba wanafanya kwa mujibu wa Katiba yao ina changamoto nyingi ya kidemokrasia katika kuwapa wanachama wao nafasi ya kushindana na kuamua nani anaweza kuwa kiongozi wao,” anasema.
Katika maelezo yake, anasema michakato yao mingi katika jicho la kidemokrasia inakanyagwa: “Ni jukumu la wanasheria, waandishi, wanaCCM na wadau kushauri warudi kwenye misingi kutoa haki ya kapata viongozi kwa misingi shirikishi,” anasema.
Onesmo anasema CCM ni chama kikongwe na kina watu wabobevu na kina hazina ya wengi wenye ubobevu wanapaswa kufanya mambo kwa kuzingatia haki na shirikishi.
“Mambo yanayofanyika sasa tulitegemea yafanywe na vyama vidogo ambavyo unakuta hata watu wakushinda hakuna, kufanya michakato ya kupitisha jina moja inakuwa haina afya,”anasema.
Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Stephen Wasira anasema uamuzi wa mkutano mkuu maalumu wa CCM, uliomchagua Rais Samia kugombea kiti cha urais wa Serikali ya Tanzania, umezingatia takwa la kikatiba na mamlaka ya mkutano mkuu.
“Baada ya kutambua kazi kubwa iliyofanywa na serikali zote mbili, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar, mkutano mkuu wa CCM ukasema kama hali ndiyo hii, kuna haja gani ya kuchelewesha kutangaza mgombea,” anasema Wasira.
Anasema kuna baadhi ya watu wanadai ni wanaCCM na hawakuelewa lakini si jambo la ajabu kwao bali watawasaidia kuwaelimisha waelewe.
“Watu wote hawawezi kuelewa sawa, lakini tunawaambia mkutano mkuu kwa mujibu wa Katiba hii, ni kikao cha mwisho na ukisoma mle unaona mkutano mkuu una mamlaka ya kubadili, kufuta au kurekebisha uamuzi wowote uliofanywa na kikao cha chini yake,” anasema.
Wasira anafafanua kwamba mkutano huo una uwezo wa kufuta uamuzi uliofanywa na kiongozi yeyote katika chama hicho kwa kuwa unawakilisha wanachama.
“CCM ni chama cha wanachama, wawakilishi wenu walipokutana na kukubaliana na kuridhika, walitumia mamlaka ya mkutano mkuu kwa kusema tutampa Samia mitano tena, huo ni uamuzi wa mkutano mkuu sasa, kama huelewi,” anasema.
Katika mkutano huo walikutana kwa dharura baada ya kutumwa na wakubwa zao kwamba wazungumze kwa kuondoa vikwazo vinavyozuia mkutano mkuu walifanya hivyo na kamati Kuu ya Zanzibar ilikutana na kumkubali Mwinyi.
“Mwenye mashaka na jambo hili, kama kote ameshindwa, basi aje kwangu nitamsaidia, maana katiba hii iko kichwani kwangu na uamuzi tuliufanya kwa kuzingatia ibara ya 101 inayotutaka kuchagua jina moja la kuwa mgombea katika kiti cha urais, tulitumia kigezo hicho,” anasema.