SIMBA ilikuwa na ofa sita mezani kutoka timu tofauti zikihitaji wachezaji wake dirisha dogo la usajili lililofungwa Januari 15, 2025 lakini kati ya hizo, ni mbili tu ambazo ilizikubali na nne ikazipiga chini kutokana na sababu mbili.
Vinara hao wa Ligi Kuu Bara, wana sababu zao walizozianisha ambazo zimewafanya mastaa wake wanne kubaki kikosini hapo licha ya kwamba kulikuwa na ofa mezani zinajadiliwa.
Sababu ya kwanza ni masharti magumu ambayo Simba ilizipa timu zilizowafuata mezani kuuliza uwezekano wa kusajili wachezaji hao lakini ya pili ni mapendekezo ya kocha mkuu wa kikosi hicho, Fadlu Davids ambaye uongozi wa timu hiyo umempa mamlaka makubwa ya kimaamuzi kuhusu kikosi chake.
Kati ya ofa hizo sita, nne zilikuwa ni za kuwaomba kwa mkopo wachezaji wake wanne ambao wamekuwa hawapati nafasi katika kikosi cha kwanza ambao ni makipa Hussein Abel na Ally Feruzi, winga Salehe Karabaka na beki Hussein Kazi huku mbili zikiwa ni za kuwanunua moja kwa moja washambuliaji wake wawili, Leonel Ateba na Edwin Balua.
Ni wachezaji wawili tu kati ya hao ambao Simba iliwaruhusu kuondoka tena kwa mkopo ambao ni Karabaka aliyetua Namungo FC na Feruzi aliyeenda Kagera Sugar huku Abel na Kazi wakibaki klabuni huku chanzo cha ndani kutoka Simba kikifichua timu zilizowahitaji hazikuweza kutimiza masharti ambayo zilipewa, pia kuna maelekezo ambayo kocha Fadlu aliyatoa ili kuruhusu wachezaji hao kuondoka.
“Timu zote ambazo ziliwataka wachezaji wetu kwa mkopo tulizipa masharti ya kulipa mshahara wote kwa mchezaji kila mwezi kwa muda ambao atacheza hadi mkopo utakapomalizika lakini pia watuhakikishie watawapa nafasi ya kutosha ya kucheza hao wachezaji.
“Hao tuliowatoa ni wale ambao timu zilizowachukua zimekubali kutimiza masharti hayo tuliyowapa. Kuhusu Hussein Kazi kocha alishauri tuhakikishe tunapata mbadala wake kabla hatujamtoa kwa mkopo kwa vile angeondoka tungebaki na mabeki watatu tu wa kati na hatukufanikiwa katika hilo ndiyo maana alibakia ila naye alikuwa na ofa za kuhitajiwa,” kilifichua chanzo hicho.
Gazeti hili linafahamu kuwa kipa Hussein Abel alihitajika na Coastal Union lakini ilishindwa kufikia makubaliano na Simba katika dakika za mwisho jambo lililosababisha timu hiyo ya Tanga kuamua kumsajili Aron Kalambo kutoka Geita Gold.
Kulikuwa na ofa mbili kutoka timu mbili tofauti za Libya zikiwahitaji washambuliaji Edwin Balua na Leonel Ateba lakini Simba ilizitupa kutokana na kutoridhishwa na ofa zilizowekwa mezani na kutokuwa na uhakika wa kupata wachezaji mbadala wa wachezaji hao kama.
“Kuna timu ya Libya ilitaka kutoa Dola 100,000 (Sh253 milioni) kwa ajili ya Balua na nyingine ilitaka kumnunua Ateba kwa Dola 150,000 (Sh379.6 milioni) lakini hizo ni fedha kidogo na zisingetosha kusajili mastraika wa kueleweka katika dirisha dogo.
“Pia Karabaka ameondoka hivyo kama Balua naye angeondoka maana yake kocha angebaki na machaguo machache katika winga kama ambavyo ingekuwa katika nafasi ya mshambuliaji wa kati ambapo tungebaki na Mukwala (Steven) na Valentino Mashaka ambaye amekuwa akisumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara,” kilisema chanzo hicho.