Fyatu asiye adabu aliniuliza ni kwa nini sikuwafyatua Chakudema wakati wa nchakato wao. Nilimjibu kuwa sikuwa na papara. Nilingoja nione ambavyo wangefyatuana, kuchakachuana, au kuchaguana. Japo si shabiki wa siasa za majitaka na mizengwe, nimeridhika na namna Chakudema, tofauti na wenzao, walivyoonyesha ukomavu na ukakamavu vilivyobainisha ukweli na uwazi katika nchakato uliokwisha karibuni. Kongoleni.
Yule fyatu alidai kuwa Chakudema wangezengua na kufyatuana japokuwa, kabla ya kuhitimisha, walivuana nguo bila sababu za msingi halafu wakasema hiyo ni demokrasia wakati ni ghasia! Hayo tuyaache. Leo nitalinganisha uchaguzi na uchakachuaji.
Wakati wenzao wakipitishana kwa kufyatuana–sijui waliogopa nini wakati twaambiwa wanafaa– Chakudema wameonyesha demokrasia kama jina lao. Walijitenga na mizengwe, mizinguano, ubabaishaji na ubangaizaji kisiasa. Sasa Freemani kabwagwa. Tutegemee matunda au matundu ya kuibuka kwa Tunda Lishe na genge lake? Je, mfupa uliomshinda fisi, dogi atauweza? Tulisikia waliojisifu kutumia njuluku zao kuendesha chama kana kwamba hawakuwa wakifyatua ruzuku. Je, huyu Tunda atatia tundu fuko lake lisilo na njuluku kuendesha chata ua michosho tu? Je, ni kweli baadhi ya vyama vinaendeshwa kwa njuluku za wanene wake au hisani na michango ya wanachama?
Je, ruzuku ilikuwa ikienda wapi na kufanya kazi gani tukiwa wakweli? Je, wahusika walitegemea kurejesha njuluku zao vipi au kutegemea nini? Mbona kuna vyama vingi vya mfukoni vinavyotupiwa makombo na wenye ulaji viwaunge mkono wanapofyatua kaya?
Upande wa pili, fyatu mmoja mkumbaff anadai wameonyesha ufyatuaji na ufyatuzi, na woga visivyo kifani kinomi. Aliwasikitikia mafyatu wanaoumezea mate unene. Kwani, hawapo japo wanajifanya hawapo na wamekubali yaishe huku viroho vikiwachonyota na kuwanyotoka?
Hili fyatu lilidai kuwa, kwenye walioshika patamu, inakuwaje mafyatu wanafyatuliwa hadi wanapitishana bila kushindana na kupingana japo kwa chati wakifyatuliwa badala ya kufyatua? Je, hili siyo pigo kwa demokrasia hata kama mambo ya Ngoswe tukimuachia Ngoswe mwenyewe? Nani alitegemea wanene kugoma kuchujwa?
Liliongeza kuwa hakuna cha mambo ya Ngoswe. Kwani, wanaopitishwa bila kupingwa au kuogopa kuchapwa, wanadhamiria kutawala kaya yetu. Mafyatu walioonyesha dhahiri woga wakashindwa kutenda demokrasia ndani ya chata lao wanaweza kuleta demokrasia ya kweli kayani? Wanaweza kuwatendea haki mafyatu na washindani wao? Yote juu ya nini? Kukosekana katiba mpya.
Mafyatu wanaogwaya ushindani, wanaweza kusimamia uchaguzi huru au uchakachuaji kama ada? Tutegemee tena ujiwe kwenye uchakachuaji, sorry, uchaguzi ujao? Nani kasahau rafu iliyochezwa kwenye ule uliopita ambapo wapingaji walienguliwa mchana kweupe tena bila chembe ya aibu? Kuna kipindi natamani kaya yetu isifanye uchakachuaji. Tutangaze umswati yaishe tusizinguane na kufyatuana kama hamnazo. Kwani, kunatupoteza njuluku na muda bila sababu zozote za msingi. Kwa nini wateule wasipitishwe moja kwa moja tukaepuka hasara hii? Maana, kuna kipindi unajua matokeo hata kabla ya uchakachuaji wenyewe kufanyika. Haiwezekani wala kuingia akilini ngurumbili, hata wawe wa chata moja, kuwa na mawazo na msimamo mmoja.
Lazima iwepo mizengwe ikizingatia uzuri wa unene na ulaji wa dezo vimpavyo ufalme na uungu mwenye navyo. Inakuwakuwaje wengine wanafyatuana na kuchaguana wakati wengine wakifyatuliwa na kuzenguana? Hapa sababu ni ujikombaji, uchawa, ukunguni, unafiki, au uchumia tumbo au woga? Maana, ukipingana na wanene, wanakunyima ulaji na kukutangaza adui wa kutengwa na kulaaniwa. Hivyo, kama vyura, wanasema ‘apite, apite’ hata wamaanishapo na kutamani asipite.
Kwa mafamba, ubabaishaji, ufyatuzi, ufyatuliwaji, na uhovyo huu, tunaweza kufanya mabadiliko na kuleta maendeleo na uwajibikaji vya kweli? Kwa anayejua hali ilivyo katika lindi la utekanaji, na upigaji anashangaa, kustuka, na kusikitika asijue la kufanya. Uchaguzi, si uchakachuaji na ufyatuaji hujikita kwenye mashindano ya mipango na sera. Katika kupitishana bila kupingwa wala kupingana na kugomea ‘kuchapwa’, sikusikia neno sera likitamkwa hata mara moja. Je, kuna ka woga kanatembea? Kama mafyatu wa chata na genge moja wanaogopana na kutoaminiana wakashindwa kujitokeza kuwapinga wateule kwa mujibu wa demokrasia, huu woga utaepukwa kwenye uchakachuaji ujao? Kama utakuwapo, wapingaji wataambua kitu kweli? Je, wapingaji na wapenda demokrasia wanajiuliza swali hili kuu na muhimu?
Kwa vile sipendi kuachia ulaji, kwenye Chama cha Madikodiko (CcM), kama walivyofanya akina profedheha Pumba, meku Lyatongolwa na bwana mafedheha Cheeeyo, sitaitisha uchaguzi wa mkiti. Nitakalia kiti hadi nirejeshe namba. Si inapendeza? Sitafanya ‘ujinga’ kama ya akina Freemani. Napenda ulaji kwa gharama na namna yoyote kama bibie. Kwangu, ulaji na unene siyo wa kuachia hata kwa viboko.
Kwa vile mafyatu wangu wamefyatuliwa hadi wakafyata, lazima niwafyatue nibakie kileleni na kuwakoga. Atakayethubutu kunipinga au kutaka kunichapa, namteka au kumtekesha na kumpoteza. Au siyo?
Nimalize kwa kuwapongeza wote waliomaliza uchaguzi na ufyatuaji kwa kujionyesha sura zao halisi.
Hivi leo nimeongelea nini na kulenga nini? Hii mibangi na gongo, itakuja kusababisha nitekwe bure.