Jicho la Msuva, Himid wanavyoitazama AFCON 2025

KATIKA droo ya upangaji makundi ya michuano ya Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) itakayofanyika Morocco kuanzia Desemba 21, 2025 hadi Januari 18, 2026, Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ itakuwa kundi C.

Droo hiyo iliyofanyika Januari 27, 2025 jijini Rabat nchini Morocco, Taifa Stars imepangwa na timu za Nigeria, Tunisia na Uganda.

Kufuatia droo hiyo, nyota kadhaa wa Taifa Stars wamezungumzia ushindani utakaokuwepo na kile walichojifunza katika AFCON ya mwisho walioyoshiriki mwaka 2023 nchini Ivory Coast.

Simon Msuva aliyeshiriki AFCON ya 2019 nchini Misri na 2023 pale Ivori Coast, amesema: “Hakuna onyonge, tumepangwa na timu kubwa, lakini sisi kama wachezaji tunajua kabisa kuwa soka ni mchezo ambao mafanikio yake yapo katika  maandalizi na juhudi.”

Msuva aliyefunga bao pekee katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Guinea ulioifanya Stars kufuzu AFCON 2025 kwenye mchezo wa mwisho, alisisitiza kuwa Tanzania ina wachezaji wenye uwezo na kiwango cha kimataifa kinachoweza kuleta matokeo mazuri katika fainali hizo.

“Tunahitaji kujiandaa vizuri na kuhakikisha kila mmoja anatoa kile kilicho bora ndani yake.

“Kwa upande wetu, hatuwezi kujali majina ya wapinzani wetu. Tunahitaji kujielekeza kwenye maandalizi yetu na kuwa na umoja kama timu,” amesema nyota huyo wa Al-Talaba SC ya Baghdad.

Msuva ameongeza kwamba, uzoefu wake wa kushiriki AFCON mbili pamoja na wachezaji wengine utasaidia katika kuhamasisha vijana kupambana na kuleta matokeo mazuri.

“Tuna uzoefu wa kutosha, katika kila mechi tutajitahidi kupata matokeo bora. Mchezo wa soka ni vita ya mawazo, tunahitaji kuwa na imani,” amesema.

Naye kiungo mkabaji Himid Mao anayecheza Talaea El Gaish ya Misri, amesema wachezaji wengi wa Tanzania wanahitaji kuwa na umoja na kupambana pamoja ili kufikia mafanikio makubwa.

“Tuna uwezo wa kushindana na timu kubwa, tukifanya kazi kwa pamoja tunaweza kufika mbali,” amesema Mao.

Miano van den Bos, mwenye umri wa miaka 21, ambaye kwa sasa anacheza soka huko Sweden na timu ya Örebro Syr, alisema michuano ya AFCON iliyopita ilimsaidia kujijua zaidi na kuwa na mtazamo mzuri kwa ajili ya michuano inayokuja.

“Mimi ni mchezaji mwenye dhamira ya kujituma, na nashukuru kuwa na nafasi ya kuonyesha uwezo wangu kwenye uwanja wa kimataifa, pamoja na kupangwa na mataifa makubwa tuna nafasi ya kuishangaza Afrika, kikubwa ni maandalizi tu,” amesema Van den Bos ambaye katika AFCON 2023 alikuwepo benchi mechi mbili za kwanza Kundi F dhidi ya Morocco na Zambia.

Kwa mujibu wa ratiba ya AFCON 2025, Taifa Stars itafungua dimba kwa kucheza na Nigeria, Desemba 23 katika Uwanja wa Fez, kisha Desemba 27 itakabiliana na Uganda katika Uwanja wa Al Barid, Rabat na mechi ya mwisho itakuwa ni dhidi ya Tunisia, Desemba 30.

Taifa Stars inakwenda kushiriki AFCON 2025 kwa mara ya nne baada ya kufanya hivyo mwaka 1980 (Nigeria), 2019 (Misri) na 2023 (Ivory Coast).

Katika AFCON ya 2019, ndiyo pekee ambayo Stars iliondoka bila ya pointi lakini 1980 ilipata pointi moja na 2023 pointi 2 ingawa mara zote imeishia hatua ya makundi.

Related Posts